NA BAADA YA LILE TONGE, SHETANI AKAMWINGIA.

NA BAADA YA LILE TONGE, SHETANI AKAMWINGIA.

Shalom, leo tutajifunza madhara ambayo tunaweza kuyapata pale tunapoukataa  ule upendo wa mwisho kabisa wa Yesu Kristo.

Yuda alikuwa ni mtume wa Yesu, lakini kama tunavyojua habari yake, alikuwa mwizi, na pia hakuwa na upendo  wa dhati kwa Bwana.. Tunaona katika biblia hali hiyo ya uasi aliendelea nayo kwa muda mrefu sana, lakini katika kipindi hicho chote haikuleta madhara yoyote katika maisha yake, aliendelea kutembea na Yesu, aliendelea kushiriki baraka zote za Yesu kama mmojawapo wa mitume wengine..

Mpaka anafikia hatua ya kwenda kupatana na wakuu wa makuhani ili kumsaliti Yesu bado,  nafasi alikuwa nayo ya kuahirisha mawazo yake, uwezo huo alikuwa nao, isitoshe alikuwa anaona Yesu akimpa viashiria vingi kuwa anavyovifanya anaweza kuviahirisha, lakini hilo halikumwingia moyoni mwake. Mpaka siku ile walipokuwa wameketi chakulani jioni na Yesu akaanza kuwatawadha miguu, kuonyesha upendo wake kwao, akamtawadha na Yuda miguu yake, huku Yuda akiyatazama macho ya Emanueli yenye upole, yasiyo na kosa lolote, akisikia kabisa rohoni anashuhudiwa kuwa anachojaribu kukifanya sicho sawa..aghahiri mawazo yake, haoni mpaka Bwana wake amekuja kumuosha miguu yake, kumthibitishia kuwa miguu yake haitakiwi kuwa myepesi kukimbilia maovu.. Lakini hilo halikuwa kitu kwa Yuda.

Mpaka dakika ya mwisho kabisa tuona Kristo anaonyesha Upendo wake wa mwisho, wa kuchukua chakula chake cha heshima na kumgawia Yuda peke yake, kama heshima ya kipekee, tusome;

Yohana 13:21 “Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti.

22 Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye.

23 Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda.

24 Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye?

25 Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani?

26 Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote.

27 NA BAADA YA HILO TONGE SHETANI ALIMWINGIA. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi.

28 Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo.

29 Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu.

30 Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku”.

Sasa Tonge sio ule mkate wa Pasaka, au sio ule mkate aliowapa wanafunzi wake kama mwili wake waule siku ile, hapana, Tonge ni chakula cha heshima kilichokuwa kinaandaliwa na wayahudi zamani, ambacho   kinaweza kikawa na mkate au kitu kingine, lakini sana sana kilitumika mkate, ambacho hicho mtu alikuwa anampa Yule mtu anayemuheshimu sana, au wa muhimu kwake, ili kuinyesha thamani yake.  Hivyo aliyeuandaa aliuchua mkate huo na kuuchovya katika mboga iliyoandaliwa pamoja na huyo mtu aliyemwandalia.

Utaliona Hilo katika kipindi cha Ruthu, alivyoitwa na Boazi kwake..

Ruthu 2:14 “Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza”.

Soma pia Ayubu 31:16, na Mithali 23:6, utaliona neno hilo.

Sasa alichokifanya Bwana ndicho hichi, kumpa Yuda heshima ya kipekee, wa kuchovya donge lake pamoja naye,. Kuonyesha upendo wake wa kipekee kwake.

Lakini mara baada ya kula tu, angali moyo wake bado hujaiacha nia ya kumsaliti   biblia inatuambia shetani akamwingia saa hiyo hiyo …Akawa amefikia “point of no return”. Hii Ikiwa na maana kuwa sasa shetani anayo nafasi ya kumchukua huyu mtu asilimia 100, anaweza kumwendesha kwa jinsi anavyotaka, (amepata hati miliki maalumu) na ndio hapo utaona akawaendea wale makuhani na kuwapa mikakati yote ya kumkamata Yesu. Na Mwisho wa siku yeye mwenyewe akajiua, kwasababu tayari alikuwa ameshavaliwa na pepo mkuu mwenyewe ibilisi.

Na sisi vivyo hivyo, Kristo anapotuonyesha upendo wake kwetu, na hatuoni jambo lolote baya likitokea kwenye maisha yetu pale tunapofanya dhambi kwa makusudi, pengine unazini na upo kanisani, na huoni jambo lolote baya likikutokea, na saa nyingine unamwomba Yesu akutendee jambo Fulani na anakutendea, na wewe unadhani itaendelea hivyo hivyo kila siku..

Upo wakati atakuonyesha upendo mkubwa zaidi ya huo, (atakumegea Tonge lake) na kama usipojua nini maana ya Upendo huo kwamba  anakutaka wewe utubu, wewe ukadhani anafurahishwa na unachokifanya, na ndio maana kukubariki, ujue tayari mwisho wako umefika. Ibilisi anakuingia na hapo ndipo unapokuwa mwisho wako.

Hivyo tusipumbazwe na rehema za Kristo. Tukiona hatuadhibiwi kwa makosa yetu, tuogope kwasababu utafika wakati tutakabidhiwa shetani moja kwa moja.

Bwana akubariki.

Hizi ni nyakati za mwisho Je! Umeokoka? Je! Umepokea Roho Mtakatifu. Kumbuka Yesu ndio mwokozi wa ulimwengu. NA HUO NDIO UKWELI PEKEE ULIODUMU DUNIANI KWA WAKATI WOTE.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

BIRIKA LA SILOAMU.

Sikukuu ya kutabaruku ni ipi?

KWANINI NI YESU KRISTO WA NAZARETI?

CHAPA YA MNYAMA

MTUMWA SI MKUU KULIKO BWANA WAKE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Fransis
Fransis
2 years ago

Shalom? Ninajengwa sana na pia nafurahia mafundisho yenu sana. Naomba msaada wa maswali yangu mawili tofauti. (1) JE, NI SAWA KWA MWAMINI KUNYWA POMBE (ALIYEOKOKA AU ASIYEOKOKA, IKIWA TUU ANAMKIRI KRISTO KAMA MWANA WA MUNGU NA MWOKOZI). (2) KUHUSU FUNGU LA KUMI KWA KANISA NI SAWA?

Jackson Mkwasa
Jackson Mkwasa
2 years ago

Tuzidi kumsifu bwana wetu YESU KRISTO

Cathy
Cathy
2 years ago

Asante kwa ufafanuzi huu, maana wengi hudhani ‘tonge’ ni sehemu ya mkate walioshiriki wote 12.

Bwana awabariki.