Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia (Neno la Mungu wetu) lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105).
Biblia inasema katika kitabu cha Yakobo…
Yakobo 4:17 “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi”
Kumbe haihitaji kwenda kuua, au kuiba, au kuzini ndipo ihesabike kuwa ni dhambi, bali hata “kujua tu kitu kilicho sahihi na kutokukifanya hicho” tayari ni dhambi mbele za Mungu!!!. Hii inaogopesha sana!!.
Ukijua kuwa unapaswa umtumikie Mungu, halafu humtumikii hiyo tayari inahesabika kuwa ni dhambi.
Ukijua kuwa unapaswa Uwe mwombaji, halafu hauombi hiyo tayari kwako ni dhambi.. Na watenda dhambi wote hawataurithi uzima wa milele, kulingana na maandiko.
Ukijua kwamba unapaswa uwe unawaombea wengine, halafu hufanyi hivyo, aidha kwasababu ya chuki au vinyongo au hasira, fahamu kuwa unatenda dhambi..
1Samweli 12:23 “Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi..”
Ukijua kuwa unapaswa uhubirie wengine habari njema za wokovu, wawe kama wewe, na hufanyi hivyo, basi fahamu kuwa unafanya dhambi!. Na watenda dhambi wote ni wana wa ibilisi na hawataurithi uzima wa milele.
1Yohana 3: 8 “Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi”.
Ukijua kuwa unapaswa ukabatizwe na hautaki kubatizwa au unapuuzia ubatizo, basi fahamu kuwa unafanya dhambi kulingana na andiko hilo “yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi”.
Ukijua kabisa kwamba unapaswa “ulisome Neno (yaani biblia)”, lakini hufanyi hivyo, kwa visingizio Fulani fulani.. Fahamu kuwa unatenda dhambi, na wewe ni muasi kulingana na biblia.
1Yohana 3:4 “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi”.
Ukijua kuwa unapaswa ufanye ibada na kukusanyika na wengine kanisani, kumfanyia Mungu ibada kulingana Waebrania 10:25, lakini wewe hufanyi hivyo, badala yake unabaki nyumbani umelala, au unaenda kufanya shughuli zako nyingine, basi fahamu kuwa unafanya dhambi..
Waebrania 10:25 “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”
Kaka/Dada usilipuuzie kamwe Neno la Mungu,..Unaposikia maonyo ya Neno la Mungu, usiyasikilize tu kama taarifa ya habari, na kuyaacha yapite, au kuyaweza akiba moyoni, bali yafanyie kazi kuanzia wakati ule ule unapoyasikia.. Kwasababu usipoyafanyia kazi baada ya kuyasikiliza basi kwako inahesabika kuwa dhambi, na hivyo utahukumiwa sana siku ile, Bwana Yesu alisema maneno yafuatayo..
Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana”
Jiepushe na hukumu ya Mungu!!, Litendee kazi Neno baada ya kulisikia.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.
JE UNA MATUMAINI YA KUPATA TENA KILE ULICHOPOTEZA?
IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.
About the author