MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA

SWALI 01: Je wakristo tunaruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja?

Jibu: Kwa mujibu wa biblia, Ndoa ya kikristo ni ya mke mmoja na mume mmoja.

Marko 10:6 “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.

7 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;

8 na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja”.

SWALI 02: Je kama mtu alifunga ndoa ya kiserikali, au kimila ndoa hiyo inatambulika mbinguni?..Yaani Mungu anawatambua kama ni mume na mke kihalali?.

Jibu: Ndio! Mbinguni watu hao wanatambulika kama ni mke na mume, ingawa ndoa yao haitakuwa ndoa takatifu ya kikristo..maana yake kuna mambo hawataweza kuyafanya wakiwa katika hiyo hali, mfano wa mambo hayo ni Uchungaji wa kundi, au Uaskofu au Ushemasi. Kwasababu nafasi hizo ni za kuhubiria wengine njia sahihi, hivyo haiwezekani mtu awahubirie wengine wafunge ndoa takatifu ya kikristo wakati yeye mwenyewe hayupo katika ndoa kama hiyo. (Atakuwa mnafiki).(Tito 1:6-7).

Hivyo ni sharti aibariki ndoa yake hiyo na kuwa ndoa takatifu ya kikristo ili asifungwe na baadhi ya mambo.

Mfano wa ndio hizi ambazo ni za kipagani lakini Mungu alikuwa anazitazama ni kama ile ya Herode ambayo Yohana mbatizaji aliikemea.

Marko 6:17 “Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;

18 kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo”.

Herode hakuwa mkristo lakini alipomwacha tu mke wake na kwenda kumchukua wa ndugu yake ikawa ni chukizo mbele za Bwana, na vivyo hivyo ndio zote zilizofungwa ambazo zimehusisha mahari pamoja na makubaliano pande zote, basi ndio hizo Mungu anazitazama na zinapaswa pia ziheshimiwe.

SWALI 03: Je Wakristo tunaruhusiwa kutoa talaka?

Jibu: Wakristo hawaruhusiwi kuachana baada ya kuoana. Kwahiyo talaka hairuhusiwi katika ndoa ya kikristo wala mwanaume haruhusiwi kumwacha mke wake katika hali yoyote ile ya udhaifu wa kimwili.

Luka 16:18 “Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini”

SWALI 04: Je! Kama Mwanamke alikuwa ameolewa na mwanaume ambaye tayari alikuwa na Mke, je anapookoka anapaswa amwache huyo mume wake au aendelee naye?.

Jibu: Kulingana na maandiko anapaswa amwache kwasababu tayari huyo alikuwa ni mume wa mtu, hivyo ili maisha yake yawe na ushuhuda na aishi kulingana na Neno ni lazima amwache huyo na akaolewe na mwanaume mwingine ambaye hajaoa (lakini katika Bwana tu), au akae kama alivyo.

SWALI 05: Kama mwanaume alikuwa ameoa wanawake wawili na kashaishi nao muda mrefu na kuzaa nao watoto, lakini ukafika wakati akaokoka je anapaswa amwache mmoja na kuendelea na mwingine au?

Jibu: Kama mwanaume alikuwa amemwoa mwanamke wa kwanza katika ndoa ya kikristo (yaani iliyofungishwa kanisani), na baada ya ndoa hiyo akaongeza mwingine wa pili…Na baadaye akatubu na kuokoka upya!. Hapo hana budi kumwacha huyo wa pili kwasababu alikuwa anafanya uzinzi kulingana na biblia, haijalishi ameishi na huyo mwanamke kwa miaka mingapi, na amepata naye watoto wangapi..anapaswa amwache na kubaki na mke wake wa kwanza.

Lakini kama alimwoa mke wa kwanza kipagani na kulingana na sheria za kipagani akaongeza wa pili, na  akaishi nao muda mrefu na wanawake hao wote wawili bado wanahitaji kukaa naye, hapaswi kuwaacha labda mmoja wapo wa wanawake hao aridhie mwenyewe kumwacha kwa hiari yake..

Lakini kama ataendelea kubaki nao mtu huyo ndoa yake hiyo ya wake wawili haitawezi kubarikiwa kanisani, na pia yeye mwenyewe hataweza kuwa Mchungaji, askofu au Mwinjilisti au shemasi bali atakuwa muumini wa kawaida tu, kwasababu biblia inasema ni lazima Askofu awe mume wa mke mmoja..

Tito 1:6 “ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii.

7 Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu”.

SWALI 06: Je?.Kujifungua kwa operation au kuzalishwa na wakunga wakiume ni halali kwa mwanandoa wa kikristo?.

Jibu: Operesheni ni njia mbadala ya kukiondoa kiumbe tumboni ili kusalimisha maisha ya mama na mtoto..Hivyo kibibla sio dhambi, kwasababu lengo lake ni kuokoa maisha na si lengo lingine.

Vile vile kuzalishwa na mkunga wa jinsia ya kiume si dhambi, kwasababu lengo ni lile lile kusaidia kuokoa maisha,..Katika eneo la uokozi ni eneo ambalo haliangalii jinsia..

Kwasababu pia zipo operesheni kubwa zaidi hata za kuzalisha ambazo zinahusisha kuondoa au kurekebusha viungo vya ndani kabisa vya uzazi wa mwanamke au mwanaume, ambazo operesheni hizo madaktari wake bingwa wanakuwa ni wa jinsia tofauti na wanaofanyiwa, hivyo hapo kama mtu anataka kupona kwa njia hiyo ya matibabu basi hana uchaguzi, wa atakayemfanyia hiyo operesheni.

Kwahiyo katika mazingira kama hayo, jinsia yoyote itakayotumika kumfanyia matibabu huyo mgonjwa wa kikristo, itakuwa si dhambi kwa mkristo huyo anauefanyiwa hiyo operesheni wala kwa yule anayemfanyia.

Shalom.

Usikose sehemu ya pili…

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

MAFUNDISHO YA NDOA.

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
1 year ago

Barikiwa sana mwalimu,Swali langu ni hili;Je,mwanamume na mwanamke waliokutana na kuanza kuishi pamoja na kuzaa watoto mbele za Mungu wanatambulika kama wanandoa?Na ikitokea wakaachana na mmojawao akaolewa au akaoa je atakuwa anaishi katika uzinzi?

Apolo peter
Apolo peter
1 year ago

Ameen nimebarikiwa