MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA- Sehemu ya 2.

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA- Sehemu ya 2.

Shalom

Hii ni sehemu ya pili ya maswali na majibu yahusuyo ndoa.. Sehemu ya Kwanza unaweza kuisoma kupitia  link hii >> MASWALI-NDOA

SWALI 01: Je Mkristo anaruhusiwa kuoa mtu wa Imani nyingine? Yaani akafunga naye ndoa tu, na kila mmoja akaendelea na imani yake.

Jibu: Ndoa ya kikristo ni ndio inayohusisha Imani moja, Bwana mmoja, Roho mmoja, tumaini moja, Ubatizo mmoja na Mungu mmoja..

Waefeso 4:3  “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4  Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

5  Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

6  Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”

Kwahiyo kabla ya Ndoa ni lazima wawili hao wafikie kuwa na imani moja, na ubatizo mmoja na Roho Mmoja na Mungu mmoja, wasipofikia huo umoja basi hiyo sio ndoa ya kikristo.

Sasa nini cha kufanya endapo ikitokea mmoja si wa imani ya  kikristo?, Jibu: Huyo ambaye tayari kashaokoka anapaswa amhubirie mwenzake habari za Wokovu kwanza, na aamini na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu (kwaufupi awe mkristo aliyesimama kweli kweli) na baada ya hapo ndipo wafunge ndoa, lakini kumbuka, si abadilike kwasababu tu anataka kuoa au kuolewa!, hapana bali anapaswa apate badiliko la kweli kiasi kwamba hata kama asipoolewa na huyo basi bado Kristo atabaki kuwa Mwokozi wake siku zote za maisha yake.

SWALI 02: Je kuna umuhimu wowote wa kupima afya kabla ya kufunga Ndoa?

Jibu: Ndio upo umuhimu wa kufanya hivyo kama kuna huo ulazima. Kuhakikisha afya zenu zipo sawa kabla ya kufanya lolote, maandiko hayajakataza kufanya hivyo. Na endapo ikitokea mmoja kakutwa na maradhi ambayo yatawafanya wawili hao wasiweze kukutana kimwili!.. Basi hapo ni uchaguzi wa Yule aliye salama, kama upendo wake ni mwingi kama ule wa Kristo, anaweza kuishi na huyo anayemchagua, lakini kamba si hawezi basi yupo huru kutafuta mwingine aliye chaguo lake hafanyi dhambi.

Lakini kama tayari wameshafunga ndoa na mmoja akapata maambukizi ya maradhi hayo basi Yule aliye salama hapaswi kumwacha huyo aliye na maradhi, wataendelea kubaki pamoja siku zote. Vile vile kama mmojawapo kapata ulemavu ambao utamfanya asiweze kabisa kukutana na mwenzake basi Yule aliye mzima pia hapaswi kumwacha mwenzake aliye na udhaifu, siku zote za maisha yake.

SWALI 03: Je wakristo wanaruhusiwa kutoa Ujauzito (Mimba)?

Jibu: Mkristo haruhusiwi kutoa ujauzito (mimba), kwasababu yoyote ile isipokuwa ya kiafya kwa maelezo ya madaktari:

Kwamfano  Ikitokea mtoto kafia tumboni hapo ni lazima ile mimba changa iondolewe ili kuokoa maisha ya mama, vile vile ikitokea itilafu katika tumbo la mama, ambayo ili mama awe salama (asipoteze maisha) na kama mama huyo hana imani ya kutosha ya kuamini kuwa anaweza kuishi bila kuitoa na akawa salama, na hivyo akakubali itolewe kufuatia maelezo hayo ya daktari, mama huyo hafanyi dhambi!, kwasababu ya usalama wake mwenyewe.

Lakini sababu nyingine yoyote ya kutoa mimba tofauti na hiyo ya kiafya, ni dhambi!..Kwamfano mwanamke kapata ujauzito bahati mbaya na alikuwa hana mpango wa kuipata hiyo, hapo hapaswi kuutoa huo ujauzito, au kapata ujauzito kwa njia ya ukahaba, hapo hapaswi kuitoa hiyo mimba, atabaki nao mpaka hatua ya kujifungua.

SWALI 04: Ni nani mtu sahihi wa kumpelekea matatizo ya ndoa? Endapo kukitokea kutokuelewana?

Jibu: Endapo kukitokea kutoelewana, ni vizuri kuomba kwa Bwana suluhisho na kurejea biblia kujua ni nini biblia inasema kuhusu hali hiyo, lakini kama bado mwanandoa anahisi anahitaji msaada zaidi basi anapaswa ayafuate makundi yafuatayo.

1: MCHUNGAJI WA KWELI WA BWANA:

Si wachungaji wote ni waaminifu, lakini pia wapo walio wa kweli na waaminifu, watu hao ni kituo bora cha kupata ushauri wa kiMungu na maombezi.

2. MZAZI:

Kama unaye mzazi aliyeokoka basi hicho pia ni kituo bora sana cha kupokea mashauri bora..na yenye msingi mkubwa.

Kamwe usitafute ushauri kwa marafiki, majirani, ndugu wa mbali, au watu usiowajua kuhusiana na mambo ya kindoa.

SWALI 05: Endapo nikagundua baada ya kufunga ndoa Mwenzangu ana matatizo katika uzazi wake (hana uwezo wa kuzaa au kuzalisha)..Je naweza kwenda kupata mtoto nje na kuendelea kuwa naye?

Jibu: Kama mwanandoa mmoja anamatatizo ya uzazi yanayomfanya asiweze kuwa na mtoto, hapo mwanandoa mwingine asiyekuwa na matatizo hayo hapaswi kumwacha Yule mwenye matatizo, wala kuondoka na kwenda kupata mtoto wa kando, atabaki naye huyo huyo siku zote za maisha yake, huku wakimwomba Bwana awafungue!.

Na kama ni mapenzi ya Bwana wao kuwa na watoto, basi Bwana atawapa mtoto haijalishi ni miaka mingapi itapita (Ibrahimu na Sara walipata watoto katika uzee), na Mungu ni Yule Yule hajabadilika.

Lakini pia kama wanaona ahadi za Mungu bado zipo mbali wanaweza ku-adopt  mtoto/watoto na kuwalea kama watoto wao.. Vipo vichanga vingi visivyo na wazazi, na mtu akiwalea hao mbele za Mungu ni zaidi hata ya Yule mwenye watoto 100 waliotoka katika uzazi wake.

SWALI 06: Je mkristo anaruhusiwa kupanga uzazi?

Jibu: Ndio wakristo wanaweza kupanga idadi ya watoto wanaotaka kuwa nao!. Biblia haijatoa amri ya kuzaa idadi ya watoto 10 au 50, ni kila mtu atakavyotaka yeye. Lakini imetoa tu angalizo kuwa tuwe watu wenye uwezo wa kuwatunza wakwetu (1Timotheo 5:8  Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.)

Kwahiyo ni lazima Mkristo awe na uwezo wa kuwatunza watoto wake, hivyo ni lazima awe na uzazi wa mpango.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA-1

MAFUNDISHO YA NDOA.

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?

Je ni viatu gani Musa aliambiwa avivue?  Vya mwilini au vya rohoni? (Kutoka 3:5).

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments