Kuomba katika roho ni kupi? na je nifanye nini ili niweze kuomba hivyo?

Kuomba katika roho ni kupi? na je nifanye nini ili niweze kuomba hivyo?

Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi;

Waefeso 6:18  kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote

Yuda 1:20  Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu

Watu wengi wanaamini kuomba katika Roho ni kuomba kwa “kunena kwa lugha tu”. Nje ya hapo sio kuomba kwa Roho. Lakini tukiwa na mtazamo huo basi tutakuwa na uelewa finyu kuhusu Roho Mtakatifu.

Ukweli ni kwamba hiyo ni namna mojawapo kati ya nyingi ambazo Roho wa Mungu anamjalia mtu kuomba.

Maana ya ‘kuomba katika Roho’ Ni kuomba ‘ndani ya Roho ya Mtakatifu/ ndani ya utaratibu/ uwepo wa Roho Mtakatifu’. Na hiyo ni zaidi ya kunena kwa lugha, Hii ikiwa na maana Mtu anaweza kuomba lakini asiwe katika uwepo huo. Na matokeo ya hivyo ni maombi kuwa makavu sana, yasiyo na nguvu.

Sasa mstari mama unaotufundisha juu ya uombaji wa Roho Mtakatifu ni huu;

Warumi 8:26  “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA”

Hapo anasema “kuugua kusikoweza kutamkwa” . Maana ya kuugua hapo ni kuweka uzito, au presha, au shauku  ya kuomba ndani ya mtu isiyokuwa ya kawaida. Tofauti na angejitahidi kwa nguvu zake yeye mwenyewe. Sasa mtu akifikia hatua hiyo, basi tayari kuanzia huo wakati anaomba katika Roho hata kama maneno yake ni ya kawaida anayoyatumia. Maombi hayo yana nguvu na yanasikika sana mbele za Mungu.

Kwamfano, ndio hapo utakuta mtu anaomba, lakini mara anasikia kububujika machozi ndani yake, mwingine anazidi kuona kiu ya kuendelea kuombea jambo lile lile kwa muda mrefu tofauti na sikuzote. Mfano wakati ule Bwana Yesu alipokuwa Gethsamane anaomba.

mwingine anajisikia wepesi usio wa kawaida, uchovu wote umeondoka ijapokuwa alikuwa amechoka sana, anaanza furahia maombi, anafurahia kuendelea kubaki palepale muda mwingi kuendelea kuomba,

Sasa hali kama hizi ukizifikia, ujue tayari umeshazama katika Roho, umeshawezeshwa na Roho, maombi yako yanakuwa na nguvu sana,

Mwingine anasikia raha Fulani moyoni, akiwa anaomba, mwingine ndio anazama katika kunena kwa lugha (kwa kusukumwa na Roho), na sio kwa akili. Mwingine anasindikizwa na kuusikia uwepo wa Mungu umemfunika, nguvu za Mungu zinashuka mwilini mwake, n.k. na unajikuta unafurahia sana maombi..

Kusudi la sisi kuomba sio kwenda kujitesa au kujiumiza, hapana bali ni mahusiano, tena ya kama mtu anazungumza na Baba yake. Kiasi kwamba ukitoka kwenye maombi unaona umetoka kweli kuwasiliana na mtu, sio umetoka kuusemesha ukuta, usiokuwa na mrejesho wowote, umeomba hewani hewani tu

Sasa ni mapenzi ya Mungu kwamba sisi watoto wake kila tuombapo tuombe katika Roho Mtakatifu. Tuzame, tuyafurahie maombi yetu. Sasa tunawezaje kufikia hatua hiyo?

Kabla ya kuona namna ya kufikia hicho kilele. Tuone kwanza vikwazo vinavyomzuia mtu asiombe kwa Roho.

VIKWAVYO VINAVYOPINGANA NA MTU KUOMBA KATIKA ROHO.

  1. Mwili
  2. Shetani

Hawa ndio maadui wawili wakubwa wa mtu kuzama. Ndio maana wewe kama mwombaji ni lazima uwafahamu, na ujue kabisa huna budi kushindana nao na ni lazima ukutane nao. Vinginevyo usipowatilia  maanani kila siku maombi yako yatakuwa ni ya “kawaida sana” na kila utakapofikiria  kitu kinachoitwa maombi utaona kama vile unapelekwa gerezani.

Ndugu Mungu hajakusudia tujihisi hivyo sisi watoto wake tunapomkaribia yeye, tuwe kama tunaliomba sanamu lisilonena, amekusudia kutupa mrejesho, na ndio hiyo zawadi ya Roho kuugua ndani yetu. Lazima atupe mrejesho wake kwamba yupo nasi.

Sasa uanzapo, hakikisha unaunyima mwili wako, raha zote, zinazokinzana na wewe kuomba. Kwamfano, ukijiona mwili unasinzia au unapoa wakati wa kuomba usipende kukakaa kwenye kiti, ni heri upige magoti, ukishindwa tembea-tembea. Tena ni vizuri ukanyoosha na mikono yako juu, huku umefunika macho. Kisha anza kuomba.

Usiogope adhabu hizo za mwanzoni hazitadumu muda mrefu sana utaingia katika Roho, ni mwili tu unakuambia wacha, kunitesa, wewe ulazimishe tu, ukikuambia leo siku nzima umefanya kazi legea-legea, pinga hayo mawazo. Hivyo ukiwa Sasa katika hali hiyo. Anza kuomba lakini pia tumia ahadi za Mungu zilizopo kwenye biblia ni muhimu sana, kulingana na jambo unaloliombea, mkumbushe Bwana, ulisema hivi, na hivi kwenye Neno lako,, Ulisema ni nani aliye Baba, mtoto wake akimwomba mkate atampa jiwe, mkumbushe mwambie ulisema, kama ungetazama dhambi zetu ni nani angesimama,..mwambie ulisema niite nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa na magumu usiyoyajua n.k..Tumia njia hiyo, kujimimina kwa Bwana

Omba huku umetilia umakini(concentrate), mawazo yako ukiyalazimisha yasiende nje ya Mungu. Tengeneza picha halisi Mungu amesimama mbele yako kukusikia, fumba macho. Usiruhusu kufikia mambo ya nje, kwasababu akili yako itakuwa shapu kukutoa, ukitoka rudi, endelea kuomba. Ndio ni kipindi kifupi utataabika , lakini hatimaye utazama tu.. Sasa ukiendelea kudumu kwa kung’ang’ania huko  kwenye maombi hayo kwa kipindi fulani. Hayo mazingira rafiki ya Roho Mtakatifu kuyaingilia maombi yako. Utashangaa tu, wepesi usio wa kawaida umezuka ndani yako. Tangu huo wakati endelea kuomba kwa jinsi usikiavyo rohoni, kwani hayo maneno unayoyaomba mengine hutaelewa unayatolea wapi, huyo ni Roho Mtakatifu anaomba na wewe.

Ndio maana akasema msifikiri-fikiri, kwasababu Roho mwenyewe atawajalia.  Wengine kabla ya kuomba wanasema sijui nitaomba nini? Ndio hujui kwasababu bado hujazama, ukishazama utaweza tu kuomba kwasababu ni yeye ndio anayekujalia. Wengine wanasukumwa kunena kwa lugha n.k.

Adui wa pili ni shetani. Huyu anapaswa apingwe kwa kukemewa. Kabla ya kuanza maombi, hakikisha unayateka mazingira yako ya kimaombi. Ukimwomba Mungu, afukuze uwepo wote wa mapepo, hapo ulipo.  Dalili ya shetani, ni pale unashangaa ukiwa unataka kuomba kichwa kinauma au tumbo, au hali Fulani isiyo ya kawaida inakuvaa katika mwili wako. Huyo ni shetani, mpinge kwa kukemea kisha endelea na maombi. Au mwingine anaona mazingira ya kusumbuliwa, mara kelele Fulani za nje, au simu zinaingia, ambazo si kawaida sikuzote kuwepo. Ndio maana ni vizuri katika kuomba kwako uzime simu. Ukae mbali na mazingira yenye mwingiliano, hiyo itakufanya umpe adui wakati mgumu kukusumbua.

Zingatia tu: Shetani haogopi sana maombi ilimradi maombi, anaogopa sana maombi yaliyo katika Roho, Hata kama ni ya muda mfupi, hayapendi, na ndio atakayoyapiga vita sana. Hivyo usiwe mwepesi mwepesi kupenda kuomba juu juu.

Kwahiyo ukizingatia mambo hayo mawili kutakufanya uzame rohoni katika maombi yako yote. Na utayafurahia na utaona matokeo pia.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika sanduku la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

HIZI NI NYAKATI ZA KUFUNGA NA KUOMBA.

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

SALA YA BWANA. (Namna ya kuiomba)

JE! TUNAPASWA TUOMBE MARA NGAPI KWA SIKU?

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments