Mahali pekee ambapo maandiko yanaeleza kuchoka kwa Yesu, ni siku ile alipokuwa anatoka Uyahudi anakwenda Galilaya. Kwasababu safari yake ilikuwa ndefu, ya saa nyingi, ilibidi waweke kituo kwanza kwenye mji wa mmoja wa wasamaria, wapumzike. Yeye na wanafunzi wake kwenye kile kisima cha Yakobo.
Yohana 4: 5 Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. 6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu AMECHOKA KWA SAFARI YAKE, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.
Jua la mchana likiwa kali, anasikia mwili ni mchovu hautaki, kufanya kazi yoyote, njaa zinauma, mpaka mitume wakaondoka kwenda kutafuta chakula mjini. Lakini katika mazingira hayo hayo Analetewa na Mungu mtu mwenye dhambi amshuhudie habari za neema ya wokovu. Ndio Yule mwanamke msamaria.
Lakini Yesu hakuwa na udhuru kwa kusema, huu ni muda wangu wa kupumzika, ni muda wangu wa kulala, ni muda wangu wa lunch nile na wanafunzi wangu. Alitii vilevile katika uchovu wake, akaanza kuongea na Yule mwanamke habari za ukombozi, kwa kipindi kirefu kidogo.
Lakini mwisho wa mazungumzo yao haukuwa bure, Yule mwanamke aliondoka, lakini baada ya muda mfupi alirudi na jopo la watu, ili kuja kumsikiliza Bwana Yesu, maneno aliyoshuhudiwa na yeye (Yohana 4:1-42). Na baada ya hapo tena, Samaria yote ikamwamini, sehemu nyingine mpaka wakawa wanataka hata kumfanya mfalme.
Lakini ni nini tunapaswa tujifunze katika habari hiyo? Wengi wetu hatujui kufanikiwa kwa huduma ile ya Yesu pale ndani ya mwanamke Yule zaidi ya wengine wengi, kulitokana na gharama ambazo Yesu aliingia. Yaani katika kipindi cha KUCHOKA kwake, alikuwa tayari kulitimiza kusudi la Mungu. Kitendo hicho rohoni huwa kinageuka na kuwa IMANI, kubwa sana mbele za Mungu.
Je! Na sisi, tunaweza kujifunza jambo hili kwa Bwana. Je! visingizio cha kuchoka, tumeshindwa kutimiza makusudi mangapi ya Mungu, yenye matokeo makubwa kama haya? Nimetoka kazini, nimefanya kazi wiki nzima, hivyo nimechoka siwezi kwenda kuomba. Weekend ni siku yangu ya kupumzika, siwezi kwenda kwenye ushuhudiaji?
Hatujui kuwa hapo ndipo Mungu anapathamini, tunataka siku ambayo tupo “free” tu.
Ukweli ni kwamba tukiwa watu wa kungojea siku ambazo tuna nafasi ya kutosha, au tuna afya, au tuna fursa, au tume-relax si rahisi kuzalisha vema kama wakati ambao tutajiona sisi ni dhaifu. Katika dunia hii ya masumbufu na mahangaiko ya maisha, utajikuta mpaka unamaliza maisha yako hujapata hata huo muda wa kupumzika vema. Hivyo tumia fursa hiyo sasa.
Isaya 40:29 Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. 30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; 31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.
Hubiri injili nyakati zote, omba nyakati zote, soma Neno nyakati zote. Kumbuka wakati wa kuchoka, ipo nguvu ya Mungu kukusaidia. Jenga ufalme wa Mungu. Na Bwana atakutia nguvu.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
WALIKUWA WAMECHOKA NA KUTAWANYIKA KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI.
NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?.
Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?
YESU HAYUPO KATIKA MAZINGIRA YALEYALE TU SIKUZOTE, USIJISAHAU.
About the author