Wengi, tumeshasikia kuwa Yesu atarudi, lakini mpaka mtu anasema atarudi, maana yake ni kuwa alishawahi kuja hapo nyuma. Na kama tunavyojua Bwana wetu Yesu Kristo alikuja mara moja tu, miaka karibu elfu mbili iliyopita, akaishi, akafa,akazikwa, akafufuka, akapaa mbinguni. Lakini wakati wote alipokuwa hapa duniani aliwaahidi wanafunzi wake kuwa atarudi tena.
Hivyo somo hili, ni muhimu kufahamu, namna ambazo Yesu alisema atarudi, ili usikose maarifa, kwasababu wengi hapa wanakosa shabaha katika kutambua kauli za Yesu. Naomba Soma kwa utulivu somo hili mpaka mwisho.
Sasa kuhusu kurudi kwake duniani, alizungumza katika nyakati tofuati tofauti kurudi kwa namna mbili.
Tuangalie kwa undani, namna hizi mbili. Husasani tutailenga hiyo ya pili.
Je! ni kwa namna gani, alirudi kama Roho,Aliwaambia hivi mitume wake;
Yohana 14:18 “Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. 19 Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.
20 Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu”.
Soma pia, katika Yohana 16:16, amerudia maneno hayo hayo,
Unaona? Mitume walidhani hawatamwona tena, lakini siku ile aliyopaa mbinguni,siku kumi baadaye, biblia inasema walikuwa wamekusanyika wote mahali pamoja, akawajilia Roho Mtakatifu akawakalia wote, wakajazwa Roho Mtakatifu. Na kama tunavyojua tangu huo wakati na kuendelea, kila mmoja alijua anaye Yesu moyoni mwake, hakuna mtu aliyeuliza Yesu yupo wapi.
Uyatima uliondoka kabisa, kabisa, ndipo wakatambua maana ya yale maneno. Hivyo tumeshaona kurudi kwake kwa kwanza duniani, kulikuja kwa namna hiyo ya Roho Mtakatifu, na mpaka sasa Kristo yupo ndani ya mioyo ya waliomwamini, na kupokea Roho Mtakatifu.
Lakini pia katika maneno yake mengine, alisema atarudi kama mwizi.
Soma,
Mathayo 24:43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
Unaona tena?, Hajasema, atarudi kama askari, au mfanya biashara, bali kama mwizi. Sasa ni vema tujue sifa za mwizi, ni zipi kibiblia, ndipo tuelewe jinsi kurudi kwake kwa namna hiyo kutakavyokuwa.
Ukisoma Yohana 10:10 Yesu anasema hivi; “Mwivi haji ila AIBE na KUCHINJA na KUHARIBU; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele”.
Kumbe mwizi hasaa, anayezungumziwa ni mfano wa jambazi, na sio wale wadokozi, ni wale wanaobeba silaha, ili kuharibu na kuua wanaowaona, wachukue mali yao waondoke.
Na Yesu ndivyo atakavyokuja katika siku za mwisho hizi, atatimiza sifa hizo zote tatu.
1.) Jambo la kwanza Atakuja saa tusiyodhani, Kisha ATAIBA kitu chake cha thamani duniani. Ni hicho si kingine zaidi ya watakatifu wake. Hapo ndio suala la unyakuo linapoibukia.
Mathayo 24:40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; 41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
2) Lakini pamoja na hilo, kuja kwake kutaambatana na KUCHINJA.
Maana yake ni kwamba, kama unyakuo utakupita, dunia itakuwa inajiandaa kuingia katika siku ile ya mapigo ya ghadhabu ya Mungu, ambayo mwisho wake utaishia na Kristo kuonekana katika umbile la kibinadamu kabisa, kuwaua mataifa yote ambayo yatakusanyika kupigana naye katika ile vita kuu ya Harmagedoni.
Ufunuo 19:11 Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.
13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.
15 NA UPANGA MKALI hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANAWA MABWANA.
Huu ni wakati ambao Yesu, atauangamiza ulimwengu, mfano wa mwizi, asiyekuwa na huruma. Usitamani uwepo wakati huo ndugu, ni majuto vilio na kusaga meno.
3) Lakini mwisho kabisa, ATAHARIBU.
Tunafahamu kuwa mwizi, huvunja, mahali ili aingie, huvuruga kila kitu anachokiona, vivyo hivyo na hii dunia itafumuliwa yote, mifumo yote itaangushwa, itafinyangwa upya, yote hayo yatatokea katika siku hiyo hiyo ya Bwana, ambayo itaharibu kila kitu.
2Petro 3:10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. 11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, 12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka?
Soma pia,(Ufunuo 16:17-21), kuongeza maarifa..
Hivyo ndugu, wakati huu wa Yesu kurudi kama mwizi umekaribia sana, ambao utaanza Kwanza kwa tukio la unyakuo. Bwana anatutaka sisi tukeshe(rohoni), asitukute tumelala. Ili Siku hiyo isitujilie ghafla, tukabaki hapa duniani.
1Wathesalonike 5:1 Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.
5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.
6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. 8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.
Bwana atupe macho ya kuona haya.
Je! Umempokea Yesu maishani mwako, Je! Ameziondoa dhambi zako? Kama jibu ni la, unasubiri nini? Hujui kesho kama utakuwepo, hujui kama leo atarudi. Hivyo tubu sasa, mwamini Yeye upate ondoleo la dhambi zako, kisha utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Ikiwa utapenda kupokea wokovu basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii bure. Bwana akubariki.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.
About the author