Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe daima. Karibu katika mafundisho ya biblia, Neno la Mungu wetu lililo Taa na Mwanga wa Njia zetu (Zab.119:105).
Zipo njia Mbili tu zilizowekwa mbele ya kila mwanadamu, Nazo ni njia ya UZIMA, na njia ya MAUTI.
Yeremia 21:8 “Nawe waambie watu hawa, Bwana asema hivi, Tazama naweka mbele yenu NJIA YA UZIMA, na NJIA YA MAUTI”.
Njia ya Uzima, inamwongoza mtu “Uzimani”..na Njia ya Mauti inamwongoza mtu “Mautini (ziwa la moto)”.
Njia ya Uzima imenyooka haina migawanyiko mingi (sawasawa na Yohana 14:6), ambapo Bwana YESU alisema yeye ndio hiyo “Njia”, na mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye.
Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”
(Maana yake hakuna njia mkato wala njia mbadala ya kumfikia Baba)…Ni moja tu! Tena iliyonyooka, nayo ni YESU KRISTO, na si kupitia mtu mwingine yoyote mashuhuri, au mtakatifu mwingine yoyote aliye hai au aliyekufa au nabii yoyote katika biblia.
Lakini ile ya Mauti inamigawanyiko mingi, inaanza kama njia moja lakini mwisho wake inamigawanyiko,
Mithali 14:12 “IKO NJIA ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni NJIA ZA MAUTI”
Hapo anamaliza na kusema mwisho wake ni “NJIA ZA MAUTI” na si “NJIA YA MAUTI” kana kwamba ni moja, bali nyingi. Na njia ya Mauti si mwingine Zaidi ya “shetani”…Kama jinsi njia ya UZIMA ilivyo Bwana YESU kadhalika njia ya Mauti ni “shetani”.
Na shetani anaabudiwa kupitia vitu vingi, anaweza kuabudiwa kupitia miti, mawe, udongo, au kupitia vitu vitu vingine kama fedha, watu, dini n.k..ndio maana hapo biblia inasema hiyo Njia (shetani) mwisho wake ni “Njia za Mauti” (maana yake zipo nyingi).
Na hiyo ndio sababu pia kwanini biblia inataja uwepo wa milango mingi ya kuzimu (Soma Mathayo 16:18). Milango ya kuzimu ndio hizo njia zote zinazoweza kumpeleka mtu kuzimu.
Nabii Isaya amezidi kuziweza vizuri njia hizi kwa ufunuo wa Roho… Amezitofautisha kama “NJIA” pamoja na “NJIA KUU”..
Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na NJIA KUU, na NJIA….”
“Njia Kuu” ni “Njia ya Uzima”…. Na “Njia” pekee yake “Ni njia ya Mauti”..
Lakini anaendelea kusema… hiyo “Njia kuu” itaitwa Njia ya utakatifu, na ya watu wasafirio..
Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio….”
Maana yake wote wanaiendea hiyo njia ya Uzima (YESU) Ni lazima “utakatifu” uwe muhuri wao sawasawa na kitabu kile cha Waebrani 12:14.
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”.
Vile vile ni lazima wawe “wasafiri”.. Tabia ya msafiri huwa anadumu katika chombo cha usafiri awapo safarini, na hawezi kujishikisha na mambo akutanayo njiani au barabarani…. na chombo chetu cha usafiri ni NEEMA YA MUNGU. Tuwapo katika safari hii ya kwenda mbinguni kupitia njia ya Bwana YESU, mambo ya ulimwengu hayapaswi yashikamane na sisi.
1Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho”.
Na mwisho anasema.. “wajapokuwa wajinga hawatapotea katika njia hiyo”
Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO”.
Ikiwa utaonekana mjinga kwa kuwa umeamua kuifuata NJIA KUU ya UTAKATIFU na umeamua kuishi kama MSAFIRI duniani, basi biblia inasema “hautapotea/hatutapotea” katika njia hiyo..
Haijalishi dunia nzima itakuona kama umepotea, umerukwa na akili, umechanganyikiwa…Mungu yeye anakuona upo katika njia sahihi na una hekima nyingi.. kwasababu mwisho wa njia hiyo ni UZIMA WA MILELE, Na Utakutana na Bwana naye atakufuta machozi.
Ufunuo 7:15 “Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao
16 Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote.
17 Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”
Je wewe leo umechagua njia ipi??… Njia kuu ya Uzima? Au Njia ya Mauti..
Kumbukumbu 30:14 “Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
15 ANGALIA, NIMEKUWEKEA LEO MBELE YAKO UZIMA NA MEMA, NA MAUTI NA MABAYA”.
CHAGUA NJIA YA UZIMA, na TEMBEA KATIKA NJIA KUU YA UTAKATIFU.
BWANA AKUBARIKI.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.
TABIA ZA NJIA YA MUNGU KWA MKRISTO
HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?
KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI
About the author