Agano la Chumvi ni nini? (2Nyakati 13:5)

Agano la Chumvi ni nini? (2Nyakati 13:5)

Swali: Agano la chumvi kama tunavyolisoma katika 2Nyakati 13:5 ni agano la namna gani?


Jibu: Turejee..

2Nyakati 13:5 “Je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa AGANO LA CHUMVI”

Neno hili “Agano la Chumvi” limeonekana mara tatu (3) katika biblia.. sehemu ya kwanza ni hii tunayoisoma ya 2Nyakati 13:5, na nyingine ni katika Hesabu 18:19, pamoja na Walawi 2:13.

Sasa swali nini maana ya Agano la Chumvi?

Nyakati za zamani na hata sasa katika baadhi ya maeneo na baadhi ya jamii, mbali na matumizi ya chumvi katika kuongeza ladha ya chakula, lakini pia chumvi ilitumika na inatumika kama kiungo cha kuhifadhia chakula ili kiweze kudumu kwa muda mrefu bila kuharibika.

Zamani hakukuwa na friji kama zilizopo leo, hivyo kitu pekee kilichokuwa kinatumika kuhifadhia vyakula ambavyo bado havijapikwa (kibichi/kikavu) kilikuwa ni CHUMVI.

Kwahiyo Chumvi, tunaweza kusema inalo AGANO BORA la kuhifadhi kitu kwa muda mrefu pasipo kuharibika kuliko kitu kingine chochote (Ni kiungo cha uhakika kinachodumisha kitu kwa muda mrefu).

Ndio maana utaona sadaka zote katika agano la kale, ziwe za Unga, au za wanyama ziliwekwa chumvi, kuwakilisha uthabiti wa agano la Mungu.

Walawi 2:13 “Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga UTALITIA CHUMVI; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote”.

Ezekieli 43:22 “Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng’ombe huyo.

23 Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng’ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume wa kundini mkamilifu.

24 Nawe utawaleta karibu mbele za Bwana, na MAKUHANI WATAMWAGA CHUMVI JUU YAO, nao watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa Bwana”.

Hivyo kitu kilichotiwa Chumvi maana yake kinadumu muda mrefu, na kilichodumu muda mrefu maana yake kimetiwa chumvi nyingi… ndio maana upo usemi unaowatambulisha wakongwe kama “WATU WALIOKULA CHUMVI NYINGI”.. Na usemi huu pia upo katika biblia, kuwakilisha kuwa Wakongwe ni watu wenye chumvi mwilini.

Ezra 4:11 “Hii ndiyo nakili ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta;watumishi wako,watu walio ng`ambo ya mto wakadhalika.

12 Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake.

13 Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara.

14 Na sisi, KWA KUWA TUNAKULA CHUMVI YA NYUMBA YA MFALME, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme”.

Hivyo tukirudi katika mstari huo wa 2Nyakati 13:5 unaosema “Je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa AGANO LA CHUMVI”..

Maana yake ni kwamba Agano Mungu aliloingia na Daudi la kumpatia Ufalme, basi ni Agano thabiti lenye kudumu muda mrefu (milele) lisilo haribika kama tu vile chumvi itiwavyo katika vyakula na kukidumisha chakula hicho.

Na sisi tunapomwamini Bwana YESU na kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha, basi TUNATIWA CHUMVI katika roho (ambayo inatufanya tudumu milele katika ahadi za Mungu, na kuwa na uzima wa milele).

Na tunatiwaje Chumvi ili tuweze kupata uzima wa milele?

JIBU, “TUNATIWA CHUMVI KWA MOTO”.

Marko 9:49 “Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto”.

Moto unaozungumziwa hapo ni moto wa Roho Mtakatifu (soma Mathayo 3:11 na Matendo 2:3) ambao ukishuka ndani ya mtu unachoma kila kitu cha kidunia, na kusafisha kama vile chuma kisafishwavyo katika moto, (moto huo unamtenga mtu na vile vitu vilivyoshikamana na maisha yake) Ambapo wakati mwingine unaweza kuleta maumivu, kwasababu unaondoa vile viungo vyote vinavyomkosesha mtu.

Ambapo baada ya hapo mtu anakuwa mpya kabisa (kiumbe kipya) na anakuwa ana uzima wa milele ndani yake, kwasababu katika chumvi.. Hilo ndilo Agano la Chumvi kwetu.

Je umetiwa Chumvi?..Kama utamkubali Bwana YESU siku ya leo, basi utatiwa chumvi na Roho Mtakatifu, na utakuwa chumvi ya dunia (Mathayo 5:13) na utakuwa na uhakika wa maisha ya Milele. Hivyo mkaribishe leo maishani mwako kama bado hujafanya hivyo.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Ninyi ni chumvi ya dunia; Andiko hilo lina maana gani?

Bwana alimaanisha nini kusema “kila mtu atatiwa chumvi kwa moto;

TUSIPOUTHAMINI WOKOVU TUTAPATAJE KUPONA?

Siri za Mungu ni zipi? (1Wakorintho 4:1)

JINSI NEEMA YA MUNGU ILIVYOKUWA KUBWA KWA MKE WA LUTU.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments