Siri za Mungu ni zipi? (1Wakorintho 4:1)

Siri za Mungu ni zipi? (1Wakorintho 4:1)

Swali: Biblia inataja siri za Mungu katika 1Wakorintho 4:1, je hizi siri ni zipi na zipo ngapi?

Jibu: Turejee,

1Wakorintho 4:1 “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu”

Awali ya yote tujue maana ya uwakili unaozungumziwa hapo?…. Uwakili unaozungumziwa hapo sio mfano wa ule wa “mahakamani” La! bali unamaanisha “Usimamizi”… Kibiblia mtu aliyepewa usimamizi wa nyumba au kazi Fulani, aliitwa “Wakili”..soma Luka 12:43-48 na Luka 16:1-13

Hivyo hapo Mtume Paulo, aliposema “.. sisi ni mawakili wa siri za Mungu” maana yake “wameweka kuisimamia nyumba ya Mungu kwa kuzifundisha siri za Mungu”….Kwa urefu Zaidi kuhusu Uwakili katika biblia fungua hapa >>> Wakili ni nani kibiblia? Uwakili ni nini?

Sasa tukirudi katika swali letu, SIRI ZA MUNGU NI ZIPI na ZIPO NGAPI?

Jibu ni kwamba “SIRI ZA MUNGU” zimetajwa MBILI TU (2), katika biblia. Ambazo ni 1)YESU NI MUNGU.   2) MATAIFA NI WARITHI WA AHADI ZA MUNGU… Tutazame moja baada ya nyingine.

  1.YESU NI MUNGU.

Wakolosai 2:2 “ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, WAPATE KUJUA KABISA SIRI YA MUNGU, YAANI, KRISTO;

3  ambaye ndani yake yeye HAZINA ZOTE ZA HEKIMA NA MAARIFA ZIMESITIRIKA”.

Kwanini au kivipi “KRISTO” ni “SIRI YA MUNGU”?.. Kwasababu ndani yake hazina zote na hekima na maarifa zimesitirika..maana yake yeye ndio kila kitu, NDIYE MUNGU MWENYEWE katika mwili wa kibinadamu!!!!..Kiasi kwamba laiti Pilato angelijua hilo, asingeruhusu hukumu ipite juu yake, laiti wale makuhani na maaskari wangelijua hilo wasingepitisha misubari katika mikono yake na miguu yake, lakini walifumbwa macho ili tupate wokovu.

1Wakorintho 2:7 “bali twanena hekima ya Mungu KATIKA SIRI, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;

8  AMBAYO WENYE KUITAWALA DUNIA HII HAWAIJUI HATA MMOJA; MAANA KAMA WANGALIIJUA, WASINGALIMSULIBISHA BWANA WA UTUKUFU”.

Siri hii ya kwamba KRISTO NI MUNGU, inaanzia katika Isaya 9:6, na kisha Yohana 1:1, Yohana 14:9, Yohana 20:28, Tito 2:13, 1Timotheo 3:16 na Ufunuo 22:13-13.

Siri ya Bwana YESU Kuwa MUNGU, inajulikana pia kama “Siri ya Utauwa/Uungu” ambayo Mtume Paulo aliitaja katika 1Timotheo 3:16..

1Timotheo 3:16 “Na bila shaka SIRI YA UTAUWA NI KUU. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu”.

Kwahiyo BWANA YESU KRISTO ni MUNGU ALIYEDHIHIRISHWA KATIKA MWILI, na wote tunaomwamini tunapaswa tuwe mawakili wa SIRI HIYO, Maana yake “KUIAMINI na KUIHUBIRI KWA WENGINE, wasiofahamu” .

  2. MATAIFA NI WARITHI WA AHADI ZA MUNGU.

Hii ni Siri ya pili (2) ambayo ilifichwa kwa vizazi vingi, lakini ikaja kufunuliwa baada ya KRISTO kupaa juu mbinguni.. Tangu wakati wa Musa mpaka wakati wa Yohana, manabii wote na wayahudi wote walikuwa wanajua na kuamini kuwa “hakuna namna yoyote, wala njia yoyote” itakayofanyika kwa watu wa mataifa wakubaliwe na MUNGU.

Wote walijua Taifa Teule la Mungu ni ISRAELI peke yake, na mataifa mengine yote ni watu najisi, lakini baada ya Bwana YESU kuondoka alianza kumfunulia Petro siri hiyo kuwa hata mataifa ni warithi sawa tu na wayahudi, kupitia msalaba wake (Bwana YESU).. Na alimfunulia siri hiyo wakati ule alipokwenda nyumbani kwa Kornelio aliyekuwa mtu wa mataifa (Matendo 10)..

Na baadaye Bwana YESU akaja kumfunulia Mtume Paulo siri hiyohiyo kuwa Mataifa nao ni warithi, tena wa ahadi moja na wayahudi, hivyo wanastahili injili, na kuhubiriwa habari njema..

Waefeso 3:5 “Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

6  YA KWAMBA MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, NA WA MWILI MMOJA, NA WASHIRIKI PAMOJA NASI WA AHADI YAKE ILIYO KATIKA KRISTO YESU KWA NJIA YA INJILI;

7  Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake”.

Na sisi lazima tuwe wahudumu (Mawakili) wa siri hii kwamba “Wokovu ni haki ya watu wote” na Mungu anawapokea watu wote, ikiwa tu watakubali kutii na kunyenyekea mbele zake.

Kwahiyo kwa hitimisho, ni kwamba “Siri za Mungu” Si zile siri za kanisa, au zile za watumishi, au wapendwa kanisani…La! Bali ni hizo zilizotajwa hapo katika maandiko…Na kumbuka, shetani naye ana siri yake ijulikanayo kama “Siri ya Kuasi” iliyotajwa katika biblia ambayo inafanya kazi kwa kasi sana nyakati hizi…

Je umempokea YESU?..Kumbuka kipindi tulichopo ni cha Neema, lakini hii neema haitadumu milele, itafika wakati itaisha.. baada ya unyakuo hakuna neema tena, vile vile baada ya kifo hakuna Neema tena. Ni heri ukayasalimisha maisha yako kwa Bwana YESU maadamu unaishi, baada ya kifo hakuna nafasi ya pili.

Warumi 10:8 “Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.

9  Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

10  Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

11  Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika

12  Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;

13  KWA KUWA, KILA ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAOKOKA”

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

Hazina za gizani ni zipi? (Isaya 45:3).

SIRI YA KUASI KATIKA KANISA LA MUNGU.

UFUNUO: Mlango wa 10.

KUWA MAKINI, HATUA ZA UNYAKUO ZINAENDELEA.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments