Je! ndoa ni lazima ifungwe kanisani? kama ndio, imeandikwa wapi?

Je! ndoa ni lazima ifungwe kanisani? kama ndio, imeandikwa wapi?

SWALI: Je! tunalisoma wapi kwenye maandiko panasema ndoa inapaswa ifungwe kanisani. Utaratibu huo upoje?


JIBU: Ili kujibu swali hili tuanzie mbali kidogo.

kufahamu ndoa ni nini? aina za ndoa, kisha mahali sahihi pa kufungia ndoa ni wapi?.

Ndoa ni nini?

Ndoa ni muunganiko kati ya watu wawili(mwanaume na mwanamke ) unaotambulika na kuheshika kijamii, au kisheria.

Pale mwanaume anapomwona mwanamke na kupatana naye waishi pamoja kama mume na mke, kwa kufuata taratibu husika za kijamii, labda kukutanishwa kwanza wazazi, au walezi, wazee wa ukoo, kupokea mahari, kisha kuidhinisha jambo hilo, au serikali kuidhinisha, hiyo tayari inaitwa ndoa.

Aina mbili za ndoa.

  1. Ndoa za wapagani
  2. Ndoa za kikristo.

Ndoa za wapagani. Hizi ni ndoa lakini hazijadhibitiwa na kanuni timilifu za Mungu. Mfano wa hizi, ndio hizo kama za kijamii, na kiserikali, au za dini nyingine zote mfano wa ki-hindu, kiislamu, ki-budha n.k. zote hizi ni ndoa za wapagani.

Zingatia: (Hapa hatumaanishi zile za mashetani, kama za jinsia moja, au za wanadamu na wanyama hapana kwasababu hizo sio ndoa, bali tunazungumzia hizi za kawaida kabisa za asili).

Kiuhalisia mtu anaweza akawa katika mojawapo ya ndoa hizi, na asihesabike kuwa ni mkosaji kwasababu ndoa hasa ni jambo la kiutamaduni, ambalo huusisha wanadamu wote, bila kuchagua dini, rangi, au kabila.

Hivyo si sawa kudhani kuwa kwasababu watu fulani hawajafungishwa ndoa kikristo(kanisani) basi, zote hizo sio ndoa kwamba ni sawa tu hata kwenda kuoa tena hapo, au kuivuruga, wasiishi pamoja. Ukifanya hivyo Mungu atakuwajibisha kwa kuzivuruga ndoa za watu wengine. 

Aina ya pili ya ndoa ni ndoa ya kikristo.

Hii ni ndoa inayofungwa katika kanuni timilifu za Mungu alizozikusudia tangu mwanzo.

Kanuni zenyewe ni hizi

    i) Wote wawe waamini.

(1Wakorintho 7:39, 1Wakorintho 9:5, 2Wakorintho 6:14 – 16)

Kuamini si lazima muwe katika viwango sawa kiroho, lakini wote muwe upande mmoja wa Kristo, (Kwasababu hayo mengine yanaweza rekebika). Lakini mmoja ni mganga wa kienyeji, mwingine mkristo,.au mmoja ni muislamu mwingine mkristo. Hilo si sawa ni sharti wote wawe wakristo. Kwasababu hakuna ushirika wowote kati ya nuru na giza.

Kwasababu Ndoa ya kikristo ni lazima iwe katika jina la Bwana, vinginevyo, itaangukia katika lile kundi lingine.

      ii) Mume mmoja, mke mmoja.

Tofauti na ndoa za wapagani. Ambazo kwao unaweza kuwa na mke zaidi ya mmoja, lakini mtu anayetaka ndoa yake itimilike mbele za Kristo, basi mume/mke atambue kuwa hana ruhusa ya kuongoza mwenza mwingine. 

Mathayo 19:4-5

[4]Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, 

[5]akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? a

      iii) Malazi yawe safi:

Waebrania 13:4

[4]Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. 

Malazi kuwa safi maana yake ni nidhamu ya kiasi, katika kukutana kimwili. Mkristo hapaswi kuwa mtu wa hulka ambaye wakati wote anawaza zinaa, mpaka anakosa muda wa kujishughulisha na mambo ya rohoni.

1 Wakorintho 7:5

[5]Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu. 

Vilevile viitendo kama kuingiliana kinyume na maumbile haviruhusiwi ndani ya ndoa (1Wakorintho 6:9).

      iv) Hakuna talaka. 

Tofauti na ndoa za wapagani, mtu anaweza kuacha/kuachwa kwa sababu yoyote, labda mfano wamechokana, au wameudhiana, lakini katika ukristo hilo jambo halipo mtaendelea kuishi pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisha. 

Bwana alitoa ruhusa hiyo katika eneo la uasherati tu lakini ukumbuke, alisema pia ‘samehe mara saba sabini’. Hivyo kwa kauli hiyo hakuna popote tunaona wigo wa wanandoa kuachana kwa sababu yoyote ile.(1Wakorintho 7:39-40)

      V) Mume ni sharti ampende mkewe. 

Mume kumpenda mkewe ni amri ya kindoa, anawajibu wa kumtunza na kumuhudumia na kujitoa kwa ajili yake, kama Kristo alivyolipenda kanisa.(Waefeso 5:25-31)

     Vi) Mke ni sharti amtii mumewe.

Ni amri mke amtii mumewe kwa agizo atakaloambiwa/ elekezwa. Tofauti na ndoa za wapagani ambazo hili linaweza lisiwe la muhimu. Kwenye ukristo, ni lazima utii wa mwanamke uonekane kwa mumewe.

Waefeso 5:22

[22]Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. 

Sasa vigezo hivi wakivikidhi hawa wakristo ambao wameokoka na wanatarajia kuishi kama mke na mume. Basi hiyo huitwa  ndoa ya Kikristo iliyokidhi vigezo vitimilifu vya Mungu,.haijalishi imefungwa kanisani au kwenye familia, .

Swali ni je? kwanini watu wafungie kanisani? Na  Je ni takwa? 

Mkristo ambaye anathamini ukamilifu wote wa ki-Mungu, katika maeneo yake yote ya kiroho na kimwili, kufungia ndoa yake kanisani itakuwa ndio chaguo lake bora. Kwanini iwe hivyo?

Hizi ndio faida za ndoa kufungiwa kanisani

  1.  Kanisa ni mahakama ya wakristo

Biblia inatueleza mashtaka yetu, hayapaswi kutatuliwa na watu wa ulimwengu, bali ndani ya kanisa. Kwasababu kanisa ni zaidi ya mahakama yoyote, ambayo Mungu ameiheshimu mpaka akaamua malaika zake wahukumiwe katika hiyo.

Hivyo endapo kuna migogoro, au kutoelewana, au kupatiwa misaada, au mashauri, au maonyo, au maongozi,  basi kanisa, limewekwa na Mungu kwa ajili yako kukusaidia katika hayo yote. 

Lakini ikiwa hukuifungia ndoa yako kanisani. Fahamu kuna mambo kama hayo yatakupita, au yatakuwa magumu kwetu kutatulika.

1 Wakorintho 6:1-3

[1]Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? 

[2]Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? 

[3]Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? 

    2) Ushuhuda mwema.

Mungu anapenda mambo mema atufanyiayo tumtukuze mbele ya kusanyiko la watakatifu. Tunajua Ndoa ni kitu chema, hivyo tunapoweka wazi mbele za Bwana,  na mbele ya kanisa lake, yeye hutukuzwa lakini pia tunapokea baraka za kanisa, Ikiwa tunapoumwa na kuponywa hatuoni sawa kukaa na shuhuda zetu ndani, tunakwenda kushuhudia mbele ya kanisa, si zaidi ndoa zetu?, ni ushuhuda mkubwa, ambao utawafariji wengine, lakini pia utaihubiri injili ya Kristo.

Zaburi 35:18

[18]Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; 

Nitakusifu kati ya watu wengi. 

Hivyo, kwa maelezo hayo tunaweza kusema hakuna sababu ya Mkristo yoyote kuifungia ndoa yake, mbali na kanisa. 

Lakini hiyo haimaanishi kuwa usipofungia kanisani, ndoa yake haitambuliwi na Mungu. Maadamu umekidhi vigezo “mama”, tulivyoviorodhesha juu. Hiyo ni ndoa.

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAFUNDISHO YA NDOA.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments