Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza 

Kitabu hichi ni moja ya nyaraka   zilizondikwa na  mtume Paulo katika agano jipya, 

Waraka huu amegusia mambo mengi, hasahasa katika eneo la marekebisho na maonyo. Unagusia nidhani na taratibu za kikristo zinazopaswa zifuatwe ndani ya  kanisa, unazungumzia pia eneo la uhalisia wa ufufuo wa wafu katika siku ya mwisho pamoja eneo la upendo.

Na huu ndio uchambuzi wake katika maeneo mama; 

1) Matabaka ndani ya kanisa. (1:10-17, 3:1-4:21)

Paulo anatoa onyo juu ya migawanyo ambayo ilianza kutokea ndani ya kanisa iliyozaa  wivu na fitina, ambayo ilisababishwa kwa baadhi ya watu kujiwekea matabaka kwa kujivunia viongozi kwa kusema mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo, mimi ni wa Kefa. Akiwatahadharisha na kuwasihi  kwa kuwaeleza kwamba wao ni wahudumu tu katika nafasi mbalimbali, bali mkuzaji ni Kristo. Na hivyo hawapaswi kujivunia wao, bali Kristo

2) Usahihi juu ya hekima ya Mungu

Kristo ni hekima ya Mungu na nguvu ya Mungu.(1:18- 2:16)

Eneo la pili Paulo anatoa ufahamu hasaa juu ya hekima anayoitambua Mungu, akionyesha kuwa hekima ya ulimwengu huu, kwa Mungu ni upuzi, bali hekima ya Mungu ameificha ndani ya Kristo Yesu, na hivyo amewachagua watu wadhaifu na wanyonge kuwadhihirishia hiyo. Akionyesha kuwa mtu asitegemee sana kumwona Mungu katika mambo yanayodhaniwa kuwa ni makuu, bali katika Kristo Yesu.

1 Wakorintho 1:24

[24]bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. 

3) Nidhamu ya kimwili ndani ya kanisa la Kristo, (1Wakorintho 5-6)

 Katika eneo hili Paulo anastaajabishwa kwa kuzuka kwa zinaa mbaya ambayo haionekani hata  kwa mataifa yaani mtu na mzazi wake kuzini,. Akiwaagiza kutoa hukumu juu ya watu kama hao, hata kwa kuwakabidhi shetani (lengo ni waponyeke)

Kwasababu wakiachwa mwisho wao huwa ni kulichafua kanisa, (kulitia unajisi), 

Vilevile tunaona Paulo akitoa agizo kuwa kanisa halipaswi kuchangamana na wazinzi.

Akisisitiza kuwa mtakatifu sio tu awe amehesabiwa haki bali pia awe ameoshwa  na kutakaswa na udhalimu wote.

Anawaagiza pia watakatifu hawapaswi kupeleka mashtaka yao kwa watu wa kimataifa, bali kanisa ni zaidi ya mahakama ambayo watakatifu wanapaswa watatulie migogoro yao hapo. 

4) Ndoa na useja. (1Wakorintho 7)

Paulo anaeleza kwa upana, taratibu ya kindoa, katika eneo la haki zao za ndani na kuachana, na wito wa utowashi(useja). Katika eneo la haki, anasisitiza kuwa kila mwanandoa anapaswa atambue kuwa hana haki juu ya mwili wake mwenyewe, bali mwenzake, lakini pia katika kuachana, anaeleza ikiwa mwanandoa mmoja haamini, Yule aliyeamini hapaswi kumwachwa mwenzake, ikiwa bado anataka  kuendelea kuishi naye. Lakini pia anatoa pendekezo lake Mtu akitaka kumtumikia Mungu kwa wepesi zaidi bila kuvutwa na mambo ya mwilini na dhiki za kiulimwengu. Basi akikaa bila kuoa/kuolewa afanya vema zaidi.

5) Uhuru wa mkristo.(1Wakorintho 8-10)

Anaeleza jinsi gani mkristo anapaswa kukabiliana na dhamiri yake na ile ya wengine,katika maamuzi ayafanyayo kwa ujuzi wake,  akigusia eneo la vyakula (hususani vile vilivyotolewa sadaka kwa sanamu), kwamba hivyo havituhudhurishi mbele za Mungu, lakini tukila pia tuangalie wengine wanaathirikaje. Tusije tukawakwaza kwa ujuzi wetu. Paulo anaeleza ili tuweze kufikia hapo yatupaswa kuyafanya yote katika upendo.

1 Wakorintho 8:11-13

[11]Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. 

[12]Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo. 

[13]Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu. 

Lakini pia anaeleza haki waliyonayo mitume, kwamba wanaouwezo wa kula katika fungu la kanisa, lakini hawakutumia ujuzi wao wote, ili waweze kuifikisha injili kiwepesi kwa watu bila kuwazuilia na wengine.

6) Adabu na nidhani katika kukusanyika ndani ya  kanisa la Mungu( 1Wakorintho 11)

Paulo anatoa utaratibu wa ki-Mungu wa namna ya kuhudumu, kufuatana na hali ya kijinsia. Kwamba kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha mwanamume ni Kristo na kichwa cha Kristo ni Mungu. Hivyo mwanawake anapaswa wafunikwe vichwa awapo ibadani, ili kuonyesha kichwa chake(mumewe) kinamilikiwa na Kristo. Na kwamba wanawake wanapaswa watii uongozi (1Wakorintho 14:34-40)

Paulo anaeleza pia nidhani katika kushiriki meza ya Bwana, kwamba inapaswa ifanywe katika ufahamu na utaratibu sahihi wa rohoni, vinginevyo itapelekea hukumu badala ya baraka

7) Karama za Roho (1Wakorintho 12-14)

Paulo anazungumzia kwa undani karama mbalimbali ambazo Mungu ameziweka katika kanisa na kwamba zinapaswa ziwe kwa lengo la kufaidiana na kujengana. Lakini anaeleza kipawa kilicho bora zaidi ya karama zote, nacho ni upendo, ambacho anakieleza kwa urefu katika sura inayofuata ya 13, kwamba hichi kimezidi vyote.

1 Wakorintho 13:1-8

[1]Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. 

[2]Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. 

[3]Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. 

[4]Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; 

[5]haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; 

[6]haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; 

[7]huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. 

[8]Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. 

8) Kufufuliwa kwa wafu. (1Wakorintho 15)

Katika eneo hili Paulo anahimiza  fundisho la kufufuliwa kwa wafu, akionyesha jinsi lilivyo umuhimu katika imani ya kikristo, na hiyo ni kutokana na baadhi ya watu waliozuka ndani ya kanisa kufundisha fundisho la kisadukayo kwamba hakuna ufufuo wa wafu. 

Akieleza jinsi Bwana atakavyokuja kwamba siku ya kurudi kwake parapanda italia na wote kwa pamoja (tulio hai na waliokufa) tutaipokea miili mipya ya utukufu itokayo mbinguni.

9) Michango kwa watakatifu. (1Wakorintho 16)

Katika sehemu hii ya mwisho Paulo anawaagiza juu ya utaratibu wa changizo kwa ajili ya watakatifu, kwamba vifanyike kila siku ya kwanza ya juma wakutanikapo, anawaagiza pia wakeshe, wawe hodari, na mambo yao yote yatendeke katika upendo.

Kwa hitimisho ni kuwa waraka huu unalenga hasa marekebisho, juu ya mambo mengi yaliyokuwa yanatendeka kwasababu ya ujinga, upumbavu, na dhambi ndani ya kanisa la Kristo. Na Ukweli ni kwamba mambo kama haya haya ni rahisi kuonekana hata katika kanisa la leo. Waraka huu tuusomapo yatupasa tuutazame kwa jicho la kikakanisa je! makosa kama ya wakorintho yapo katikati yetu, kama ni ndio basi tujirekebishe haraka sana.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Warumi.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments