Swali: Kuna utofauti gani uliopo kati ya Hasira ya MUNGU na Ghadhabu ya MUNGU?
Jibu: Kujua tofauti yake turejee mistari michache katika biblia..
Zaburi 6:1 “Bwana, usinikemee kwa HASIRA YAKO, Wala usinirudi kwa GHADHABU YAKO”.
“Hasira” ni hisia ya “kuchukizwa” inayompata mtu kutokana na tendo Fulani baya alilofanyiwa, au lililomtokea kinyume na matakwa yake. Hii ni hisia ya ndani ambayo inaweza kumfanya mtu apoteze hamasa, au hamu au shauku ya jambo Fulani.
Lakini “Ghadhabu” yenyewe inaenda mbali zaidi haiishii kumfanya mtu ajisikie tu vibaya na kujitenga bali inampeleka kuadhibu, au kulipiza kisasi.
Kwamfano kuna mtu aliyepigwa na mwenzie, akaishia kukasirika na kujitenga na Yule mtu, (Huyu anahesabika kuwa anazo hasira, kakasirika).. Lakini kuna mwingine anaweza kupigwa na mwenzake asiishie tu kukasirika lakini akarudisha mapigo, sasa huyu maana yake kaghadhibika, hivyo hasira yake imerudisha majibu hasi kwa aliyemtendea.
Sisi wanadamu tuna hasira lakini pia tunazo ghadhabu.. Ila Biblia imetuonya tusiizalie matunda hasira hata kuwa ghadhabu.. kwasababu hasira iliyozidi hata kutenda dhambi ndio ghadhabu..
Waefeso 4:26 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;
27 wala msimpe Ibilisi nafasi”.
Kwanini Biblia imezuia tusiwe watu wa kuwa na hasira ya kupitiliza?… Ni kwasababu hisia zetu zina mapungufu na hukumu zetu si kamili..
Lakini hukumu za MUNGU ni kamili kwani MUNGU anayo hasira na pia Ghadhabu.. Lakini mpaka ghadhabu ya MUNGU imemwaga basi ni hakika kuwa tumestahili, lakini sisi wanadamu hatujapewa ruhusa ya kuwa na ghadhabu, kwasababu hukumu utakayompimia mwenzako MUNGU akikuangalia nawe pia unastahili hiyo hiyo kwa makosa yako mengine (Mathayo 7:1), Lakini yeye MUNGU akihuhukumu hana wa kumhukumu kwakuwa ni mkamilifu, hivyo hukumu zake ni kamili!.
Na pia ni kwa maarifa ya ziada ya kujua ni hasira ya namna gani ambayo tumepewa ruhusa ya kuwa nayo, fungua hapa>>MWE NA HASIRA, ILA MSITENDE DHAMBI.
Sasa Maandiko yanasema MUNGU aliyetuumba si Mwepesi wa hasira (maana yake hakasiriki haraka) lakini ni Mwingi wa hasira (maana yake hasira yake inafikia kiwango cha ghadhabu), cha kuadhibiwa na kujilipiza kisasi,.
Nahumu 1:2 “Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; BWANA HUJILIPIZA KISASI JUU YA ADUI ZAKE, huwawekea adui zake akiba ya hasira.
3 BWANA SI MWEPESI WA HASIRA, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; Bwana ana njia yake katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake”.
Kilichowapata watu wa nyakati za Nuhu ni Ghadhabu ya MUNGU, kilichowapata watu wa nyakati za Sodoma na Ghomora ni Ghadhabu ya MUNGU!, Ndio maana hawakupona, na kitakachotokea kwa dunia ya wakati wa Mwisho ni Gadhabu ya MUNGU, soma (2Petro 3:6-7 na Ufunuo 16:1).
Na MUNGU anaweza kuimimina Ghadhabu yake kwa Mtu mmoja, na kwa watu wengi kwa pamoja au kwa dunia nzima.. Mtu anayefanya dhambi kwa makusudi yupo katika hatari ya kukumbana na ghadhabu ya MUNGU yeye kama yeye…
Wakolosai 3:5 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;
6 KWA AJILI YA MAMBO HAYO HUJA GHADHABU YA MUNGU”.
Hivyo Biblia (Neno la MUNGU) linatufundisha kuiogopa Ghadhabu ya MUNGU kwa kutembea katika mapenzi yake na pia kujizuia sisi na ghadhabu kwasababu hasira ya mwanadamu haiitendei haki ya MUNGU.
Yakobo 1:19 “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; WALA KUKASIRIKA;
20 KWA MAANA HASIRA YA MWANADAMU HAIITENDI HAKI YA MUNGU.
21 Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu”.
Mithali 15:1 “Jawabu la upole hugeuza HASIRA; Bali neno liumizalo huchochea GHADHABU”.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
BWANA SI MWEPESI WA HASIRA, LAKINI BWANA NI MWINGI WA HASIRA.
KIKOMBE CHA GHADHABU YA MUNGU KINAJAA.
NIMEAZIMIA KUWAKUSANYA MATAIFA. NIPATE KUWAMWAGIA GHADHABU YANGU
Biblia inamaana gani kusema ‘maana Mungu wetu ni moto ulao’ (Waebrania 12:29)
About the author