Nehemia 8:10 “Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU”.
Hapa anaposema “Furaha ya Bwana ni Nguvu zetu” hamaanishi “kufurahi kwa Bwana ndio Nguvu zetu”, hapana bali anamaanisha “Furaha yetu sisi katika Bwana ndiyo Nguvu yetu”.. Maana yake tunapofurahi tukiwa ndani ya MUNGU hiyo ni Nguvu kwetu..
Neno la Mungu linasema katika 1Wathesalonike 5:16 na Wafilipi 4:4 kuwa tufurahi siku zote katika Bwana..
Wafilipi 4:4 “Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini”
Furaha ya Bwana inapokuwa ndani yetu, ndivyo tunazidi kupata NGUVU za mambo yote.. Sasa tunaivutaje Furaha ya MUNGU ndani yetu?..Kwa mambo haya sita (06), furaha ya Mungu itaingia ndani yetu.
1. KUOKOKA
Mwimbaji mmoja wa Tenzi no. 22, (wimbo; Kale nilitembea) alisema hivi katika ubeti mmoja …
“ Hicho ndicho chanzo cha kufurahi kwangu, hapo ndipo mzigo uliponitulia…
usifiwe msalaba, lisifiwe kaburi linalozidi yote, asifiwe Mwokozi”.
Akimaanisha Msalaba ndio chanzo cha kwanza cha Furaha yake, na hiyo ni kweli kabisa.. Mtu aliyemkimbilia YESU huyo kafungua mlango wa kwanza wa mkondo wa Furaha katika maisha.. kwasababu yeye mwenyewe alisema tukienda kwake atatupumzisha na mizigo tuliyotwikwa na shetani na tutapata raha.
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”
2. MAOMBI.
Huu ni ufunguo wa pili wa Furaha ya kiMungu.. Bwana YESU alisema tuombe ili furaha yetu iwe timilifu..
Yohana 16:23 “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.
24 Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu”.
Unapokuwa mwombaji wa mara kwa mara, ukiwa binafsi au katika kikundi cha maombi, kamwe huwezi kupungukiwa Furaha, kwani maombi yanaumba Furaha ya kiMungu yenyewe ndani ya mtu.
3. KULIISHI NENO LA MUNGU.
Huu ni ufunguo wa tatu wa Furaha ya Mungu: Tunapolitenda Neno la Mungu/amri za Mungu moja kwa moja Furaha ya Bwana inaumbika ndani yetu, ambayo ndio chanzo cha nguvu yetu.
Yohana 5:10 “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
11 Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na FURAHA YENU ITIMIZWE”.
4. KUIFANYA KAZI YA MUNGU.
Huu ni ufunguo wa Nne wa Furaha ya kiMungu ndani.. Unapojishughulisha na kazi yoyote ya Mungu, iwe kuhubiri mitaani, au kufanya huduma kanisani, au kumtolea Mungu sadaka, au shughuli nyingine yoyote ile ya kikanisa au nje ya kanisa inayohusu ufalme wa Mbinguni, hiko ni chanzo kikubwa sana cha Furaha ya kiungu, ambacho ndicho chanzo cha Nguvu za MUNGU.
Watu wenye kumtumikia Mungu kwa nguvu zao au mali zao wamejaa furaha siku zote.. hata kama watapitia vipindi vya huzuni, lakini kwa kipindi kifupi sana Furaha yao inarejea na wanakuwa na nguvu nyingi za rohoni, wanapotazama matunda ya kazi yao katika Mungu furaha yao inaongezeka.
2Wathesalonike 2:19 “Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji ya kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu Yesu, wakati wa kuja kwake?
20 Maana ninyi ndinyi utukufu wetu, NA FURAHA YETU”.
5. KUMSIFU MUNGU.
Huu ni ufunguo wa tano wa Furaha ya kiMungu, tunapomsifu Mungu katika Roho na Kweli, Furaha ya kiMungu inaumbika ndani yetu.. na matokeo ya Furaha hiyo ni Nguvu ya Mungu..
Zaburi 43:4 “Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu, kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, Mungu wangu”.
Msifu Mungu kwa vitu unavyoviona, msifu Mungu kwa uumbaji wake, msifu kwa upendo wake, msifu kwa miujiza yake n.k
6. KUSOMA NENO LA MUNGU.
Hiki ni chanzo sita cha Furaha Mungu, Mtu anayesoma Neno la Mungu maisha yake yatatawaliwa na Furaha tu siku zote..
Yeremia 15:16 “Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na MANENO YAKO yalikuwa ni FURAHA KWANGU, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi”.
Ukiwa na Furaha ya Mungu utakuwa na Nguvu ya Kuendelea mbele katika mambo yote, utakuwa na nguvu ya kuomba, utakuwa na nguvu za kusubiri, utakuwa na nguvu ya kuinua wengine nk n.k.
Anza leo kuitafuta Furaha ya Mungu kwani hiyo ndio Nguvu yako, na kama tayari ipo ndani yako basi zidi kuipalilia kwa kufanya mambo hayo sita na mengine yanayofanana na hayo.
Mungu akubariki.
Maran atha!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
MWIMBIE BWANA ZABURI KATIKA NYAKATI ZA FURAHA.
IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.
MUNGU HAJARIBIWI NA MAOVU BALI MEMA.
About the author