SWALI: Yule tajiri alimaanisha nini kumwambia Lazaro, achovye ncha ya kidole chake majini uuburudishe ulimi wake?
Luka 16:24
[24]Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
JIBU:
Habari hiyo la Tajiri na Lazaro, Bwana Yesu aliieleza kufunua uhalisia wa jehanamu jinsi ulivyo… Na mambo ambayo mtu aliyeukataa wokovu atakutana nayo baada ya kifo.
Anaeleza jinsi yule tajiri alivyokufa katika hali ya dhambi..na hatimaye akajikuta mahali pale pa mateso, ambapo hakutana hata ndugu zake wafike, tunaona hata alipoomba mtu atokaye kwa wafu aende kuwahubiria ndugu zake akaambiwa hawatashawishwa…Ni kuonyesha kuwa mahali pale palikuwa pa mateso Sana, kiasi cha kutaka mwingine yeyote kufika.
Lakini tukio lingine tunaonyeshwa akimwomba Ibrahimu Amruhusu Lazaro achovye ncha ya kidole Chake majini amburudishe ulimi wake, nalo pia akaambiwa haiwezekaia kwasababu kuna kizuizi kikubwa Sana katikati yao.
Sasa swali linakuja tukio lile linamaana gani Je kiu kile ni halisi au ni ufunuo?.
Bwana Yesu alipokuja duniani.. aliona Dunia nzima ina Kiu kikubwa sana.. na hivyo inahitaji maji ya kuweza iponya.
Sasa maji inayohitaji sio haya ya mtoni..bali maji ya rohoni ambayo ni ya uzima, na mtu pekee awezayo kutoa hayo ni yeye mwenyewe..hakuwahi kutokea mtu aliyeweza kuyatoa.
Kama tunavyojua mwili ukikosa maji, mwishowe utakufa..Ndivyo ilivyokuwa sisi sote, hapo mwanzo kabla ya Kristo, Wote tulikuwa wafu kiroho..
Utauliza vipi kwa watakatifu wa kale kama akina Musa na Eliya?…Wale walikuwa wanaishi kwa ahadi ya Kristo, Hivyo walitii madhihirisho yake aliyokuwa akijifunua kwao kwa namna mbalimbali huku wakiiongejea ahadi kamili ya ukombozi ambayo alikuja kuikamilisha yeye mwenyewe (Yesu Kristo) alipofufuka Katika wafu..(waebrania 11)
Yeye mwenyewe Alisema..
Yohana 7:37-39
[37]Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.
[38]Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.
[39]Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.
Sasa kiu hii ni ya nini?
Ya maisha….
Tangu zamani mwanadamu amekuwa akitafuta ‘maisha’ ambayo hata sasa hajayapata…ndio maana wengi wanakimbilia kutafuta elimu, fedha na utajiri wakidhani kuwa ndio wamepata maisha, lakini hivyo vipo mbali sana na maisha …vitakufanya ule vizuri tu, unywe vizuri, ulale vizuri kama maandalizi ya heri ya kifo chako baadaye..kwasababu Haviwezi kukudumishia maisha.. vinapooza tu kiu..lakini haviondoi kiu.
Yesu amekuja kuondoa kiu.
Sasa watu Ambao watapuuzia kuyapokea maji hayo ambayo Yesu anatupa…wakifa Katika hali hiyo hiyo huko waendapo ni majuto makubwa.
Kwasababu watataka hata tone dogo la maji hawatapata…yaani kiwango kidogo tu cha neema ya uzima hawatapata…
Leo Yesu hatupi maji tu, kwa kipimo fulani bali anapanda kabisa chemchemi za maji ndani yetu Ambazo zinabubujika uzima wa milele.
Yohana 4:14
[14]walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
Madhara ya kukosa maji ya uzima si tu baada ya kufa…hata hapa Hapa duniani.. mtu ambaye hana Kristo rohoni anajulikana kama nchi kamena matokeo yake ni kuwa makao ya mapepo yanakuwa Ndani yake hata kama hujui..
Angalia Yesu alichokisema juu ya hilo.
Mathayo 12:43-45
[43]Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.
[44]Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.
[45]Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.
Yanakwenda mahali pasipo na maji…yaani moyo ambao hauna Kristo ndani yake.
Ndugu…umeona hatari waliyonao wenye dhambi, hapa duniani na baada ya kifo?
Shetani asikupumbaze, tubu leo kwa kumpokea Bwana Yesu katika maisha yako ili upate ondoleo la dhambi zako haraka sana.
Hizi ni siku za mwisho, dunia hii inakwisha…vilevile hujui ni siku Gani utakufa…Acha kuchezea maisha yako, ukafanana na yule tajiri aliyekosa maji ya uzima angali akiwa hai.
Okoka leo..
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
About the author