FUNGUA KINYWA CHA ROHO MTAKATIFU KIHUDUMU.

FUNGUA KINYWA CHA ROHO MTAKATIFU KIHUDUMU.

Ahadi mojawapo ya Roho Mtakatifu Kwa wote waliompokea ni kupewa uwezo wa kuzungumza “ufahamu wa Mungu”, kwa vinywa vyao.

Ufahamu huu unaweza kujifunua katika maumbile mbalimbali aidha kwa kueleza habari zilizopita, au habari zijazo, au zinazoendelea sasa hivi, au kutoa maelekezo, au faraja, au neno la hekima, au maarifa, au uponyaji au baraka..Namna zote hizi kwa lugha rahisi kuitwa utabiri/ unabii.

Ukiwa kama mwamini ni vema kufahamu sehemu kubwa sana ambayo Roho Mtakatifu anaitumia kuhudumu ni katika vinywa vyetu. Ndio maana siku ile ya kwanza ya pentekoste aliposhuka, alikaa juu ya wale watu kama “ndimi za moto”. Maana yake ni kuwa huduma yake hasaa hujidhihirisha katika ndimi…ndio maana akaweka moto wake juu ya ndimi zao, lugha zao zikabadilishwa wakaanza kunena kwa lugha mpya.

Kwahiyo kinywa cha mtu aliyeokoka, ni kinywa cha Mungu duniani. Usipojifunza kukifungua kinywa chako kiufasaha, ujue hiyo ni namna mojawapo ya kumzimisha Roho Mtakatifu ndani yako.

Watu wengi hawajui kuwa kila mmoja amepewa uwezo wa kutabiri/ kuhutubu na sio suala la huduma fulani ya kinabii tu, hapana utauliza hilo lipo wapi kwenye maandiko? Soma..

Matendo 2:17 wana wenu na binti zenu watatabiri..

Lakini pia 1 Wakorintho 14:31. Inasema..

[31]Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe.

Kuhutubu kama ilivyotumika hapo, ni kutabiri/ kusema ufahamu wa Mungu. Jambo ambalo ni la wote sio baadhi.

Sasa unafunguaje kinywa cha Roho Mtakatifu na unafanya hivyo katika mazingira gani?

Usisubiri mpaka karama fulani ije juu yako, yaani kuonyeshwa/kufunuliwa.. hapana…kwasababu tayari una Roho Mtakatifu ndani yako anza kusema maneno yanayolanda na ahadi za Neno la Mungu, bila kufikiri- fikiri

Kwamfano…

Umepelekwa kwenye mashtaka fulani kwa ajili ya Neno. Au unatakiwa uwasilishe hoja, au ufundishe Neno, au uhubiri, au umekwenda mtaaani kushuhudia.. usianze kusema mimi nitawezaje kuhubiri, au kujieleza, sijui sheria, sijui vizuri biblia, sijui kupangilia maneno…hupaswi kufikiri hivyo. bali ukumbuke ulishapewa kinywa cha moto, tangu siku ulipoamini, wewe nenda kisha anza kuzungumza huko huko katikati ya maneno yako Roho Mtakatifu ataunganika na wewe.

Mathayo 10:18-20

[18]nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.

[19]Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.

[20]Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.

Mwingine atakuambia mimi siwezi kuomba masafa marefu ninaishiwa na maneno…ndugu hupaswi kukatisha maneno na kuacha Kuomba, ukaenda kulala.. endelea kutafakari huku ukizunguza na Mungu wako Habari mbalimbali za kwenye maandiko, na ghafla tu baada ya muda kidogo utaona unaingia kwenye mkondo fulani wa kimaombi, linatoka neno hili kwenye ufahamu linakuja neno hili la kuombea…ulikuwa umepanga uombe Saa 1, unajikuta unaomba matatu.hapo ni Roho Mtakatifu amekupa Kinywa cha kuomba..na ndani ya maombi hayo ni utabiri tosha, kwasababu sio ufahamu wako, bali ni wa Mungu ndani yako.

Vilevile jifunze kutoa sauti katika uombaji wako wa mara kwa mara..ndio tunafahamu Maombi sio sauti, hata kimoyo- moyo Mungu anasikia, lakini usimzimishe Roho..

Watu wengi wanatamani kunena kwa lugha lakini, wanazuia vinywa vyao kutoa sauti.. wanategemea vipi wanene kwa lugha mpya..unapojiachia Kwenye maombi huku unatoa sauti ni rahisi sana kujazwa Roho Na kuomba kwa lugha.

Eneo lingine labda mtu ni mgonjwa..anahitaji maombi…Fungua kinywa chako kwa ujasiri mtamkie uponyaji…unaweza kudhani ni maneno yako, hujui kumbe Ni Roho Mtakatifu Ameyaingilia na kulifanya tayari kuwa Neno la kinabii la uponyaji, na hatimaye anapokea uponyaji wake saa hiyo hiyo.

Uwapo na Watoto wako, Acha kuzungumza nao, habari za kidunia dunia tu..wawekee mikono wabariki kwa Imani kama vile Isaka alivyowabariki Yakobo na Esau na maneno yale yakawa kweli. Vivyo hivyo na wewe tabiri juu ya watoto wako unataka wawe nani wawapo watu wazima.

Uwapo kazini na marafiki zako, penda kuzungumza maneno ya ki-Mungu wakati mwingi kwasababu huko huko unabii unaweza kupita bila wewe kujijua… mwangalie kayafa

Yohana 11:49-52

[49]Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote;

[50]wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima.

[51]Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo.

[52]Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja.

Hivyo kinywa cha ni kinywa cha Roho Mtakatifu usikifunge Bali kijaze Maneno ya Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

VIASHIRIA VINGINE VYA ROHO MTAKATIFU KUWEPO NDANI YAKO.

TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.

KWA KUWA ROHO BORA ILIKUWA NDANI YAKE.

Print this post

About the author

Devis administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments