Jina
Bwana wetuYesu libarikiwe. Ni siku nyingine tena Bwana ametupa neema
kuiona hivyo nakukaribisha ndugu popote pale ulipo tushiriki pamoja
Baraka Bwana alizotuandalia leo.
Tukisoma Zekaria 12:9-14, inasema.
“ 9 Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu.
10 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.
11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.
12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;
13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.
14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.
Watu wanaozungumziwa hapo ni wayahudi (yaani Waisraeli) ,
Embu leo jiulize tu Israeli ni Taifa dogo sana kama mkoa wa njombe, ni
taifa ambalo huwezi hata ukaenda na kukutana na vitu vya kuvutia huko au
vya kushangaza kama mataifa mengine makubwa, lakini ni kwanini leo hii
imekuwa ni JICHO LA DUNIA?. Wapo
mbali na Mungu lakini ni watu wenye akili na wenye mafanikio makubwa
duniani, jiulize siku wakiwa karibu na Mungu itakuwaje?
Hayo
maandiko hapo juu ni lazima yatime, utafika wakati biblia inasema Roho
ya neema itaachiliwa juu yao na watamwamini huyu Yesu ambaye sasa
hawamwamini, Siku hiyo Watalia na kuomboleza baada ya kugundua makosa
yao kuwa Yule waliyemsulibisha na KUMCHOMA MKUKI miaka 2000 iliyopita
kumbe ndiye Masiya waliokuwa wanamsubiria kwa miaka mingi..Ile roho ya
ufarisayo na usadukayo itaondoka juu yao.
Kama vile biblia inavyotabiri kutakuwa na maombolezo makubwa sana huko Yerusalemu wakitubu makosa yao.
Sasa hicho ndio kile kipindi ambacho mtume Paulo alikiandika katika
Warumi 11:25 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili [anasema na sisi watu wa mataifa]; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.
27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao”.
Unaona
hapo unabii huo utatimia katika hiyo siku?, Huo wakati wa Israeli
kurudiwa na kutengwa na maovu yao upo karibuni sana, na utakapoanza tu
basi ujue utimilifu wetu sisi mataifa utakuwa umeshawasili yaani kwa
lugha nyingine neema kwetu itakuwa imeshaondoka na kurudi tena Israeli,
na hiyo itaambatana na tendo KUU la UNYAKUO.
Sasa
wayahudi ambao leo hii utawaona wanalia usiku na mchana pale kwenye ule
Ukuta wa maombolezo (wailing wall). wakimwomba Mungu wa Ibrahimu baba
yao aje kuwaokoa na maadui zao na kuleta utawala wa masihi duniani, ipo
siku hayo maombolezo yatakoma, na ndipo Mungu atawarudia kwa kuwafumbua
macho na kumwona YESU, Kumbuka Mungu aliwapofusha kwa makusudi kabisa
wasimwamini Kristo ili sisi mataifa tuipate neema vinginevyo huyu Yesu
wa thamani ambaye leo hii tunaifurahia neema yake, tungemsikilizia tu
kwa wayahudi, sisi tungeendelea kuwa waabudu miti,vinyago, na wachawi.
Na hata hivyo dunia ungekuta imeshakwisha siku nyingi, wakati ule ule tu
Yesu aliokuwa ndio ungepaswa uwe ni wakati wa wao kurejeshewa ufalme wa
dunia na Yesu.
Unakumbuka
mitume walimuuliza Yesu baada ya kufufuka je! Huu ndio wakati wa
kuwarudishia Israeli ufalme? Yesu akawaambia, sio kazi yenu kujua
nyakati wala majira.(Matendo 1:6), Hii ikiwa na maana kuna wakati utafika watarudishiwa na huyu huyu masihi Yesu Kristo.
Hivyo
huo wakati unafika, Pale Mungu atakaposimama tena upande wa Israeli na
kuwashindania kwa nguvu nyingi kama alivyokuwa anafanya zamani, pale
mataifa yote ulimwenguni yatakapoungana ili yaje kujaribu
kuisambaratisha Israeli katika ile vita ya Harmagedoni ndipo hapo Kristo
atakawapigania toka juu kwa nguvu na uweza mwingi…damu nyingi
itamwagika sana, maadui wote wa Israeli watakufa kama kuku waliochinjwa
wakaachwa, wakati huo Bwana atakapolipigania Taifa lake…. Tunalisoma
hilo katika..
Zekaria 14:1 “Tazama, siku moja ya Bwana inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako.
2 Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali.
3 Hapo ndipo ATAKAPOTOKEA BWANA, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita.
4 Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.
5 Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku zaUzia, mfalme wa Yuda; na Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.
Kwahiyo
tusifurahie tu kuona leo hii Israeli inazidi kufanikiwa lakini badala
yake tuogope na tujiulize maswali je! Wewe tumejiandaaje sasa?, neema
ndio hivyo inaondoka kwetu, tazama hata hali ya ukristo sasa hivi
duniani sio kama ile ya zamani, tazama mataifa ya ulaya ambayo ndio
yalikuwa ya kwanza kutuleta injili lakini sasa jinsi yanavyozidi
kujitenga na ukristo kwa kasi, hiyo ni dalili kuwa neema inaondoka kwa
mataifa, inakimbilia Israeli..Itafika wakati mataifa yote yataenda
kinyume na taifa teule la Mungu hata hili taifa letu vilevile litaungana
na yule mpinga-Kristo ili kuiangamiza Israeli.
Zekaria 12: 3 “Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake”.
Ndugu
wakati huo sio wa kuutamani kwanini tusubirie mpaka hayo yote yatukute
kwa ghafla wakati tunayo nafasi sasa? Neema inamalizikia AFRIKA, usiiche
ikupite, chukua hatua ya kumwamini Yesu ayasafishe maisha yako, ili uwe
tayari kwa unyakuo ulio karibuni kutokea.
Bwana akubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
MAMBO YATAKAYOTOKEA ISRAELI SIKU ZA HIVI KARIBUNI.
WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.
MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.
“WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI”
UNYAKUO.
Rudi Nyumbani
Print this post