SWALI: Nini maana ya hii Mithali 10:25
Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.
JIBU: Mstari huo unajifafanua vizuri kwenye ule mfano Bwana Yesu aliutoa kuhusiana na watu wanaoyasikia maneno yake, halafu hawayatendi. Tusome.
Mathayo 7:24 Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;
25 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.
26 Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;
27 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.
Hivyo tukirejea katika vifungu vile vya kwenye mithali. Unaweza kuelewa mtu asiye haki hasaa ni nani?
Ni Yule ambaye anaisikia injili, halafu hatii. Mtu Yule anayesema ameokoka, lakini zao la wokovu halionekana ndani yake. Rohoni anaonekana hana tofauti na yule ambaye hajamjua Mungu kabisa. Wote hao huitwa wasio haki. Bado wapo dhambini, hawajakombolewa na damu ya Yesu Kristo.
Hawa wataonekana kwa nje kama vile ni watakatifu. Lakini kinapokuja tu kisulisuli aidha cha majaribu, shida, dhiki, udhia,au mapigo kwa ajili ya Kristo, mara ghafla wanarudi nyuma, wanakuwa kama watu ambao hawajawahi kumjua Mungu kabisa, kwasababu hakujikita katika mwamba. Wengine sio majaribu ya shida, bali yale ya mafanikio makubwa, ndio hapo anasa zinawazidi wanamsahau Mungu, wanaiaga imani, kwani walimfuata Yesu kwasababu ya shida tu. Wengine ndoa, elimu, vyeo wakishavipata, huwaoni tena kwa Yesu.
Lakini mtu anayeyasikia maneno ya Kristo na kuyatii, ni kinyume chake, huitwa msingi wa milele. Huyo hatikiswi na wimbi, kisulisuli au dhoruba yoyote. Kwasababu yupo juu ya mwamba.
Okoka, upokee msamaha wa dhambi, kisha ishi kufuata na toba yako, ili uhakika wa kusimama uwe nao wakati wote.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
About the author