Jehanamu au Jehanum ni Neno lenye chimbuko la kiyunani Gehenna, ambalo limetafsiriwa kutoka katika lugha ya kiyahudi ge-hinnom Ikiwa na maana bonde la mwana wa Hinomu.. Hili ni eneo lililokuwa kusini mwa mji wa Yerusalemu, lililojulikana kama Tofethi ambao watu wasiokuwa wanamcha Bwana walikuwa wanalitumia kuwatolea watoto wao kafara kwa kuwapitisha motoni kwa miungu waliyoikuta huko Kaanani. Jambo ambalo lilikuwa ni chukizo kubwa sana kwa Mungu, ambalo nalo pia lilikuwa ni mojawapo ya mambo yaliyowafanya wachukuliwe utumwani Babeli.
Tunasoma hayo katika..
Jeremia 7:30 “Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema Bwana; wameweka machukizo yao ndani ya nyumba hiyo, iitwayo kwa jina langu, hata kuitia unajisi.
31 Nao wamepajenga mahali palipoinuka pa Tofethi, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ili kuwateketeza wana wao na binti zao motoni; jambo ambalo mimi sikuliagiza, wala halikuingia moyoni mwangu.”
Yeremia 19:1 “Bwana akasema hivi, Enenda ukanunue gudulia la mfinyanzi, ukachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa watu, na baadhi ya wazee wa makuhani;
2 ukatoke uende mpaka bonde la mwana wa Hinomu lililo karibu na mahali pa kuingia kwa lango la vigae, ukahubiri huko maneno nitakayokuambia,
3 ukisema, Lisikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi, Angalieni, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, ambayo mtu ye yote akisikia habari yake, masikio yake yatawaka.
4 Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia;
5 nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu;
6 basi, angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo katika siku hizo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu, bali, Bonde la Machinjo.”
2Wafalme 23:10 “Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.”
likabakia kutumika kama dampo la jiji, na bonde la kutupia miili ya watu waovu, pamoja na wanyama waliokufa pamoja na kuchoma takataka na kila aina ya uchafu wote uliotoka mjini..Na hiyo ilipelekea bonde hilo kuwa la kinyaa sana na wakati wote kuwa linawaka moto, na moshi mkubwa unaopanda juu pamoja na harufu kali sana, kutokana na kwamba kila wakati uchafu ulikuwa unaingia..
Sasa zile sehemu ambazo moto ulikuwa haufiki vizuri, kulikuwa na funza wengi sana, ambao walipita katikati ya mizoga ile iliyokuwa imetupwa, ni eneo ambalo hakuna mtu angeweza kukaa hata dakika mbili au kusogea karibu na akawa sawa. Kama ulishawahi kuona jalala kuu la manispaa au jiji basi fahamu kuwa huo ni mfano mdogo sana ukilinganisha na GEHENA ilivyokuwa..bonde hilo lilikuwa linatisha sana. Funza wa jehanamu walikuwa ni wagumu kufa kwasababu walikuwa ni tofauti na funza wengine.
Na ndio maana Bwana YESU alitumia mfano huo, kueleza picha halisi ya kuzimu ilivyo kwa wale ambao watakufa katika dhambi zao. Alisema..
Marko 9:43 “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika;
44 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.] 9.45 Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; [
46 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.]
47 Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum;
48 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.”
Ni wazi kuwa hakuna mtu anayependa kuwepo sehemu yeyote chafu, basi hiyo inatupa chachu pia tujiepushe na kuzimu kwasababu kuzimu ipo kweli na si mahali pazuri hata kidogo huko hakuna raha, ukishajikuta kule, utakuwa katika mateso siku zote ukisubiria hukumu ya siku za mwisho kabla ya kutupwa katika lile ziwa la moto..
Kama upo nje ya Kristo, wakati ndio huu, tubu sasa, mpe Bwana maisha yako naye atakupokea..Na kukusamehe kabisa, kwasababu mbingu amekuandalia wewe, hivyo daima hataki nafasi yako ipotee.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
BWANA ALIMAANISHA NINI KUSEMA “WAACHE WAFU WAZIKE WAFU WAO?.
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.