Neno la Mungu linasema pale tulipo dhaifu ndipo tulipo na nguvu, ikiwa na maana pale tunapokuwa si kitu ndipo tunapoonekana kuwa kitu mbele za Mungu, Bwana Yesu alisema yeye ajishushaye atakwezwa na ajikwezaye atashushwa, pale tunapokataa akili zetu kututawala na kumwachia Mungu azitawale ndipo tutakapofungua mlango na wigo mpana wa kuuona UWEZA wa Mungu zaidi katika maisha yetu.
Na ndio maana mtume Paulo alisema
2Wakoritho 12:9-10″ Naye akaniambia neema yangu yakutosha; maana UWEZA WANGU HUTIMILIKA KATIKA UDHAIFU. Basi najisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili UWEZA WA KRISTO ukae juu yangu.Kwahiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida kwa ajili ya Kristo. MAANA NIWAPO DHAIFU NDIPO NILIPO NA NGUVU.”
Mungu hawezi akawa ni mponyaji kwetu kama hatujawa na madhaifu (mwenye afya haitaji tabibu),mafarisayo na masadukayo YESU alikuwa hana maana kwao kwasababu wao walijiona kuwa wana afya hivyo hawakufaidiwa chochote na uweza wa Mungu katika Yesu Kristo. Kwa kawaida huwa tunashukuru pale tunapotendewa mahitaji yetu, huwezi ukashukuru au ukaomba kama unayo mahitaji yako yote.
Na pia hauwezi kutegemea kama unao uwezo wa kujitegemea. vivyo hivyo na kwa Mungu wetu ili tuweze kuuona UWEZA WAKE, yatupasa tuwe dhaifu mbele zake kwa namna zote, kiasi cha kwamba tujione pasipo yeye sisi hatuwezi lolote. Kwa jinsi tutakavyojiachia kwake kwa kila kitu ndipo tutakapofungua wigo wa yeye kutuhudumia sisi na kuuona uweza wake,
Watoto wa Mungu wamefananishwa na kondoo na sio mbuzi kwasababu kondoo hawezi akajiongoza mwenyewe huwa anamtegemea mchungaji wake kwa kila kitu tofauti na mbuzi wao wana uwezo wa kwenda kujichunga wenyewe hivyo hawahitaji msaada mkubwa sana kutoka kwa mchungaji. Vivyo hivyo Na mtoto mdogo anahudumiwa kwa kila kitu na wazazi wake ikiwemo malazi, chakula, afya, n.k. kwasababu anaonekana dhaifu kwa wazazi wake pasipo wao hawezi kufanya lolote hivyo uweza mkubwa wa wazazi wake unaonekana juu yake,
Kwa jinsi hiyo hiyo na sisi pia tunapaswa tuwe hivyo kwa Baba yetu wa mbinguni, sisi ni watoto kwake tunapaswa tujinyenyekeze kama vitoto vichanga ili tuone uweza wake katika maisha yetu, kumbuka yule mtoto anapojifanya amekua na kutaka kujiamulia mambo yake mwenyewe ndipo kidogo kidogo anapojiachilia kutoka katika mikono ya wazazi wake na uweza wao unavyozidi kupungua juu yake, mpaka inafikia wakati mzazi hana sehemu yoyote kwa mtoto.
Biblia inasema “Mkaribieni Mungu naye atawakaribia”(Yakobo 4:8). hii ikiwa na maana kwa kiwango kile kile tutakachompa Mungu katika maisha yetu, ndicho atakachokitumia kufanya kazi katika maisha yetu. Kama unampa Mungu Jumapili kwa jumapili na yeye atajifunua kwako hiyo hiyo jumapili kwa jumapili, kama ni mwezi kwa mwezi na ndivyo hivyo atakavyojifunua kwako mwezi kwa mwezi, lakini kama ni siku kwa siku ndivyo utakavyomwona siku kwa siku, kwa kiwango kile kile utakachopima ndicho utakachopimiwa biblia imesema.
Kama umempa Mungu asilimia 20 ya maisha yako ayatawale ataonekana kwako katika hiyo asilimia 20 usitegemee zaidi ya hapo, kama umempa 70% ataonekana katika hiyo 70, kama umempa 100% ataonekana katika hiyo 100% kama Bwana YESU alivyompa Baba yake. Maana uweza wa Mungu unatimilika katika udhaifu na udhaifu huu ni pale unapokataa kuzitegemea akili zako na kuwa kama mtoto mchanga mbele zake.
Nakumbuka kipindi cha nyuma zamani kidogo tulikuwa tumepanga chumba sehemu fulani na kila mwisho wa mwezi tulikuwa na desturi ya kulipia bill ya umeme lakini ilifika wakati fulani hatukupata pesa ya kulipia na hatukuwa na chochote mfukoni lakini tulimwamini Mungu na kumwachia yote, tukasema kama Mungu wetu yupo atatupigania, maana hao wadai pesa za umeme ni watu wakorofi ukipitisha tu siku moja haujalipia ni balaa umelianzisha, lakini ulipofika mwisho wa mwezi hatukuwa na chochote mfukoni,
cha ajabu wale wadai-umeme hawakuja siku hiyo kudai pesa ya umeme na sio desturi yao, vyumba vingine vyote walienda kulipa kilikuwa kimebaki chumba chetu tu! lakini ni kama walipigwa upofu hivi hawakuja, ukaingia mwezi mwingine, tarehe 1,2,3……mpaka tarehe 24 tulikuwa bado hatujalipa deni la mwezi uliopita na kweli hela hatukuwa nayo na umeme tunaendelea kutumia lakini tulimwachia Mungu yote tulisema liwalo na liwe hatutamkopa mtu,
nakumbuka siku hiyo hiyo pia gesi ya kupikia iliisha kwahiyo matatizo yakaongezeka, lakini ilipofika tarehe 25 mida ya jioni huku tukiwa na mawazo tulifungua simu tukakuta sh.48,000 kwenye mpesa hatukujua imetoka wapi, haijatumwa na mtu yoyote, wala hakuna jina wala message ya kuonyesha mtu katuma pesa, ni kama vile iliongezeka katika account ya m-pesa. tukaenda kuitoa jioni ile ile cha ajabu saa hiyo hiyo baada ya kuitoa hiyo pesa wale wadai-umeme wakafika na ghadhabu wanataka pesa yao ya umeme ya mwezi uliopita, tukawapa saa ile ile, sh.15,000 kiasi kilichobaki tulinunua gesi na matumizi mengine.. Bwana amekuwa akituonekania sisi watoto wake kwa namna hii mara nyingi tu na kwa njia nyingi.
Lakini tungesema tujiongeze tukakope pesa hakika uweza wa Mungu tusingeuona maana yeye anasema zaburi 46:1″ Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, MSAADA UTAKAOONEKANA TELE WAKATI WA MATESO.” pale tutapokuwa dhaifu na kumwachia yeye ndipo tutakapouona uweza wa Mungu, wana waisraeli wasiongeweza kuona bahari inagawanyika kama wasingekutana na kizuizi cha bahari, wasingekula mana kama wasingepita jangwani, wasingepasuliwa maji miambani kama wasingekuwa na kiu, Hivyo pale unapomkabidhi Mungu mambo yote atawale katika misukosuko pasipo kutafuta njia mbadala ya akili zako, ndipo uweza wa Mungu utakapoonekana.
Vivyo hivyo unapopitia shida fulani, au unapoumwa, au tatizo fulani haraka haraka usikimbilie kutafuta njia mbadala, usianze kutangatanga jua hiyo ndio fursa ya wewe kuuona uweza wa Mungu na ndio yeye anataka iwe hivyo, ndio ni vizuri kwenda hospitali na sio dhambi kwenda hospitali lakini sio kila ugonjwa kukimbilia hospitali ukifanya hivyo uweza wa Mungu utauonaje?,
Naweza nikakupa mfano ulifikia wakati nilikuwa nikipata ugonjwa kidogo nakimbilia dawa lakini ilifika wakati nikasema nataka nimuone Mungu katika maisha yangu, yeye aniponye pasipo kumtegemea mwanadamu wala dawa, nikasema sitameza kidonge cha aina yoyote wala kwenda hospitali, tangu niseme hivyo hadi sasa ni miaka mingi imepita sijawahi kumeza kidonge wala kwenda hospitali, kila ninaposikia hali ya udhaifu ndani yangu, nasema Bwana ndiye daktari wangu ataniponya na kweli ile hali haidumu baada ya muda mfupi narudia hali yangu ya kawaida, kwa kufanya hivyo uweza wa Mungu nauona ndani ya maisha yangu kila siku.
Na kwako wewe ndugu unaweza ukasema mbona sijawahi kumwona Mungu akinifanyia miujiza katika maisha yangu? ni kwasababu wewe mwenyewe hujaruhusu atende kazi ndani yako. haujataka kuwa dhaifu mbele zake kwa kujishusha kuwa kama mtoto,.jambo fulani limetokea chukua iwe ndio fursa ya wewe kumwona Mungu wako usitegemee akili zako, wala mwanadamu wala kitu chochote,mwachie yeye na utauona utukufu wake kila siku.
Hiyo ndio njia pekee itakayokufanya uone UWEZA WA MUNGU maishani mwako na ndio njia Paulo aliyoinena na kuiishi iliyomfanya amwone Mungu siku baada ya siku katika huduma yake. kwa mfano shedraki, Meshaki na Abednego walipohukumiwa kutupwa katika tanuru la moto hawakusita walimwachia Mungu yote na kwa kufanya hivyo waliweza kukutana na Mungu kule na kupelekea Mungu wao kutukuzwa babeli yote, vivyo hivyo na Danieli pia alipotupwa katika tundu la simba aliuona uweza wa Mungu kule, tukiwaangalia pia akina Paulo na Sila walipotupwa gerezani ndipo walipouona uweza wa Mungu pale malaika wa Mungu alipoitetemesha ardhi na kufungua malango ya gereza. Hawa wote ni kwasababu walikubali kuwa wadhaifu kwa ajili ya Bwana hivyo ikawafanya wauone utukufu mkubwa wa Mungu.
Mithali 3:5-6 ” Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zake mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye naye atanyosha mapito yako.”
Amen!
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa msaada wa maombi/Ushauri/ubatizo/mafundisho/Whatsapp: Namba zetu ni hizi:
+255693036618/ +255789001312
Mada Nyinginezo:
NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!
MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI
KWANINI MUNGU AWACHOME WATU KWENYE ZIWA LA MOTO NA HALI YEYE NDIYE ALIYEWAUMBA?
About the author