1Yohana 3:1 “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye”
Katika maisha ya kila mmoja wetu, kuna ushuhuda ambao Mungu ameuandika.Bwana ameruhusu kila mtu apitie hatua mbili kuu muhimu maishani mwake nazo ni KUWA MTOTO, NA KUWA MZAZI ( BABA/MAMA) Mungu hakuona vema mtu atokee tu duniani akiwa mtu mzima bali aliruhusu kwa makusudi kabisa mtu apitie hatua zote hizi mbili,ya kwanza awe mtoto, na kisha awe baba/mama,
Ili kusudi kwamba Mungu atakapojifunua kwetu kama Baba tuweze kumuelewa, kwa namna gani Baba ana nafasi yake katika maisha yetu kwakuwa tumeshayapitia hayo maishani ya kuwa na baba wa mwilini na kufahamu vizuri nafasi yake kwetu, ndio maana akasema ni pendo la namna gani alilotupa baba sisi kuitwa wana wa Mungu, kwasababu malaika hawajafananishwa na wana wa Mungu, kwakuwa hawajapitia njia tunazozipitia sisi wanadamu kama vile kuzaliwa na kuwa baba.
Wao waliumbwa tu katika hali zao walizopo sasa Mtume Paulo alieleza wazi kabisa katika
Waebrania 1:5 “Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?”
kwahiyo tunaona hapa malaika hawakuitwa wana wa Mungu, kwasababu hawajaumbiwa ile hali ya kuwa wana, wala kupitishwa katika maisha ya kuwa wana, biblia inasema wao ni roho zitumikazo ( waebrania 1:14 ” Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?”)
TABIA YA MWANA:
Kama sisi tumepewa neema hii kubwa ya kuitwa wana wa Mungu inatupasa sisi tufahamu jinsi Mwana anavyopaswa kuwa kwa Baba yake ili ampendeze Baba yake, inajulikana kuwa tabia ya mtoto yoyote mdogo hafikirii atakula nini wala atakunywa nini,wala atavaa nini, wala atalala wapi,wala hafikirii kesho itakuwaje, wala hafikirii kuhusu afya yake.
Hizi ni tabia za watoto wote ikiwemo hata mimi na wewe tulivyokuwa watoto wadogo. Ujasiri huo wa maisha anao kwasababu anajua Baba yake yupo na ndiyo yeye anajukumu la kumlisha, kumvisha, kumnywesha,kuiangalia afya yake na kumlinda..mtoto haitaji kumweleza baba yake kuwa anaumwa ni jukumu la baba yake yeye kufahamu, mtoto hawezi kwenda kumsaidia baba yake kuleta chakula nyumbani hiyo haimuhusu mtoto kwasababu mtoto hayatambui hata hayo, na baba hachukizwi kumuona mtoto kuwa hivyo kwasababu anajua huyu ni mtoto tu, hawezi kufanya lolote.
Mtoto siku zote anaujasiri mkubwa sana kwa baba yake, kiasi cha kwamba anaona hakuna mtu mwingine yeyote anaweza akawa mkubwa kuliko baba yake, mtoto hana tabia ya kuweka kinyongo akiadhibiwa na baba yake baada ya muda mfupi ameshasahau, mtoto siku zote huwa anajishughulisha na vitu vidogo vidogo na huwa hatafuti ukubwa na ana tabia ya kupenda kukaa nyumbani na kuamini chochote atakachoambiwa na mzazi wake.
Na sisi kama wazazi tunachukuliana na watoto wetu na kuwapenda sana wakiwa katika hali kama hizo, tunawapenda pale tunapowaona watoto wetu wanavyojitoa kikamilifu kwetu,watiifu na wasio na kiburi, wanaojiachia kwetu..sidhani kama kuna mzazi yeyote anaweza akamchukia mtoto wake akiwa katika hali hiyo kwasababu anajua huyo ni mtoto tu hajiwezi na anahitaji uangalizi wote, na hakuna mzazi asiyemuhurumia mtoto wake, akimwona mtoto wake hana chakula yuko radhi alale njaa yeye ili mtoto wake ashibe, akimwona mtoto wake ana dalili tu ya kuumwa anamuhurumia na kumpeleka hospitali haraka sana. JE! SI ZAIDI KWA BABA YETU ALIYE MBINGUNI??
kumbuka Mungu alitupitisha makusudi katika hatua hizi za kuwa mtoto au mzazi ili tumuelewe Mungu kama Baba yetu ana nafasi gani na umuhimu gani kwetu.
Kama Baba zetu wa mwilini wanaweza kututendea mema yote hayo, kutuangalia na kutuhudumia maisha yetu bure, kutuvisha,kutulisha, kutunywesha, kutupa malazi na kutupa afya pasipo kumlipa chochote si zaidi sana kwa Baba yetu aliye mbinguni??
Kuna mafundisho mengi ya uongo ya shetani na yanafundishwa hata na baadhi ya wanaojiita wahubiri wakisema Mungu wetu ni baba wa rohoni na kwamba yeye anatuhudumia tu kwa mambo ya rohoni na kwamba ya mwilini inatupasa tujihudumie wenyewe.
Lakini biblia inasema
waefeso 3:14-15 “Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa”
Unaona hapo ni ubaba wote unaozungumziwa wa mbinguni na wa duniani sio tu wa mbinguni bali hata na wa duniani pia. Kwa namna ile ile uliyokuwa una mtegemea baba yako hapa duniani akulishe, akunyweshe, akuvishe, na akulinde na kukupa afya vivyo hivyo inakupasa umtegemee Mungu ambaye ni Baba yako hapa duniani kwa mahitaji yako yote ya mwilini na ya rohoni kwa kuwa ni baba wa rohoni pia.
Yesu Kristo alisema katika
Mathayo 6:25-34 ” Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?
26 Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?
27 Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?
28 Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti
29 nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.
30 Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?
31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”
Neno hili shetani ameligeuza na kutoa tafsiri nyingi zinazopingana na maana ya maneno yaliyopo hapo juu.Maneno hayo Bwana Yesu aliyoyazungumza yana maana kama yalivyoandikwa, shetani anafahamu kuwa hii ni SIRI inayobeba uhusiano mkubwa kati ya Baba na Mwana, BWANA YESU anasema msisumbukie maisha yenu mle nini au mnywe nini kwamba baba yetu anajua kuwa hayo yote tunayahitaji, kama vile baba zetu wa mwilini tulivyokuwa watoto walikuwa wanajua yote kwamba tunahitaji kula na kunywa je! si zaidi kwa Baba yetu aliye mbinguni?
Embu jaribu kufikiri juu ya hilo ndugu kwa undani. Pamoja na mambo mengi Bwana Yesu Kristo aliyosema tujifunze kwayo, alisema pia tujifunze kwa kunguru, n.k alisema tutazame kunguru, tujifunze jinsi wanavyokula, na kunywa, na kuishi hawapandi, hawavuni, hawana bima, hawana maghala lakini kila siku wana kula, kunguru anauwezo wa kuishi hadi miaka 80 na hajawahi kumeza kidonge katika maisha yake yote.
Na maua ya mashambani hayafanyi ”KAZI” lakini yanatoa harufu nzuri na rangi nzuri na kuuzwa kwa bei ghali kumbuka hayasogei hata inchi moja..Mungu ambaye ni baba yetu anasema “sisi si zaidi kuliko hao??”
Mathayo 18:3 ” Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni?
Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”
Hapa tunaona Kristo anazungumzia aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni ni yule atakayejinyenyekeza kuwa kama mtoto mdogo. Unyenyekevu uliozungumziwa hapa ni maisha ya mtoto kwa baba yake, ni tabia ya mtoto kwa baba yake na sio kumpigia mtu magoti au kuonyesha utiifu fulani hapana. Kwetu sisi kujinyenyekeza kama watoto ni kujiweka/kujiachia kama watoto kwa baba yetu aliye mbinguni, na kuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni ni kuweza kuyashika na kuyaishi hayo maneno yote BWANA YESU aliyoyazungumza hapo juu kwenye mathayo 6:25-34.(huko ndio kujinyenyekeza kama mtoto) lakini kuwa na upako, au kuwa muhubiri mkubwa, au kuwavuta watu kwa Kristo au kuwa mchungaji au kuona maono au kuomba sana, au kufunga sana, au kwenda kanisani sana hakukufanyi wewe kuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. unapaswa uwe mtoto kwa Mungu(Baba wa mbinguni) kama vile mtoto alivyo kwa baba yake wa duniani.Hivyo ndivyo BWANA YESU KRISTO alivyokuwa hapa duniani kujiachia kwa baba yake wa mbinguni.
Uthibitisho mmoja wapo kuwa wewe umempokea Roho Mtakatifu ni wewe KUFANYIKA KUWA MWANA WA MUNGU
Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;”
na pia katika Warumi..
warumi 8 :14-16 inasema “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.
Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.
Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”
Kwa hiyo uthibitisho kuwa wewe ni mtoto wa Mungu, ni Mungu kwako kuwa kila kitu na unamwona katika maisha yako akikuhudumia kwa mahitaji yote ya mwilini na ya rohoni( kumbuka! sio ya rohoni tu bali hata ya mwilini) hautasumbukia maisha kwasababu unaye baba, wewe sio yatima, baba yako atakuvisha, atakulisha, atakunywesha sikwambii wewe ufanye kazi akunyweshe hapana! ana njia zake mwenyewe, unaweza usifanye kazi kabisa wala kujishughulisha na jambo lolote na akakulisha na kukuvisha, unaweza usiwe na fedha hata kidogo na bado akakuvisha, akakulisha na akakuvisha, njia zake sio njia zetu, unaweza usiende hospitali kabisa na bado akakupa afya,
BWANA YESU alisema Baba yetu anajua kabisa kuwa tunahitaji haya yote yaani tule, tunywe, tuvae, tulale, tuwe na afya, kasema mwenyewe kama yeye anaweza kuwafanyia hivyo ndege wa angani na maua ya kondeni je! sisi sio zaidi?? usimruhusu shetani autangue uhusiano wako wewe na Baba yako aliye mbinguni kwa kumwekea Mungu vikwazo na mipaka kwamba yeye hawezi kukuhudumia mpaka ufanye kazi..sipo kinyume na kazi, unaweza ukafanya kazi lakini Mungu hatumii hivyo tu kukuhudumia wewe…
Je! mtoto anajihangaikia mwenyewe?? ..Mungu alitupitisha huko ili tujue nafasi ya baba kwa mtoto ni ipi?.. Yeye ni Mungu tu na ni baba yako, kama wewe ulivyokuwa mtoto ulikuwa huwezi kuzichunguza njia za baba yako lakini ulikuwa una kula, ulikuwa hufikirii wala kuyasumbukia ya kesho wewe..kwanini leo kesho ikufikirishe sana mpaka ukakosa hamu ya kuishi?.
BWANA YESU alisema msisumbukie ya kesho, kwa kuwa ya kesho itajisumbukia yenyewe..huko ndio kufanyika kuwa mwana.
Sasa sikufundishi kuwa mvivu…Lakini kuwa kama Mwana…Weka mipango yako, ya leo na ya kesho, pia fanya shughuli zako kwa bidii kama kawaida, lakini usisahau kuwa unaye Baba mbinguni, hata hizo shughuli zako zikikwama, hatashindwa kukulisha, wala kukuvisha wala kukutunza… Baba anamfurahia mtoto mwenye malengo yake na mipango yake aliyojiwekea, lakini hafurahii kuona mtoto wake ajihisi kama vile hana mzazi ambaye siku mambo yake yakiharibika atakosa hifadhi..
Petro alipewa ufunuo mkubwa kuwa YESU KRISTO ni nani! ambao Bwana alimwambia Petro juu ya ufunuo huo atalijenga kanisa lake na milango ya kuzimu haitaiweza
Mathayo 16:18 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?
Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.
Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia,
Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”
Ufunuo huu Petro aliopewa sio wa Yesu Kristo kuwa ni Mungu, wala Yesu Kristo kama Mwokozi bali alipewa ufunuo kuwa yeye ndiye MWANA WA MUNGU aliye hai.
Petro kwa kuona jinsi Kristo alivyokuwa anamtegemea baba yake kwa kila kitu, na jinsi baba yake alivyokuwa ana muhudumia kwa mambo yote, akatambua kuwa ule uhusiano ulikuwa ni wa kipekee kama vile wa BABA NA MTOTO WAKE. Hakukuwahi kutokea mtu yeyote katika torati au huko nyuma ambaye alishawahi kuwa na mahusiano ya kama baba na mtoto kwa Mungu, hiyo ilionekana kwa Yesu Kristo tu na ndio maana Petro alipewa ufunuo huo na Mungu jambo ambalo lilifichwa hata kwa baadhi ya mitume.
Sauti ilisikika kutoka mbinguni Yohana alipokuwa akibatiza na Yohana pekee yake ndiye aliyeusikia huo ufunuo
Mathayo 3:17 “na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye”.
Hapa Kristo hakushuhudiwa kama yeye ni Mungu au mfalme(ingawa Yesu Kristo alikuwa ni Mungu na Mwokozi) bali alishuhudiwa yeye kuwa ni Mwana wa Mungu .
Chunguza tena maisha yako je! wewe ni kweli mwana halali au mwana haramu. mwana halali anaonekana kwa maisha yake anayoyaishi na uhusiano wake yeye na baba yake vilevile na mwana haramu anaonekana kwa maisha yake jinsi alivyo na mambo yake mwenyewe, hapendi kujishughulisha na mambo ya baba yake, asiyeweza kuadhibiwa anapokosea(kurudiwa), hamtegemei baba yake,
Je! Umepokea Roho Mtakatifu?? kama umepokea Roho wa Mungu atakushuhudia katika maisha yako kuwa wewe ni mtoto wa Mungu kwasababu maandiko ndivyo yanavyosema
Warumi 8 :14-16 inasema “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.
Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.
Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;“
MUNGU AKUBARIKI!
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NIFANYAJE ILI NI NIJUE KUWA UAMUZI NINAOUFANYA NI MAPENZI YA MUNGU?
NI KOSA GANI DAUDI ALILOLIFANYA KATIKA KUWAHESABU WATU?
Moja ya somo ambalo limegusa maisha yangu ni hili jamani sijui nisemeje ila Mungu awainue zaidi, hii ndio injili nilikuwa naitafuta kwa muda mrefu sana, fanyeni hima muwafikie wengi najua sio wote wataipenda au kukubali, lakini Yesu alisema kondoo wake wanajua sauti yake kutokwa machozi, Mungu awabiriki Sana Sana Sana na awainue kazi yenu ni njema Sana.
About the author