Luka 19: 37 “Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,
38 wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.
39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. 40 Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, MAWE YATAPIGA KELELE”.
Zamani nilijua kuwa Mimi nisipofanya kazi ya Mungu, basi kazi ya Mungu itasimama katika eneo nililopo..Ndivyo nilivyokuwa nafikiri hivyo kwa muda mrefu sana..Nilijua tunapoihubiri Injili ni kama tunamsaidia Mungu, kwamba pasipo sisi kujitoa basi watu wengi hawataokolewa..Na ndivyo nilivyofundishwa hata mimi.
Lakini namshukuru Mungu, nilikuja kuelewa zaidi ya hapo…kwamba Mungu hasaidiwi kazi, wala hajalemewa na kazi, wala haitaji msaada wowote kutoka kwa Mwanadamu…Mungu alipoiumba dunia na watu ndani yake, hakuiweka pasipo mipango kama sisi wanadamu tunavyofanya kwamba tunafikia mahali tunabanwa na majukumu yanayotuumiza kichwa mpaka wakati mwingine tunakata tama ya kuendelea..
Mungu hayupo hivyo, alipoumba kila kiumbe chini ya jua alikwisha kiwekea sehemu yake katika dunia kwamba kitazaliwa wapi, kitahitaji kiasi gani cha chakula mpaka kife, kitahitaji hewa ya ujazo kiasi gani n.k …Hayo yote Mungu alishayaweka kabla hata ya hicho kiumbe kuzaliwa au kuwepo..
Kadhalilka na kila mwanadamu anayezaliwa chini ya Mbingu, Bwana alishampangia azaliwe wapi, aishi miaka mingapi, ale chakula kiasi gani, aokolewe wakati gani, afe wakati gani n.k Kwahiyo mwanadamu anapozaliwa ni kama anakuja tu kutimiza maandiko kwa yale aliyoandikiwa.
Kwahivyo basi hakuna mwanadamau yoyote anayeweza kumsaidia Mungu majukumu yake…Yeye mwenyewe anatenda kazi zake kama alivyopanga…Kama alipanga nchi ya Tanzania ifikie idadi ya watu milioni 60 mpaka mwishoni mwa mwaka 2019..penda tusipende hiyo idadi itafika tu!!..Hata kama mtu fulani akatae kuzaa watoto…hiyo haizuii idadi ile kufika..Bwana atatumia wengine kufidia nafasi yake.
Kadhalika tunapokuja katika suala la watu kuokolewa..Bwana Yesu alisema “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu asipovutwa na Baba aliyenipeleka”..Sentensi hii inaonyesha kwanza wokovu ni wa kuchaguliwa..Sio kila mtu tu anaweza kuupokea..Ni lazima uchaguliwe na kisha uitwe/uvutwe kwa Bwana ndipo umfuate..ikiwa na maana kuwa kama mtu hajasikia mvuto wowote au msukumo wowote ndani yake wa kwenda kumfuata au kumpokea Bwana Yesu huyo hawezi kamwe kumwamini ni sawa na kumlazimisha mtoto mdogo aliyezaliwa leo azungumze haitawezekana.
Kwahiyo kama Bwana amekusudia idadi fulani ya watu wamfuate yeye mwaka huu katika mji fulani labda wa Dar es salaam, hakuna yoyote atakayeweza kupunguza au kuongeza idadi hiyo..wala hakuna mtu yoyote atakayeweza kuisimamisha kazi yake.
Atanyanyua watu wake (watumishi wake) wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee labda tuchukue mfano watumishi 5,000 kwa mji wa Dar es salaam..atawatuma wakaihubiri injili katika huo mji na endapo hao aliowatuma walipaswa wavune idadi ya wale watu milioni 20 wale waliokusudiwa uzima wa milele, na ile idadi ikatimia basi kazi yao itakuwa imeisha watapelekwa mji mwingine..Lakini mfano endapo kati ya wale 5,000 waliotumwa 2,000 wakawa wavivu wasilete mazao..basi Bwana atawanyang’anya ile kazi na kuwapa watu wengine lakini mwisho wa siku ile idadi ya watu milioni 20 waliokusudiwa kuokolewa itatimia tu!..kwa vyovyote vile itatimia tu! Wataondolewa wale wavivu watapewa wale wachapa kazi.
Kwahiyo ndugu huu sio wakati wa kufikiri kazi ya Mungu itasimama endapo sisi (mimi na wewe) leo hii tukikataa kuitenda kazi..Hiyo haitakuwa hasara kwa Mungu bali itakuwa ni hasara kwetu.. kwasababu Nafasi zetu watapewa wengine walio na bidii kuliko sisi endapo tukizembea..Na sisi tutakosa thawabu mbele za Mungu siku ile.
Ukikataa leo kuwashuhudia wengine habari njema za wokovu usidhani umeathiri kazi ya Mungu kwa vyovyote vile..Kazi ya Mungu itafanyika tu na watu wale waliokusudiwa kuokolewa wataokolewa..Bwana alipotuambia tuenende ulimwenguni kote tukahubiri injili kwa kila kiumbe sio kwa faida yake yeye..Ni kwa faida yetu sisi, Hatutumi ili tukamsaidie kazi yake hapana! Yeye hasaidiwi..katutuma ili tukapate faida sisi sio yeye..
Wewe usipoihubiri injili mtaani kwako, mjini kwako au nchini kwako. Kazi ya Bwana haitasimama, Mungu atanyanyua mwingine na kumleta hapo mjini kwako, au nchini kwako kuitangaza habari yake na wale waliokusudiwa kuokolewa wataokolewa tu!..lakini utakuwa umejizuiliwa thawabu yako mwenyewe..
Wewe ukikataa kuichangia kazi ya Mungu mahali ulipo, usifikiri itasimama kwa vyovyote vile.. Hapana Mungu hasaidiwi kazi wala hategemei mfuko wa mtu hata kidogo..atanyanyua wengine kutoka mahali pengine watakaoipalilia ile kazi…Anapotushauri tumtolee yeye sio kwa faida yake yeye bali ni kwa faida yetu sisi..Yeye tayari ana kila kitu..sasa ana haja na nini tena? Dunia yote ni yake sasa ni nini tutamwongezea yeye??
Anapokuambia umtafute yeye, au umtegemee yeye..sio kwamba yeye ana uhaba wa watu au wa sifa, au anahitaji sana utukufu..hapana ndugu anao mabilioni ya malaika watakatifu huko mbinguni wanaomsifu usiku na mchana…anakuambia umsifu wewe kwa faida yako?? Sio kwa faida yake..
Ni sawa na mtu mwenye kampuni kubwa tajiri lililoendelea sana na lenye wafanyakazi wengi wanaojitosheleza, na akamwona mtu maskini na kwa huruma zake akaona ampatie nafasi ya kazi kwenye lile kampuni, sasa sio kwamba kampa ajira kwa sababu anaupungufu wa faida kwenye kampuni lake hapana bali kampa ajira kwasababu amemuhurumia yule maskini na anataka na yeye apate kitu..lakini endapo yule maskini akikataa ile nafasi basi hasara haitakuwa kwa yule mwajiri bali kwake yeye kwasababu yeye tayari anao wafanyakazi wengi wanaojitosheleza….Na kwetu sisi katika kumtumikia Baba yetu wa mbinguni ndio ivyo hivyo.
Ndio maana mahali fulani Bwana Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu aliwaambia mafarisayo maneno yale..
“ 39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, MAWE YATAPIGA KELELE”.
Umeona! Hapo…Bwana alikuwa anataka kuwaonyesha kuwa sio kwamba Mungu ni maskini wa sifa..kwamba pasipo wao kumsifu yeye basi ndio hana sifa mahali pengine..hapana hata mawe yatapiga kelele endapo wao wakinyamaza.
Kama Mtume Paulo alivyosema pia kwa uwezo wa Roho…2 Timotheo 2: 13 “Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe”.
Kwahiyo tukiyafahamu hayo ni wakati wa kumtumikia Mungu kwa Nguvu zote..kwa talanta tulizopewa..tukijua kuwa ni kwa faida yetu, kwasababu siku ile inakuja katika Mbingu mpya na nchi mpya..ambapo Bwana hatakuwa na upendeleo kule..Kila mtu atakuwa na nafasi yake kule, kulingana na talanta alizozifanyia kazi hapa duniani.. Katika mbingu mpya na nchi mpya watakuwepo wafalme, na watu wakawaida, nafasi mtu atakayokuwa nayo kule ndio itakuwa yake hiyo milele..Kwahiyo tujitahidi tupige mbio tukiyatazamia mambo yale yanayokuja kama vile Mtume Paulo alivyokuwa anayatazamia..
Ufunuo 22: 10 “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.
11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.
12 TAZAMA, NAJA UPESI, NA UJIRA WANGU U PAMOJA NAMI, KUMLIPA KILA MTU KAMA KAZI YAKE ILIVYO.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho. 14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”.
Tukaze mwendo, tumtumikie Bwana katika nafasi alizotuweka, naye atatuhifadhi kwa reema zake.
Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.
Mada Nyinginezo:
WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.
About the author