Kwanini maandiko yanajichanganya yenyewe kwenye habari ya Paulo alipotokewa na Yesu alipokuwa anakwenda Dameski?

Kwanini maandiko yanajichanganya yenyewe kwenye habari ya Paulo alipotokewa na Yesu alipokuwa anakwenda Dameski?

SWALI: Shalom mtumishi wa Mungu; Naomba unisaidie kuelewa haya maandiko katika (matendo 9:3-7, 22:6-9, 26:12-14). Pale Mtume Paulo alipokuwa anatoka Yerusalemu kwenda Dameski kushika wakristo na kukutana na YESU njiani. Kama yanazungumzia habari moja mbona kama yanajichanganya yenyewe?.

JIBU: Mtafaruku mkubwa kwenye vifungu hivyo vitatu ni pale ile sauti ilipotoka mbinguni ikisema na Paulo. Watu wanajiuliza inakuaje sasa sehemu moja biblia inasema wale watu waliisikia sauti ya Yesu iliyosema na Paulo , na sehemu nyingine biblia inasema hawakuisikia?, Ni kwanini iwe hivyo?Kwamfano Tukisoma 

Matendo 9:7 inatuambia…. “Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, WAKIISIKIA SAUTI, WASIONE MTU.”

Lakini tukirudi tena kusoma kwenye kitabu hicho hicho cha Matendo ile sura ya 22:9 Paulo anasema…

Na wale waliokuwa pamoja nami WALIIONA ILE NURU, LAKINI HAWAKUISIKIA ILE SAUTI YA YULE ALIYESEMA NAMI”. 

Unaona hapo kunaonekana kama kuna mkanganyiko fulani, inaonyesha kama maandiko yanajipinga hivi, huku yanasema wale watu waliisikia sauti, wakati huo huo tena mbeleni kidogo inasema wale watu hawakusikia ile sauti iliyosema naye. Ni kweli kabisa tukisoma kwa juu juu tu tunaweza kuona maandiko yanajipinga lakini kiuhalisia maandiko hayajichanganyi, badala yake ni sisi ndio tunakosa shabaha ya kuyaelewa..uelewa wetu ndio unaojichanganya. Na ndio maana Mtume Paulo kwa kuyaona mambo kama hayo alikuwa akimsisitiza Timotheo mara kwa mara, akimwambia afanye bidii katika KUSOMA (1Timotheo 4:13)..

Sasa Kusoma kunakozungumiziwa hapo sio kusoma kama mtu asomavyo gazeti, halafu basi, hapana bali ni kusoma kwa KUJIFUNZA..yaani Kwa kuchukua muda kutafakari na kuchambua kwa undani maandiko huku ukimwomba Roho Mtakatifu akuongoze kuyaelewa vinginevyo biblia inaweza kubakia kwako kuwa kama kitabu kisichoeleweka daima, na kinachojipinga siku zote. Sasa tukirudi darasani. Katika maandiko kumbuka Neno KUSIKIA linamaana kubwa zaidi ya “kusikia” tu peke yake..Kwa mfano Utaona Yesu alipofundisha mifano yake mingi alimalizia na kauli hii “mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

Unaona hapo Hakumaanisha kuwa watu waliokuwa mahali pale walikuwa viziwi hawasikii alichokuwa anakizungumza, hapana bali alimaanisha “mwenye masikio ya kuelewa na akielewe kile alichokuwa anakimaanisha.”..

Hali kadhalika Mungu anaweza kuzungumza na mtu maneno yanayoeleweka kabisa na kumshushia ujumbe, lakini kwa mtu mwingine ujumbe ule ukamwasilia kama sauti tu ya ajabu, au ngurumo tu, au mlio wa ajabu usioeleweka,..tunalithibitisha hilo kwa Yesu siku ile aliponyanyua kichwa chake juu na kumwomba baba ndipo sauti ilipotoka juu na kusema naye.…,

Yohana 12: 28 “Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.

29 Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye.

30 Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu

Unaona? Wale watu waliisikia sauti kabisa, na wengine wakatambua ya kuwa ni Mungu ndiye aliyekuwa anasema naye, lakini Hawakuielewa …ilikuja kwao kama kitu kingine kama ngurumo tu, sauti isiyoeleweka.. “” kwahiyo waliisikia sauti lakini ni sawa na hawajaisikia maana hawajaielewa. 

Na ndicho kilichowakuta kundi la watu hawa, walipokuwa wanatoka Yerusalemu kuelekea Dameski, wakiongozwa na kiongozi wao mkuu Sauli (Paulo), waliokwenda kuwakamata Wayahudi wote waliokuwa wakimtangaza Kristo hadharani ili kuwarudisha Yerusalemu waadhibiwe….Ndio katikati ya safari yao walipokutwa na tukio hilo la ajabu, njia mida ya adhuhuri ile nuru kuu kutoka mbinguni ikawaangazia wote, ndipo Yesu akaanza kuzungumza na Sauli kwa lugha ya Kiebrania. Sasa hapo wale watu waliokuwa na Sauli muda ule waliisikia kweli sauti fulani iliyotoka mbinguni, lakini kwao ilikuja kama sauti isiyoeleweka…kama mlio tu au mngurumo!.. 

Na ndio hapo sasa tukirudi kwenye vile vifungu kama kile cha kwanza mwandishi anasema..”

Matendo 9:7 …. “Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, WAKIISIKIA SAUTI, WASIONE MTU.”

Unaona, Hapa ni sawa na kusema walisikia ngurumo tu au sauti isiyoeleweka kutoka mbinguni mahali pale, hakukuwa kimya kabisa kulikuwa na sauti fulani mahali pale,.

Sasa Tukirudi kwenye kile kifungu cha pili inatuambia..Matendo 22.9 …”Na wale waliokuwa pamoja nami WALIIONA ILE NURU, LAKINI HAWAKUISIKIA ILE SAUTI YA YULE ALIYESEMA NAMI”. Hapo ni sawa na kusema Hawakuelewa, kile walichokisia..Hivyo maandiko yapo sawa, na wala hayajipingi na hata sasa biblia inatumbia Luka 8:18 “Jiangalieni basi jinsi msikiavyo;”..

Tunapaswa tuwe makini na kile Mungu anachosema nasi, katika maandiko wakati mwingine tunaweza kujiona tumefika tunaelewa kila kitu, biblia tunaifahamu yote, hakuna hadithi tusioyoijua katika biblia, lakini kumbe hatujaielewa sauti ya Mungu iliyojificha nyumba yake. Bwana Yesu alisema.. 

Mathayo 13:14 “Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, KUSIKIA MTASIKIA, WALA HAMTAELEWA; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.

15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.”

Mungu aturehemu na atujalie kumjua zaidi..

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

SIRI YA KUFANIKIWA KWA MTUME PAULO.

MTUME PAULO ALIKUWA NA MAANA GANI KUSEMA ″…NINAKUFA KILA SIKU?

KWANINI MTUME PAULO HAKUMSAMEHE MARKO, PINDI WALIPOTAKA KWENDA WOTE KAZINI?

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

DALILI NYINGINE INAYOUTAMBULISHA UZAO WA NYOKA

SIKU YA TAABU YA YAKOBO.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments