MTU ANAPOKUFA ANAENDA WAPI?
Ikiwa imetokea umekufa ghafla, muda huo huo utawaona malaika wa Mungu wamesimama pembezoni mwako, ili kukuchukua na kukupeleka mahali panapokustahili, Sasa ikiwa wewe ni mtakatifu (Yaani ulipokuwa hapa duniani uliishi kwa KRISTO, na kujitenga na uovu) basi malaika hao wanakuchukua kwa furaha na kwa shangwe na kwa nyimbo na kukupeleka moja kwa moja sehemu inayotwa Peponi wengine wanaiita Paradiso (Luka 23:43)..
Bwana Yesu alitumia ule mfano wa Lazaro kueleza picha halisi ya kinachomtokea mtakatifu mara baada ya kufa..
Luka 16:22 “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa”.
Kifuani mwa Ibrahimu ndio peponi kwenyewe kwa lugha nyingine, ni mahali pazuri sana, ni sehemu ya mbingu japo sio kule mbinguni kabisa Mungu alipo, ni sehemu ya kitambo tu ambapo watakatifu wanahifadhiwa wakisubiria siku ile ya Unyakuo ifike warudi makaburini kuichukua miili yao, na kwa pamoja sasa waungane na wale watatakatifu ambao watakuwa hai wakati huo, kisha wote kwa pamoja wapewe miili ya utukufu waende kumlaki Bwana Yesu mawinguni, baada ya hapo safari ya mbinguni moja kwa moja inaanza, kwenda kula karamu ya mwana-kondoo kwa Baba mahali ambapo hakuna hata mmoja wetu amefika kwasasa, huko ndipo tutakapomwona Mungu wetu uso kwa uso..tutaona vitu ambavyo hatujawahi kuona, wala kusikia.
Lakini kinyume chake ni nini kinatokea baada ya kifo kwa mwenye dhambi? ikiwa amekufa akiwa mlevi, mzinzi, muuaji, mtukanaji, yaani kwa ufupi yupo nje ya Kristo, basi wale malaika ambao Mungu aliwaandaa kwa kazi ya kuyatenga magugu na ngano (waovu na wema) wanafanya kazi yao hapo,..
Mathayo 13:49 Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki,
50 na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Kumbuka biblia inaposema Mwisho wa dunia inamaanisha mwisho wa aina mbili, aina ya kwanza ni ule mtu anapokufa ndio unakuwa mwisho wake wa dunia, vilevile siku ile ya kiama ambapo dunia yote itahukumiwa nayo pia inaitwa mwisho wa dunia, vyote viwili malaika watafanya kazi hiyo..
Hivyo basi mtu kama ni mwovu, akifa bila kupoteza muda atachukuliwa na malaika hawa na kwenda kutupwa mahali panapoitwa JEHANAMU, huku Jehanamu ni mahali tofauti kabisa na ZIWA LA MOTO, Jehanamu ni kama mahabusu, watu waovu wanahifadhiwa kwa muda tu, wakisubiria hukumu ya mwisho, kisha ndio wakatupwe kwenye lile ziwa la moto siku ile ya mwisho, kama hujafahamu bado Jehanum ni mahali pa namna gani utanitumia ujumbe inbox nikutumie maelezo yake..
Sasa huko ni mahali pa mateso sana, sehemu mbaya, ndio kule Yule tajiri wa Lazaro alipopelekwa
Luka 16.22 “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.
26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
27 Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,
28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.
29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.
30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu
31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu”.
Mtu huyu atakaa huko huko katika mateso hayo muda wote huo akisubiria ufufuo ambao utakuja mara baada ya ule utawala wa miaka 1000 kuisha, ndipo atakaposimama sasa mbele ya kiti cha hukumu cha mwana-kondoo kisha atahukumiwa kutokana na maovu yake yote, na kisha kutupwa katika lile ziwa la moto mahali ambapo pana mateso makali sana ya moto usiozimika…Na Baada ya hapo habari yake itakuwa imeisha.(Ufunuo 20:11-15)
Hivyo usidanganyike kuwa baada ya kifo kutakuwa na nafasi ya pili, hapana biblia imeweka wazi kabisa katika..Waebrania 9:27 “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”;
Ukishakufa leo, shughuli zote za hukumu zinaendelea juu yako, hakuna maisha tena hapo..
Swali linakuja je! Na wewe umejiwekaje tayari ikiwa siku hiyo imekukuta kwa ghafla?, Je! Unao uhakika wa kusikia sauti nzuri za malaika wakikuimbia nyimbo za ushindi wakikunyanyua na kukupeleka kule peponi walipo watakatifu wengine au kuwaona wakija katika hasira kali kukukokota ili kwenda kukutupa Jehanum?. Jibu lipo moyoni mwako,
Na mara nyingine malaika hawa huwa wanawatokea watu hata kabla hawajakata roho vizuri, japo si mara zote, Na ndio maana utaona muda mfupi kabla hawajafa, wengine wakiwa na amani sana, wengine wakitabasamu, wengine wakisema wanaona malaika karibu yao wakizungumza nao, n.k. ukiona hivyo ujue hawa hatma yao ni njema, lakini wapo wengine pia utaona kabla hawajafa muda mchache wanahangaika sana, au wanateseka, wengine wanakufa wakiwa na mwonekano kama vile wamenyongwa, au wameuawa n.k. Ujue kuwa malaika hao wanawachukua kwa hasira na kuwapeleka kule Jehanamu.
Je! Wewe utakuwa upande gani,?Jibu unalo badilika, tengeneza maisha yako kwa Bwana YESU sasa, ikiwa bado unasua sua, kwasababu hiyo kesho unayoisumbukia pengine inaweza isiwe yako. Na baada ya kufa ni hukumu
Ubarikiwe.
Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba
+225693036618/ +225789001312
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA.
About the author