Ujana ni wa thamani..hususani unapotumika vyema…Na kila mahali panaitaji vijana kwaajili ya nguvu kazi, nchi inahitaji vijana kwaajili ya nguvu kazi, shetani naye anawahitaji vijana zaidi kuliko wazee kwa ajili ya nguvu kazi zake…Hali kadhalika Roho Mtakatifu anawahitaji vijana pia.
Na takwimu zinaonyesha kuwa kipindi cha kati ya miaka 13-20 ndio kipindi ambacho watu wengi wanausikia wito wa ki-Mungu, 21-30 mara nyingi ni kipindi cha madarasa ya kiroho na 30-50 ni wakati wa kazi… Sasa ni wachache sana wanapata neema ya kuvutwa kwa Kristo wakiwa na miaka 40 au 50… Utakuwa umepewa neema kubwa sana kama utampokea Kristo katika umri huo Kwasababu ujana pia unathamani mbele za Mungu…
Sasa katika umri wa ujana…Ndio wakati wa kuwa na nguvu nyingi za kiroho..(hiyo ni neema ya kipekee ambayo Mungu anaiachia kwa vijana tu)..haiwahusu wazee.
1Yohana 2:14 “Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna NGUVU, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, NANYI MMEMSHINDA YULE MWOVU”.
Kama vile nguvu kazi ya Taifa ni vijana, vivyo hivyo Taifa la Mungu linajengwa na vijana watakatifu, kwasababu hao ndio wamepewa nguvu!..wazee hawana nguvu hizo..Kwahiyo UJANA ni wa kuuthamini sana.
Mtume Paulo mwishoni mwa huduma yake, alilijua hilo ndipo akatafuta vijana kadha wa kadha kwaajili ya kazi maalumu ya kuujenga ufalme wa Mbinguni…Baadhi yao walikuwa ni Timotheo na Tito. (walikuwepo wengi lakini hebu tuwatazame hawa wawili).
Hawa ni vijana ambao Mtume Paulo aliwaandaa..akawa anawatuma pia…walikuwa ni vijana tu! Labda miaka 20-25 hapo!..Lakini walikuwa wanaifanya kazi kubwa Sana! na kuleta uharibifu mkubwa kwenye ufalme wa giza…Mpaka Paulo ilimbidi kuwaandikia nyaraka zao binafsi, Timotheo alipewa jukumu kubwa sana la kuyasimamia makanisa yaliyopo Asia, na Tito naye hivyo hivyo, Huyu Tito Mtume Paulo alimpa jukumu kwa uwezo wa Roho wa kuteua maaskofu wa kanisa, ambao walikuwa ni wa umri mkubwa kuliko yeye…
Hebu jiulize ni kijana lakini ndiye anayesimamia makanisa yote na ndiye anayepewa jukumu la kuteua wazee na maaskofu wa makanisa…(kasome kitabu cha Tito chote utaona) na Timotheo naye ni hivyo hivyo, alikuwa ni kijana mdogo lakini alipewa majukumu kama hayo kasome 1Timotheo 3, na utaona kwa majukumu hayo Mtume Paulo alikuwa anawaasa pia wakaripie na kukemea na kuwaonya wazee kama wazazi.
Lakini lililo kubwa na muhimu pia Mtume Paulo alilowaasa hawa vijana ni kwamba MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO!..Hebu tusome kidogo
1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi”.
Huyu ni Timotheo, hebu tumwangalie na Tito naye..
Tito 2:15 “Nena maneno hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote”.
Maana yake unapofika wakati wa injili, Hubiri injili usitazame uso wa mtu au kichwa cha mtu kina mvi kiasi gani….Sema kwa ujasiri kwamba WAZINZI WOTE WASIPOTUBU WATAKWENDA MOTONI !!!…usijiangalie wewe ni mdogo na wao ni wakubwa!!..kwamba watakudharau..Kile kitu ambacho Roho Mtakatifu amekiweka ndani yako kizungumze kwasababu ni Mungu ndiye aliyekuambia ufanye hivyo na sio wao!!… Na utaona wote unaowahubiria hata kama wana umri wa Baba yako wanakuja kwa Kristo..Kwasababu Injili ni Uweza wa Mungu uletao wokovu. Hivyo usiudharau ujana wako wala mtu yeyote asikudharau.
Ukidharauliwa na kuambiwa wewe hujui kitu..puuzia hayo maneno!..Lihubiri Neno kwasababu kuna nguvu nyingi za Mungu katika ujana kuliko walizonazo wazee.. Na shetani analijua hilo ndio maana hawapendi vijana na ndio anaowatafuta wengi awaangushe.
Lakini pia Mtume Paulo aliwaonya hawa vijana kwamba wazikimbie TAMAA ZA UJANANI! Katika utumishi wao.
1Timotheo 2:22 “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi”.
Maana yake ni kwamba ujanani kuna vishawishi vingi,na kuna tamaa nyingi…(sio kwamba ukishakuwa mtumishi wa Mungu kijana basi ndio hautakutana na vishawishi/tamaa)…Utakutana navyo lakini biblia imesemaje? TUZIKIMBIEEE…na sio TUZIOMBEEE…Hakuna maombi yeyote ya kuziepuka tamaa wala kuzishinda!…Hakuna maombi yoyote ya kuepukana na uasherati na ulevi na uzinzi!!..HAKUNA! wala usidanganywe na mtu yeyote hata anayejiita mtumishi! …suluhisho ni kuzikimbia…maana yake ni kwamba kama ulikuwa unamahusiano au unaona kuna dalili ya kuzama kwenye uasherati na mtu Fulani, unajiepusha naye! Sio unamwomba Mungu akuepushe naye! Ni wewe ndiye unayeanza kujiepusha naye..unakata mazoea naye.…kadhalika kama ni marafiki ndio waliokuwa wanakushawishi kwenda kuzini kwa mazungumzo yao au tabia zao..unajitenga nao…huko ndiko kuzikimbia tamaa….Yusufu alimkimbia mke wa Potifa hakumwombea!.
Picha za uchi na pornografia unazoziangalia kwenye simu ndizo zilizokuwa zinakupeleka kujichua na kufanya uasherati…hakuna maombi yeyote katika maandiko ya kuiondoa hiyo tabia!…Suluhisho ni wewe kuamua kuachana na hiyo tabia…kufuta hizo picha kwenye simu yako na kama bado inakushinda unajikuta unazifungua, badilisha hiyo simu yako ya smart unayoitumia na anza kutumia simu ya tochi!..Hilo tatizo utakuwa umelitatua moja kwa moja/umelikimbia….Biblia inasema kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate, ili usije ukapoteza roho yako yote..
Usisubiri ujana wako uharibiwe na ibilisi, umri ulionao ni wa thamani, kama hutastuka leo, utafika wakati utajuta sana kwanini hukumtumikia Mungu katika ujana wako. Zinduka usingizini.
Bwana akubariki, kijana!..
Kama hujampa Kristo maisha yako, basi tayari yapo mikononi mwa shetani hata kama utakuwa hujui…Kuwa nje ya Kristo tayari upo kinyume cha Kristo kwasababu hukusanyi pamoja na Kristo, Na hivyo unatapanya..(Mathayo 12:30). Hivyo geuka leo mpe maisha yako, ujana wako unathamani sana katika ufalme wake…Wengi watabadilika kupitia wewe endapo utakubali kumtii Kristo, na siku ile utapewa taji ya Uzima.
Maran atha!.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author