JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

Utauliza je! Shetani ana uwezo wa kuzuia majibu ya maombi?. Jibu ni ndio!.

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa shetani kamwe hana uwezo wa kuzuia maombi kumfikia Mungu..Maombi yeyote yale mtu anayoomba, yanapanda juu kwa Mungu moja kwa moja..Lakini kitu pekee ambacho shetani anachoweza kufanya ni kuzuia majibu ya Maombi..

Tunaona jambo hili kipindi cha Nabii Danieli..

Danieli 10:12 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danielii; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.

  13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi”

Mkuu wa Uajemi, biblia inayomzungumzia hapo, ni Pepo lililowekwa kuwa kuu juu ya ufalme wa Uajemi..Hivyo kazi zote za giza zilizokuwa zinaendelea katika Taifa hilo la uajemi zilikuwa zinaratibishwa na pepo hilo.

Lakini utasoma hapo, Tangu siku ile ya kwanza tu Danieli alipotia moyo wake ufahamu, (yaani maana yake alipoanza kufikiria mambo ya kuomba)..tayari mawazo hayo yalishamfikia Mungu kama maombi..Na tayari majibu yalishatolewa..lakini Malaika yule alipokuwa anarudisha majibu kwa Danieli alizuiliwa na pepo hilo la Uajemi.

Sasa hivyo ndio vita vinavyoendelea hata sasa.. Vita vya Malaika wanaotuhudumia dhidi ya majeshi ya mapepo..Na vita hivyo si vingine zaidi ya vile vya hoja!..

Maana yake ni kwamba..Bwana anapoachilia majibu ya wewe kupata jambo fulani..shetani anakimbilia kupeleka hoja za mashitaka dhidi yako.. Anamwambia Bwana huyu mtu hastahili kupokea hicho unachompa kwasababu ana tabia hii, hii na ile…jana tu katoka kuiba, juzi katoka kuzini na wala hajatubu…Na wewe neno lako linasema husikii maombi ya waovu!..iweje umsikie na kumpa huyo kitu hicho?..Na mashitaka mengine mengi, anayapeleka mbele za Mungu kuhusu wewe.. Sasa mashitaka hayo kama ni ya kweli, basi Mungu hana upendeleo, shetani anashinda dhidi yako…Hivyo malaika yule aliyepewa jukumu la kukuletea baraka zako, anakuwa hawezi kukufikishia kile ulichoomba kutokana na kwamba umeonekana hustahili kukipokea kile kitu, kutokana na mashitaka ya shetani..

Ndivyo biblia inavyosema..

1Petro 5: 8  “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa MSHITAKI  WENU IBILISI, kama simba angurumaye, huzungukazunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Hapo inasema “mshitaki wenu” na si “mshindani wenu”..Maana yake kazi yake kubwa ni kutushitaki.. Na pia biblia inazidi kutufundisha jambo hilo hilo katika…

Ufunuo 12:10  “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, YEYE AWASHITAKIYE MBELE ZA MUNGU WETU, MCHANA NA USIKU

Hivyo ni muhimu kufahamu kila kitu KIOVU tunachokifanya ni POINT kubwa kwa shetani, kwa ajili ya kutuzuilia maombi yetu na baraka zetu siku za mbeleni.

Na sio tu mambo mabaya tunayofanya ni POINT kwa shetani, hata mazuri tunayofanya bado shetani hatachoka kutushitaki kupitia hayo hayo mazuri…ndicho kilichomtokea Danieli pamoja na Ayubu Mtumishi wa Mungu..

Ayubu 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. 

7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. 

8 Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.

 9 Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?

  10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.

 11 Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.

 12 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana”.

Unaona na hapo?..Ayubu anatenda mema lakini bado shetani hakuacha kumchochoe Mungu amuangamize..

Ayubu 2: 3 “Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, UJAPOKUWA ULINICHOCHEA JUU YAKE, ILI NIMWANGAMIZE PASIPOKUWA NA SABABU”.

Hapo Bwana alimletea Ayubu mabaya kwa uchochozi wa shetani ijapokuwa Ayubu alikuwa mkamilifu, hebu jiulize kwa mtu ambaye sio mkamilifu, mzinzi, mwasherati, msengenyaji, mtukanaji n.k ni Mashitaka mangapi mabaya yanapelekwa mbele za Mungu na shetani dhidi yake??..

Hivyo ni muhimu kufahamu hilo kwamba shetani anao uwezo wa kuzuia majibu ya maombi yetu kwa njia hiyo.

Hivyo suluhisho pekee ili maombi yetu yasizuiliwe ni KUWA WAKAMILIFU MBELE ZA MUNGU KAMA AYUBU… Ndio ni kweli, Bwana alisikiliza uchochezi wa shetani na kumletea Ayubu yale majaribu, lakini haimaanishi kwamba kila uchochozi shetani anaoupeleka sasa kwa Mungu dhidi yetu, basi Mungu atausikiliza kama alivyousikiliza wa Ayubu, kama tukiwa wakamilifu. La Mwingi anaukataa kwasababu ni wakamilifu mbele zake, na zaidi ya yote anatuletea baraka badala ya mabaya shetani anayotutakia.

Lakini tusipojitahidi kuwa wakamilifu, kwa kuzishika amri zake na kuliishi Neno lake, basi tufahamu kuwa majibu ya maombi yetu yatakuwa ni ndoto, na badala yake tunaweza kupata matatizo badala ya baraka, kwasababu shetani yupo kutushitaki…

NA NI UKAMILIFU UPI AMBAO UTATUSAIDIA KUPATA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

  1. Kwa kuwa watakatifu rohoni na mwilini (Waebrania 12:14). Na utakatifu inajumuisha Upendo, uvumilivu, utu wema, kiasi n.k (Wagalatia 5:22)

     2. Kwa kuwa waombaji (Yohana 14:13, 1 Wathesalonike 5:17, Luka 22:40).

  1. Kwa kulisoma Neno na kuliishi (Wakolosai 3:16, Yohana 5:17, Warumi 10:17).

Na mengine yanayohusiana na mambo hayo… Tukiyafanya hayo, basi tunao uhakika wa maombi ya majibu yetu kutufikia, bila kuzuiwa na mamlaka ya giza. Na pia kama tuna uhakika kwamba tunayafanya hayo, basi tuombe kwa ujasiri na Imani, pasipo mashaka…

Na pia kumbuka sio kila jibu la ombi linalokawia ni limezuiliwa na shetani.. Hapana!..Mengine hayajazuiliwa isipokuwa wakati wake wa majibu bado haujafika…Ukifika wakati jibu litakufikia tu!. Ni sawa na mwanafunzi anayemwomba Mungu awe daktari, hawezi kupata jibu la ombi hilo siku ile anayoomba, kashasikiwa maombi yake lakini hana budi kupitia madarasa fulani ambayo yatamjenga ili wakati utakapofika wa kupokea jibu la ombi lake, awe kashaandaliwa kielimu vya kutosha, ndio hapo inaweza kumchukia hata miaka 15 mbeleni, mpaka hicho alichomwomba Mungu kitimie (sasa huo ni mfano tu!).. Na maombi mengine ni hivyo hivyo, unaweza kumwomba Mungu leo, usikipate hicho kitu leo leo..kikaya kutokea baadaye sana, baada ya Mungu kukuaandaa vya kutosha. Hivyo ni muhimu kulijua pia hilo.

Bwana atubariki na kutusaidia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

FAIDA ZA MAOMBI.

FAIDA ZA MAOMBI YA USIKU

Je! kuna maombi yoyote ya kumtoa mtu aliyekufa kwenye mateso ya kuzimu?

MUNGU HANA MBARAKA MMOJA TU!..MWAMINI.

TUMEPEWA, SI KUMWAMINI TU KRISTO, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Godfrey Kenjewala
Godfrey Kenjewala
2 years ago

Nimefurahi sana kuifikia kurasa yenu nabarikiwa sana sana

Richard
Richard
2 years ago

Nabarikiwa sana na jumbe na mafundisho yananijenga sana