SOMO no.02 (BINTI WA YEFTHA).

SOMO no.02 (BINTI WA YEFTHA).

Karibu katika mwendelezo wa masomo yawahusuyo wanawake wa kwenye biblia,  Leo tutamtazama mwanamke mmoja/binti mmoja aliyekuwa mtoto wa pekee wa Mwamuzi wa Israeli.

Binti huyu alikuwa alikuwa ni mtoto wa pekee wa mtu aliyeitwa Yeftha, ambaye alikuwa ni Mwamuzi wa taifa la Israeli. Nafasi ya mwamuzi katika Israeli nyakati hizo, ilikuwa inakaribia sana kufanana na ile ya Mfalme, ingawa sio ya kifalme.  Hivyo mtu aliyekuwa mwamuzi katika Israeli katika nyakati hizo, alikuwa ni Mkuu sana, na mwenye kujilikana na kuheshimiwa katika nchi nzima.

Lakini tunasoma katika biblia alitokea Mwamuzi mmoja aliyeitwa Yeftha, ambaye huyu alikuwa ni shujaa sana..Na hakuwa na mwana wa kiume katika nyumba yake bali wa kike tu, tena mmoja. Lakini tunasoma wakati Fulani alipokwenda vitani, alimwekea Bwana nadhiri kubwa, kutokana na ukubwa wa vita iliyoko mbele yake, alitazama mbele yake akaona hiyo vita anayotaka kwenda kukumbana nayo, sio ndogo!, na endapo ikitokea kashinda basi ni muujiza wa Mungu tu umefanyika, na si kingine, kwasababu katika hali ya kawaida ni ngumu kushinda…kwasababu wanaokwenda kupigana nao ni wengi kuliko wao na wenye nguvu kuliko wao.

Kwahiyo ili kujihakikishia ushindi zaidi, alimwekea Mungu nadhiri, kwamba endapo Mungu atampa ushindi, basi kile cha kwanza, kitakachotoka kumlaki wakati anarudi vitani atakitoa kiwe sadaka ya kuteketezwa mbele za Bwana. Na katika mawazo  yake pengine alilenga mtumwa wake mmoja, au ndugu mmoja aliye katika nyumba yake, ndiye atakayekuja kumlaki (kwani nyumba yake ilikuwa na watu wengi, kwasababu yeye alikuwa ni Mkuu katika Israeli). Lakini cha kushtusha ni kwamba alitokea Binti yake wapekee kuja kumlaki, kinyume na matarajio yake. Na alipomwona akahuzunika sana, lakini akawa hana cha kufanya…(Hawezi kuitangua nadhiri yake)

Hebu tusome kidogo habari yenyewe kisha tusonge mbele..

Waamuzi 11:28 “Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea.

 29 Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.

30 NAYE YEFTHA AKAMWEKEA BWANA NADHIRI, AKASEMA, KWAMBA WEWE UTAWATIA WANA WA AMONI MKONONI MWANGU KWELI,

31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.

 32 Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake.

33 Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.

34 Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye.

35 Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia Bwana kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma.

36 BINTI YAKE AKAMWAMBIA, BABA YANGU, WEWE UMEMFUNULIA BWANA KINYWA CHAKO; BASI UNIFANYIE SAWASAWA NA HAYO YALIYOTOKA KINYWANI MWAKO; KWA KUWA YEYE BWANA AMEKULIPIA KISASI JUU YA ADUI ZAKO, HAO WANA WA AMONI.

  37 Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu.

  38 Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani.

 39 Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume. Kisha ikawa desturi katika Israeli,

 40 kwamba binti za Israeli waende mwaka baada ya mwaka ili kumkumbuka huyo mwana wa Yeftha, Mgileadi, siku nne katika mwaka”

Leo nimetamani tujifunze kuhusu huyu binti, Kwasababu alikuwa ana roho ya Ushujaa ndani yake!..

Dada/Mama/ binti siku zote kumbuka hili: ni vizuri kwanza kujifunza kwa wanawake waliopo katika biblia kabla ya kuwatafuta wanaume.

Wanawake wengi wanapenda sana kujifunza kwa Isaka!.. Jinsi alivyonusurika kifo!, cha kuchinjwa na kutolewa sadaka ya kuteketezwa, lakini hawajui kuwa Isaka alinusurika tu!!, hakuchinjwa, wala hakutolewa sadaka… Yupo Shujaa mmoja katika biblia ambaye Alikubali mwenyewe kuchinjwa na nyama yake kukatwa katwa vipande na kisha kutolewa kama sadaka ya kuteketezwa!.. Ambaye pengine tutakapofika mbinguni tutamkuta ni mkuu kuliko ISAKA!..Na tutajilaumu sana kwanini hatukujifunza kutoka kwake!

Na huyo si mwingine zaidi ya huyu binti wa Yeftha!!. Binti huyu baba yake alimwambia dhahiri kabisa kwamba atakwenda kutolewa sadaka ya kuteketezwa!.. Jambo ambalo kiuhalisia ni gumu sana mtu kukubaliana nalo, lakini Binti huyu baada ya kupewa hizo taarifa!, wala hazikumwazisha.. wala hakuogopa kufa!, wala hakuogopa makali ya visu katika mwili wake, wala moto.. badala yake alisema maneno haya..

“36 BINTI YAKE AKAMWAMBIA, BABA YANGU, WEWE UMEMFUNULIA BWANA KINYWA CHAKO; BASI UNIFANYIE SAWASAWA NA HAYO YALIYOTOKA KINYWANI MWAKO; KWA KUWA YEYE BWANA AMEKULIPIA KISASI JUU YA ADUI ZAKO, HAO WANA WA AMONI”.

Bila shaka maneno kama haya, Isaka mwana wa Ibrahimu asingeweza kusema, pale alipokuwa anapelekwa mlimani kuchinjwa! Na Baba yake. Si ajabu, Ibrahimu hakumwambia Isaka chochote, kwamba anakwenda kumchinja na kumtoa sadaka!..pengine ingekuwa kitimtimu pale!, pangekuwa hapatoshi!, pangetokea vurugu kubwa sana!…Ndio maana Ibrahimu alimficha, kwasababu alimwona pengine hana huo utayari wa kujitoa kufa!!.

Mwanzo 22: 6 “Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja.

 7 Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa?

 8 Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja”.

Huyo ni Isaka anaulizia sadaka ya kuteketezwa ipo wapi!, maana yake yeye haimwingii akilini kujiweka katika hilo kundi!, kwamba yeye anaweza kuwa hiyo sadaka!.. Lakini alikuja kutokea Shujaa mmoja!, binti mdogo, ambaye taarifa za msiba si kitu kwake!, ambaye visu shingoni si kitu kwake, ambaye moto juu ya mwili wake si kitu kwake.. Zaidi ya yote alikuwa mtoto, tena ni binti, na tena ni BIKIRA!.. Lakini alikuwa na Imani kubwa kuliko ya Isaka!!. Huyu taarifa za kuchinjwa zilipomjia hakupepesuka wala hazikumshutua, alianza kuufikiria mambo mengine kabisa (Ubikira wake!!..na kwenda kuomboleza kwaajili ya huo, na alipomaliza kwa miezi miwili), kama vile kondoo apelekwavyo machinjoni, alikwenda mwenyewe na akachinjwa na kufa na kuteketezwa..

Labda inawezekana hujui vizuri!, sadaka ya kuteketezwa inakuwaje.

Sadaka ya kuteketezwa ambayo Mungu alimjaribu nayo Ibrahimu amtoe mwanawe , ilikuwa ni kwamba.. mtoto Yule anakamatwa, anafungwa kamba na kisha kisu kinapitishwa shingoni, anachinjwa kama ng’ombe, damu inachuruzika, na baada ya kuchinjwa, mwili wake unakatwa vipanda vipande, kisha vile vipande vinawekwa juu ya kuni, zilizopo juu ya mawe, na moto unawashwa na ile nyama inateketea kabisa mpaka inakuwa jivu!.. Hiyo ndiyo sadaka aliyokusudiwa Isaka!, ambayo Mungu alimwepusha nayo haikumpata, lakini ikatimia kwa shujaa huyu mmoja Binti wa Yeftha!, yeye alikubali mwenyewe kwenda kuchinjwa!.

Waebrania 11:35  “Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora”

Isaka aliibeba picha ya Yesu tu!, lakini huyu binti alilibeba tukio zima la Yesu!.. alionja kile Bwana alichokipitia pale Kalvari.. Na baada yake hatuoni mtu mwingine, awe mwanaume au mwanamke aliyefanya jambo la kishujaa kama hilo!, wengine wote kwenye biblia waliingia kwenye dhiki bila idhini zao, walishikwa wakakatwa vichwa na kuchinjwa, lakini si kujipeleka wenyewe kuchinjwa!…

Jambo hilo tunaliona kwa watu wawili tu! Kwenye biblia nzima, wa kwanza ni MKUU WA UZIMA MWENYEWE, MWAMBA-YESU KRISTO..Na mwingine ni huyu “Binti wa Yeftha”.

Dada/Binti /mama umeona ni jinsi gani una mashindano makubwa mbele yako??… Siku ile utajitetea vipi, kwamba umeshindwa kujitoa kwake!, na kumtumikia  kwasababu tu wewe si mwanaume??..Leo hii unaogopwa kuchekwa!, wenzako walikufa kabisa!..jambo ambalo hata mwanaume hawakuweza kulifanya!.. Bado huoni tu! Siku ya hukumu binti wa Yeftha atasimama kuhukumu mabinti wengi??..Bado huoni tu hilo!..fahamu kuwa!..hukumu ya wanawake itakuwa ni kali kuliko ya wanaume.. kwasababu katika biblia wapo wanawake waliofanya makubwa kuliko wanaume.  Eliya alimkimbia Yezebeli, ili ayanusuru maisha yake, lakini huyu binti wa Yeftha, yeye anakifuata kifo mwenyewe!..jiulize kati ya hao wawili ni yupi mwenye imani kubwa!..Wanawake kama hawa pamoja na mfano wa Yule Malkia wa Sheba Bwana Yesu aliyemtaja, watasimama kuhukumu vizazi vyetu..

Mathayo 12:42 “Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani”.

Hivyo, wewe kama Mwanamke, simama itambue nafasi yako!.. kama Dada simama!, kama binti simama!.. usiogope kufa!, badala yake uwe tayari kufa hata kwaajili ya imani, usiogope kupitia dhiki,badala yake uwe tayari kukumbana nazo kwaajili ya imani yako, usiogopwe kuonwa mshamba unapoacha mambo yote ya kidunia, na fashion zote!..Badala yake uwe tayari kuonekana umerukwa na Akili, Fahamu kuwa thawabu yako ni kubwa mbinguni.. Kuanzia leo anza kupiga mbio, ukijifunza kwa wanawake mashujaa katika biblia..

Vile vile usiutamanie  udunia, ukasema ngoja uule ujana, ndio utamtumikia Mungu, siku ile huyu binti wa Yeftha atasimama kukuhukumu, kwasababu yeye alikufa katika ubikira wake bila mume, angeweza kumwambia baba yake amruhusu akaolewe kwanza miezi miwili ndipo, amtoe sadaka!..lakini hakufanya hivyo, aliuthamini ubikira wake, akafa hivyo hivyo..

Vile vile hakuwa mtoto wa maskini, labda tuseme amechoka maisha ndio maana kakubali kujitoa afe!.. hapana!, alikuwa ni mtoto wa Mwamuzi wa Israeli..Ni tajiri sana!, kwasababu waamuzi walikuwa ni kama wafalme, lakini hakuutumainia utajiri wake, wala ubikira wake, wala uzuri wake.. Alikubali kuondoka!, kwasababu alijua, anao mji unao mngojea huko mbele. Yeru salem mpya. Alijua ufufuo unakuja na atakuwa mkuu katika ufalme wa mbinguni.

Kumbuka Mungu aliwachagua tu wanaume kwenye biblia wawe kama mwonekano tu!.. ndio maana utaona kila mahali wanatajwa wanaume..kama Isaka, Yakobo, Eliya n.k Lakini hiyo haimaanishi kuwa wao ndio wa kwanza katika ufalme wa Mbinguni.. Kwaufupi ni kwamba Mbinguni watakuwepo wanawake watakaopata thawabu kubwa hata kuliko hata wakina Ibrahimu, Isaka na akina Eliya na Musa. Kwasababu Mungu siku zote hana upendeleo.

Hivyo unaposoma biblia, anza kutafuta matendo ya wanawake mashujaa, ujifunze kwao, na vile vile, jifunze kwa wale waliojiharibia njia zao pia, ili uchukue tahadhari.

Mwisho wa muhtasari huu kumhusu “binti wa Yeftha” shujaa wa Bwana. Usikose mwendelezo wa wanawake wanaofuta!.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Sadaka ya kuinuliwa ni sadaka ya namna gani?

FUNGUO WALIZOKUWA NAZO MABINTI WATANO WA SELOFEHADI!

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

Maana Ya Maneno Katika Biblia.

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments