IEPUKE GHADHABU YA MUNGU.

IEPUKE GHADHABU YA MUNGU.

Tofauti na inavyoaminika na wengi kuwa hasira ya Mungu au ghadhabu ya Mungu, inakuja au inachochewa sana na watu waliomwacha Mungu, wa ulimwengu huu, yaani watu ambao hawajamwamini Mwokozi Yesu.

Hiyo ni kweli kabisa, lakini nataka nikuambia kuwa hiyo haichangii pakubwa kuimwaga ghadhabu ya Mungu ulimwenguni.

Jambo kubwa linaloleta ghadhabu ya Mungu ulimwenguni ni maovu katikati ya watu wa Mungu, pamoja na ndani ya nyumba ya Mungu. Kikawaida mtu asiyekujua akikutusi, au akikudhalilisha jambo lile haliwezi kuugusa moyo wako sana, kama ukitukanwa au kudhalilishwa na mtu unayemjua, au uliye na mahusiano naye ya karibu sana.

Yule uliye na mahusiano naye ya karibu ndiye anayeweza kukuudhi sana na kukufurahisha sana, tofauti na mtu mwingine ambaye hamna mahusiano yoyote au hata hamjuani.

Ndivyo hivyo hivyo na Mungu wetu, watu wanaompendeza sana ni watu wale alio na mahusiani nao maana yake watu waliookoka, na wala si watu wa ulimwengu huu ambao hawamjui Mungu.. kadhalika watu wanaomuudhi sana, ni watu waliookoka ambao hawajasimama sawasawa. Hao ndio wanaomhuzunisha sana na wanaougusa moyo wake kwa maovu yao zaidi ya watu wale ambao hawajaokoka kabisa na wanatenda mabaya.

Maana yake ni kwamba mtu anayesema ameokoka na huku ni mzinzi, au mtukanaji, au muuaji.. Huyo anamhuzunisha Mungu na kumuudhi mara nyingi zaidi ya Yule ambaye hamjui Mungu kabisa na ambaye hajaokoka. Mtu ambaye hajaokoka kabisa na yupo katika ulimwengu, na anafanya maasi, ni kweli anamhuzunisha Mungu lakini si kwa kiwango kile cha mtu aliye katika mahusiano na Mungu, na wakati huo huo anafanya maasi.

Ni muhimu sana kulijua hili ili tuweze kuchukua tahadhari, na kuacha kunyoosha vidole kwa watu waovu wasiomjua Mungu, ilihali sisi wenyewe tuliomjua Mungu hatujajiweka sawa ipasavyo.

Wewe uliyeokoka utasema unazini mara moja tu kwa mwezi au kwa mwaka, na kufikiri moyoni mwako kuwa una heri sana kuliko Yule kahaba unayeona anajiuza kila siku ambaye hamtaki Mungu na hajaokoka kabisa.

Nataka nikuambie wewe uliyeokoka unayezini mara moja kwa mwezi au mara moja kwa mwaka ndiye mwenye dhambi kubwa kuliko Yule kahaba anayezini kila siku ambaye hajaokoka!.. Wewe ndiye unayemhuzunisha Mungu sana kuliko Yule kahaba..

Wewe unayesema umeokoka na kulewa mara moja kwa mwezi, ndiye unayeichochea ghadhabu ya Mungu kuja ulimwenguni zaidi hata ya Yule mlevi, anayeshinda bar kila siku na huku hajaokoka kabisa.

Wewe unayejiita umeokoka na huku unatazama picha za utupu mitandaoni na unajichua, mara moja kwa mwezi ndiye unayefanya dhambi kubwa kuliko Yule ambaye hajamjui Mungu kabisa na anafanya mambo hayo kila siku.

Sasa hivi utatazama mataifa mengine, watu wanatembea uchi barabarani, watu wanamtukana Mungu.. na moyoni ukadhani una heri wewe ambaye humtukani Mungu lakini unatukana mara moja moja.. Nataka nikuambie ndugu, hao wamemkataa Mungu tangu zamani, na Mungu alishawaacha sawasawa na (wafuate tamaa zao), hivyo wanayo hukumu yao inayokuja kama hawatatubu..Lakini wewe unayejua kila kitu, ambaye umeshaanza mahusiano na Mungu, na unafanya mambo kama hayo, hata kama ni siku moja moja.. jua kuwa wewe ndiye unayeichochoa hasira ya Mungu.

Hivyo ndugu kumbuka siku zote, Maasi katikati ya  watu wa Mungu ndio yanayoleta ghadhabu ya Mungu zaidi ya wale walio nje ya Imani.

Hivyo ni wajibu wetu, kujitakasa zaidi, nyakati hizi za siku za mwisho.. wala tusijilinganishe na watu walio nje!.. na kufikiri kuwa makosa yao Mungu anayafananisha na yetu. Ni wakati wa kuukataa uvuguvugu wote na kutafuta kuwa moto katika Imani.

Ufunuo 3:14 “Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu”.

Bwana akubariki.

Kumbuka pia ule mwisho umekaribia sana, na parapanda ya mwisho ipo karibuni kulia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

“Shinikizo” ni nini kibiblia, Na maana yake rohoni ni ipi?

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments