NINI MAANA YA KUTUBU

NINI MAANA YA KUTUBU

Tofauti na inavyodhaniwa na wengi kuwa kutubu ni kuomba msamaha, lakini kiuhalisia kuomba msamaha kunakuja baada ya kutubu.

Kutubu maana yake ni “Kugeuka” yaani kuacha kile ulichokuwa unakifanya.
Maana yake unapojigundua kuwa wewe ni mkosaji, jambo la kwanza ni “Kuacha kile ulichokuwa unakifanya” kisichokuwa sawa. Kisha ndipo unakwenda kuomba msamaha.

Hakuna mtu anayekwenda kuomba msamahaka kabla hajaacha kile alichokuwa anakifanya.

Umemwibia mtu, au boss wako, je unaweza kwenda kumwomba msamaha huku bado unamwibia?

Jibu ni la!. Cha kwanza utakachokifanya ni kuacha kwanza wizi, kisha ndipo unakwenda kumwomba Msamaha. Maana yake matendo yako ndiyo yatakayoelezea kama kwenye kama umetubu kweli au la!, Na si maneno.

Na kwa Mungu ni hivyo hivyo, haangalii wingi wa maneno yetu, wala wingi wa machozi yetu, wala wingi wa majuto yetu, bali wingi wa Matendo yetu!.

Kwa Mungu “Matendo” ni Alama kubwa sana kuliko hata “Maombi”. Mtu anayetenda sana ni rahisi kufanikiwa zaidi na yule anayeomba sana bila kutenda.

Yakobo 2:17 “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake”.

Kadhalika na Toba ni matendo si maneno.
Ili tulielewe hili vizuri hebu tujikumbushe ile habari ya Yona.

Yona 3:3 “Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu.

4 Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.

5 Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.

6 Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.

7 Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;

8 bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake.

9 Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?

10 Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende”

Nataka tuuone huo mstari wa 10 unaosema “Bwana akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya”…hapo haisemi “Bwana akaona kufunga kwao na kujitesa kwao, wala kulia kwao”.

Sasa sio kwamba kufunga Mungu hakuoni, anakuona lakini kunapaswa kuje baada ya mtu kuacha njia zake mbaya.

Tunapokwenda kuumaliza mwaka tulikumbuke hili, inawezekana umeomba sana Msamaha kwa Mungu kwa mambo unayoyafanya, lakini nataka nikuambie kuwa ni muda tu ulikuwa unapoteza, hakuna msamaha wowote ulioupata endapo hukuamua mwenyewe kuacha njia zako mbaya, kama hawa watu wa Ninawi.

Kama hukuamua kuacha njia ya Ulevi,uzinzi, anasa, wizi, utukanaji, uuaji, utapeli, rushwa n.k bado toba yako haikukamilika, haijalishi uliongozwa sala ya Toba na nani?, Bado mbele za Mungu hujapokea msamaha wa dhambi.
Sasa swali ni wakati gani sahihi wa kutubu?
Biblia inasema saa ya Wokovu ni sasa, wakati uliokubalika ndio huu.

2 Wakorintho 6:2 “(Kwa maana asema,
Wakati uliokubalika nalikusikia,
Siku ya wokovu nalikusaidia;
tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)”

Je Umetubu??..Yaani umegeuka na kuacha njia zako mbaya?. Kumbuka baada ya wewe kuamua kuacha njia zako mbaya ndipo Bwana kupitia Roho wake Mtakatifgu anakuongezea nguvu ya wewe kuweza kushinda dhambi, kwasababu Roho Mtakatifu ni msaidizi, maandiko yanasema hivyo, (kumbuka tena, Yeye ni msaidizi na si mtendaji). Watendaji ni sisi, yeye kazi yake ni kutusaidia, kutuongezea nguvu.

Sasa jiulize atamsaidiaje mtu ambaye hajaanza kufanya chochote??, Utamsaidiaje mtu aliyechoka kutembea na ilihali hata hiyo safari yenyewe hajaianza?.

Isaya 40:29 “[Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo”.

Leo kuna watu wengi wanaoshindwa na dhambi, ambao hawawezi kuacha ulevi, uzinzi, kujichua, kuiba, kusengenya n.k. Na hawajui tatizo ni nini?.

Tatizo ndio hilo, walitangulia kuomba msamaha kabla ya kuamua kuacha matendo yao.

Bwana alipofika nyumbani kwa Zakayo, alitubu wizi wake kwa matendo kwa kwenda kuwarudishia mara 4 (Luka 19:1-10) wale aliowadhulumu, na ndipo Bwana akamwambia leo wokovu umefika nyumbani kwake, hakutubu kwa maneno tu!.

Watu kama Zakayo ndio Bwana anawaongezea nguvu ya kushinda dhuluma, kwasababu wameshaanza safari ya kuacha dhuluma kwa vitendo.
Na wewe leo anza toba kamili kwa kumwacha huyo mke/mume ambaye si wako, kwa kumwacha huyo mtu mnayeishi kama girlfriend/boyfriend na ilihali hamjafunga ndoa, kwa kumrudishia mtu kitu ulichomdhulumu au kumwimbia.

Na baada ya kufanya hayo na kumwomba Bwana msamaha, utaona Amani fulani isiyoelezeka imeiingia ndani yako, hiyo itakuwa ni uthibitisho wa kwamba Toba yako imekubalika mbele za Bwana.

Na baada ya hapo Bwana atakuongezea nguvu ya wewe kushinda dhambi, ghafla utaona kiu ya kudhulumu imekufa, kiu ya kuzini imekufa, kiu ya kufanya mambo yote uliyokuwa unayafanya imekufa.

Bwana akubariki, na Bwana atubariki sote.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

NGUVU YA MSAMAHA

WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.

NATAKA REHEMA, WALA SI SADAKA!

KIFAHAMU KIGEZO  CHA KUSAMEHEWA NA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucy
Lucy
3 months ago

Shalom mtumish