USIYADHARAU MARUDIA YA BWANA.

USIYADHARAU MARUDIA YA BWANA.

Mwana anayependwa na wazazi wake ni lazima apitie vipindi vya kurudiwa! (maana yake vya kuonywa, au wakati mwingine kuadhibiwa pale anapokosa). Na kama sisi wanawadamu tunawarudi watoto wetu pale wanapofanya makosa, kadhalika Mungu naye anawarudi watoto wake pale wanapokosa.

Kumbuka sio watu wote wanaorudiwa na Mungu duniani, wengi wanapigwa tu na Mungu.. na wachache sana wanarudiwa.. Wanaorudiwa ni wana wa Mungu na wanaopigwa ni wana wa ulimwengu huu, waliomkataa Mungu.

Kurudiwa ni kitendo cha kurekebishwa kwa adhabu.. Maana yake unaadhibiwa ili ujirekebishe. Bwana Mungu anapomrudia mwana wake, anakuwa anamwonesha kosa lake, huku anamwadhibu, hivyo anayeadhibiwa anajua adhabu hiyo ni kutokana na kosa fulani.

Lakini anayepigwa na Mungu, mara nyingi anakuwa hajui chochote.. kwasababu uhusiano wake na Mungu upo mbali sana.. kama hata kuipambanua sauti ya Mungu hawezi,  au haamini hata kuna Mungu atawezaje kujua kuwa anayemwadhibu ni Mungu?. Hivyo ataona mabaya tu yanamjia! Na hatajua chanzo, ndio hivyo atababaika kwenda kutafuta suluhisho huku na huko, hadi hata kwa waganga, kutafuta chanzo cha tatizo lake.

Na wewe kama mwana wa Mungu (yaani uliyemwamini Bwana na kutubu na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu), utapitia hivyo vipindi vya kurudiwa na Bwana.

Unapogundua umefanya jambo fulani ambalo sio zuri, na unaona mkono wa Bwana upo juu yako kutokana na hicho ulichokifanya. Basi huo ni wakati kufanya yafuatayo.

1 . JIFUNZE KUTOKANA NA MAKOSA.

Ukigundua hiyo shida au hasara iliyokupata ni kutokana na Uongo uliousema muda mchache nyuma, fahamu kuwa umerudiwa na Bwana, hivyo ni wakati wa kulitambua hilo kosa na kujifunza, ili siku nyingine usilirudie tena.

Ukiona ajali hiyo uliyoipata ni kutokana na Hasira uliyomwonea ndugu yako muda mchache nyuma, hapo umerudiwa, hivyo jifunze kutokana na makosa.

Ukiona furaha au amani imeondoka ndani yako, na hiyo ni baada ya kumkosa ndugu yangu muda mfupi tu nyuma, fahamu kuwa ni Bwana amekurudi

Ukiona magonjwa fulani, au tabu fulani zimekuandama baada tu ya kuacha Maombi uliyokuwa umezoea kuyaomba jua ni Bwana anakurudi. Hivyo rudia upesi ratiba yako ya kuomba.

Ukiona siku hiyo umekosa chakula, au riziki, baada tu ya wewe kumfungia riziki mwingine jua ni Bwana amekurudi, hivyo jirekebishe haraka sana.

Na mambo mengine yote ni hivyo hivyo… Ukiona kuna vishida au vitabu unavipitia baada ya kuokoka, ni mkono wa Bwana huo juu yako, ni kiboko cha Bwana!.. Na lengo la kurudiwa huko si kukudhoofisha wewe bali kukuimarisha.. ili uwe mkamilifu zaidi..

Ufunuo 3:19 “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu”.

  1. USIDHARAU KURUDIWA NA BWANA.

Mfano wa kudharau kurudiwa na Bwana ni pale unapoadhibiwa na unajua kabisa kwamba tatizo hili ni kutokana na kosa lile ulilolifanya, labda kutokana na uwongo uliousema, au kutokana na kiburi ulichokionesha, au kutokana na mawazo mabaya uliyoyawaza n.k, Na baada ya kujua hayo hujifunzi kutokana na makosa hayo, ili wakati mwingine usirudie tena..lakini badala yake unapuuzia!!, unachukulia kiwepesi..hapo umeyadharau marudia ya Bwana kama maandiko yanavyosema..

Waebrania 12:5 “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye;

6 Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye”.

  1. USIZIMIE MOYO.

Jambo la tatu: Usizimie moyo, Usife moyo wala usikate tamaa, unapoona unapitia hizo adhabu ndogo ndogo…usikate tamaa kabisa.. Jirekebishe tu na kisha songa mbele, kwasababu ni adhabu ya funzo tu na si ya kukukomoa wewe..

Tusome tena mstari huo..

Waebrania 12:5 “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, WALA USIZIMIE MOYO UKIKEMEWA NAYE

Adhabu siku zote si kitu kizuri!, lakini hatuna budi kuzistahimili maadamu ni kweli tumekosa, Vile vile hatuna budi kuendelea kumpenda Mungu hata kama anatuadhibu!!, Mwana mwenye hekima hawezi kumchukia baba yake au mama yake anapomwadhibu kwa kosa ambalo kweli kalifanya..Kadhalika na sisi hatuna budi kuendelea kumpenda Bwana, na kumtumikia, kwasababu hayo yote yametupata kwa faida yetu sisi na si yake..

Waebrania 12:6 “Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye.

7 Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?

8 Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.

9 Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi?

10 Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.

11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.

12 Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza,

13 mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe”.

Je wewe ni mwana halali wa Mungu?.. kumbuka tunafanyika wana kwa kumwamini Bwana Yesu tu peke yake..

Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.

Kama hujampokea Bwana Yesu, bado wewe ni mwana haramu, asiyeweza kurudiwa.. Na hakuna faida yoyote ya kuwa Mwana haramu, kwasababu huna urithi..hivyo mpokee leo Bwana Yesu na ukabatizwe uweze kuwa mwana wa Mungu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

MJUE SANA YESU KRISTO.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

ADHABU KALI KUTOKA KWA MUNGU, ITAMPATA MTU WA NAMNA GANI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments