Shalom, karibu tujifunze maandiko.
Kila ishara inayo sauti nyuma yake..Kwa mfano “tunapoona ishara ya mawingu kuwa meusi”..ujumbe au sauti uliopo nyuma ya hiyo ishara ni kwamba “muda si mrefu mvua inashuka”..Sasa sio kwamba mawingu yametoa sauti na kusema “mvua inakuja”..la! mawingu hayawezi kuongea.. lakini yametoa tu ishara, ambayo ndani ya hiyo ishara ipo sauti.
Hali kadhalika pia na kwa upande wa Mungu wetu, Sauti yake pia wakati mwingine ipo katika Ishara.. Mungu anaweza kuzungumza moja kwa moja tukaisikia sauti yake, lakini pia sauti yake anaweza kuiweka ndani ya ishara fulani, kwamba tutakapoona ishara hiyo, basi ni wajibu wetu kutambua sauti gani ipo nyuma ya hiyo ishara.
Na siku zote sauti ya Mungu ipo kwa lengo la kutufundisha, kutufariji na kutuonya!. Wengi Mungu kashazungumza nasi kwa njia ya Ishara..lakini hatujamsikia Mungu… Wengi tumeshaonywa sana kwa njia ya Ishara lakini hatujasikia..na huku tukidhani Mungu hajawahi kuzungumza nasi…
Neno la Mungu linasema..
Isaya 50:2 “Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu?…”
Umeona?..Kumbe Mungu huwa anatujia lakini hatujui kama ametujia, na huwa anatuita lakini hatusikii!..Ni kwanini?..ni kwasababu hatuijui Sauti ya Mungu.. Tukidhani kuwa ana njia moja tu ya kusema na sisi.
Hebu tumwangalie mtu mmoja katika biblia ambaye Mungu alizungumza naye kwa njia ya Ishara lakini aliipuuzia sauti ya Mungu, iliyokuwepo nyuma ya hiyo ishara.. Na mtu huyo si mwingine zaidi ya Mtume Petro.
Kuna wakati Bwana Yesu alimwambia Petro kuwa “kabla jogoo hajawika mara mbili atamkana mara tatu”..
Hebu tusome,
Marko 14:29 “Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi
30 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu”.
Hapo Bwana Yesu alimpa Petro “ishara ya jogoo” na akampa na “Sauti” moja kwa moja nyuma ya hiyo ishara, kwamba atamkana!. ..Angeweza kumwambia tu “leo utanikana” asimpe na ishara yoyote…lakini hapa utaona hapa Bwana Yesu anampa Petro “Ishara” na “sauti ya hiyo ishara”.
Na kweli wakati ulipofika, Petro akaanza kumkana Bwana Yesu, na pengine wakati anaanza tu kumkana kwa mara ya kwanza..papo hapo “Jogoo akawika”.. na Petro akamsikia Yule jogoo akiwika lakini hakutilia maanani…hakukumbuka kwamba Bwana alimwambia kabla ya jogoo kuwika atamkana!…
Hivyo kwa kuwika tu jogoo mara ya kwanza, ilitosha kumkumbusha Petro dhambi yake na kumfanya “atubu”..
Lakini Petro hakuizingatia hiyo sauti ya Mungu, iliyomwamsha roho yake atubu… badala yake akaendelea na dhambi yake!.. akaendelea kumkana Bwana tena kwa mara nyingine ya pili na ya tatu!.. Lakini kwasababu Bwana ni wa rehema, akairudia tena ishara ile ile, ya jogoo kuwika mara nyingine ya pili..
Na jogoo alipowika mara ya pili, ndipo akili zikamrudia Petro, na kutafakari..na kugundua dhambi yake ambayo tayari ameshairudia mara tatu..Na ndipo akaenda kutubu!..lakini kama asingeisikia sauti ile nyuma ya ile ishara, huenda angeendelea kumkana Bwana zaidi na zaidi na madhara yake yangekuwa makubwa mbeleni.
Umeona hapo!.. tafsiri rahisi ya kisa hicho ni kwamba.. kipindi Petro anaanza kumkana Bwana, Mungu alimtumia jogoo kumwambia Petro, “Acha Hicho unachokifanya”…usimkane Bwana!.. lakini hakusikia, “Yeye alidhani ni mlio wa jogoo tu”…Bwana akarudia tena kwa mara nyingine..Acha!..Sauti iliyotoka ni ya jogoo, lakini katika ulimwengu wa roho ni Mungu anasema acha!, ndipo Petro akapata akili.
Sasa kama Mungu alimtumia jogoo kumwonya Petro, unadhani ni mara ngani katumia watu au wanyama na viumbe kuzungumza nasi?..kutuonya tubadili njia zetu?, tutubu dhambi zetu? Tufanye hiki au kile?..
Je unadhani tukikataa leo kutubu na kulitii Neno lake siku ile tutakuwa na udhuru wowote!..je unadhani siku ile tutakuwa na cha kujitetea kwamba Bwana hajawahi kusema nasi?..Siku ya hukumu utaona ile miti uliyokuwa unadhani ni miti tu, kumbe ilikuwa ni sauti ya Mungu kwako, siku ile utaona ule ugonjwa uliokuwa unakurudia mara mbili mbili ulikuwa ni sauti ya Mungu kwako…
Siku ile utaona wale wanyama waliokuwa wanashambulia mazao yako ni sauti ya Mungu kwako,..siku ile utaona kumbe hata wale wezi waliokuibia na wale matapeli waliokudhulumu, ni Mungu alikuwa anazungumza na wewe,…. na utajuta na kusema laiti ningeisikia ile sauti na kutii!!, na wakati huo utakuwa umeshachelewa.
Na tabia ya Mungu ni kuwa “sauti yake imejificha katika vitu vinyonge tunavyovidharau sisi”… Sauti yake aliificha nyuma ya mlio wa jogoo, kwa Petro, vile vile utasoma pia kuna wakati punda aliweza kusema maneno ya Mungu mbele ya Balaamu.. Vivyo hivyo kamwe tusitegemee kuisikia sauti ya Mungu katika mambo makubwa, yeye anatumia hata vitu vinyonge kusema na sisi..
Bwana Yesu atusaidie tuitii sauti ya Mungu, iliyopo nyuma ya kila ishara yake.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
TEGEMEA MUNGU KUZUNGUMZA NAWE KATIKA MAMBO MADOGO
About the author