Agano ni nini? na kuna aina ngapi za maagano?

Agano ni nini? na kuna aina ngapi za maagano?

Agano ni makubaliano kati ya pande mbili; Na kuna aina saba (7) za maagano kibiblia.

1)Agano kati ya “MTU NA MTU”, 2) kati ya “MTU NA KITU”, 3) kati ya “MTU NA shetani” 4) kati  ya “MTU  NA MUNGU” 5) kati ya  “MUNGU NA MTU”, 6) kati ya “MUNGU NA VIUMBE Vyake” 7) kati ya “MUNGU, NA MWANAE”.

Kwa taratibu tuvitazame vipengele vyote hivyo vya maagano. Na kisha tutajifunza ni Agano lipi lenye nguvu kuliko yote!

  1. Agano kati ya “MTU NA MTU”.

Mfano wa Agano kati ya Mtu na mtu, ni lile Yakobo aliloingia na Labani..Kwamba Yakobo asiwatese wana wake huko aendako.. na wala asije akaongeza mke wake wengine zaidi ya hao wanawe aliompa..

Mwanzo 31:43 “Labani akajibu, akamwambia Yakobo, Hao binti ni binti zangu, na wana ni wanangu, na wanyama ni wanyama wangu, na yote uyaonayo ni yangu; nami naweza kuwatendea nini leo binti zangu na wana wao waliowalea

44 Haya! Na tufanye agano, mimi na wewe, liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe.

45 Yakobo akatwaa jiwe akalisimamisha kama nguzo…………

50 Ukiwatesa binti zangu, na ukitwaa wake zaidi ya binti zangu, wala hapana mtu pamoja nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati ya mimi na wewe?”

Mfano wa mwingine wa Agano la “Mtu na mtu”..ni lile “agano la Ndoa”.. Watu wawili wanafunga ndoa, wanakuwa wameingia Agano la kuishi pamoja, mpaka kifo kitakapowatenganisha..Agano hilo linakuwa ni la mtu na mtu, mbele ya Mungu wa mbinguni. Na ikitokea mmojawapo kavunja agano hilo, basi laana itakuwa kuu yake.

2. Agano kati ya “MTU NA KITU”.

Mtu pia anaweza kuingia agano na kitu.. Kwamfano utaona Ayubu ambaye alikuwa ni mtu mkamilifu sana, aliweza kuingia agano na Macho yake, kwamba asimtazame mwanamke na kumtamani..

Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?”

Hii ikiwa na maana kuwa hata sisi tunaweza kuweka Agano na macho yetu yasitazame ubaya, na midomo yetu isizungumze mabaya na miguu yetu isikimbilie mabaya n.k

3. Agano kati ya “MTU NA SHETANI”

Mtu anaweza kuingia Agano na shetani (miungu), na agano hili ndio baya kuliko maagano yote, kwasababu kamwe shetani hawezi kumpa mtu uzima, bali mauti!. Na maagano haya watu wanaingia aidha kwa kujua au kutokujua.. Mara nyingi Mila na Desturi!, na Kuhudhuria kwa waganga wa kienyeji na maisha ya dhambi ndiyo yanawaingiza watu kwenye maagano na mashetani bila kujua..

Kutoka 23:31 “Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hata bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako.

 32 Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao

33 Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako”

4. Agano kati ya “MTU NA MUNGU”.

Watu pia wanaweza kuingia maagano na Mungu wa mbingu na nchi…Mfano katika biblia utaona kipindi Israeli wamerudi nchini kwao baada ya kukaa utumwani miaka mingi, waliporudi waliweka agano na Mungu kuwa watawaacha wanawake wa kimataifa waliowaona na vile vile wataifuata torati ya Musa.

Ezra 10:3 “Haya basi! NA TUFANYE AGANO NA MUNGU WETU, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati”

5. Agano kati ya “MUNGU NA MTU”

Agano hili linakuwa thabiti, tofauti na lile ambalo mtu anaingia na Mungu, kwasababu Mungu kamwe havunjagi maagano, lakini sisi wanadamu tunavunja maagano, tunayoyaingia.. Mfano wa Agano ambalo Mungu aliingia na mtu au watu, ni lile aliloliingia na Ibrahimu, kuwa atakuwa Baba wa mataifa mengi..

Mwanzo 17: 1 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. 

2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. 

3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema,

 4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi,

 5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.

 6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. 

7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.

 8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.

 9 Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako”.

Agano hili ambalo Mungu aliingia na Ibrahimu, mpaka leo lina nguvu.. Ndio maana unaona ni kwanini Taifa la Israeli bado ni Taifa teule la Mungu. Na ambarikiye Israeli amebarikiwa, na amlaaniye amelaaniwa (Hesabu 24:9).

6. Agano kati ya “MUNGU NA VIUMBE”

Mungu pia anaweza kuingia agano na viumbe vyake alivyoviumba.. vilivyo na uhai na visivyo na uhai.. kama kama wanyama na mawe na miti na mabonde… Mfano wa Agano kama hili ni lile alilolifanya wakati anaigharikisha dunia, nyakati za NUHU.

Mwanzo 9:9 “Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu;

 10 tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi.

11 Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. 

12 Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; 

13 Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.

14 Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni,

 15 nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

 16 Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi”.

Agano hili Mungu aliloingia na ardhi na wanyama kwamba hatawagharikisha tena kwa maji, lina nguvu mpaka leo, ndio maana utaona tangu wakati wa Nuhu mpaka leo hakuna gharika tena, na ule upinde tunaouna ni ishara ya agano lake hilo aliloingia nasi pamoja na viumbe vyote..

7. Agano kati ya “MUNGU, NA Mwanawe”.

Hili ndio Agano kuu, na lenye Nguvu kuliko maagano yote!.. Agano hili ndio lile aliloingia na Mwanawe mpendwa Yesu Kristo, kupitia Damu ya mwanawe. Na kwanini Agano hili lina nguvu?.. ni kwasababu Yesu Kristo ni Mungu katika mwili, hivyo Agano hili, ni Mungu kaingia na NAFSI YAKE MWENYEWE. Hivyo haliwezi kuvunjika wala haliwezi kupungua nguvu..

Agano la Mungu aliloingia na viumbe vyake kwamba havitagharikishwa kwa maji, ni kweli mpaka leo lina nguvu, lakini itakuja gharika nyingine ya moto na si ya maji, hivyo Agano la kwanza limetupa uzima lakini si wa milele, kwasababu itakuja gharika nyingine ya moto..

2Petro 3:6 “kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7  Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”.

Lakini Agano la Damu ya Yesu ni Agano jipya, na la Mwisho, hakuna agano lingine litakalokuja katika haya maisha litakalokuwa timilifu zaidi ya hili. Kwamba kila amwaminiye Mwana wa Mungu (YESU KRISTO), anao uzima wa Milele, na anakuwa mrithi wa Baraka na ahadi za Mungu.

Kwahiyo ni muhimu sana kumpokea Yesu kila mmoja, ili tuweze kushiriki Baraka hizi za Agano jipya la Mungu.

Na damu ya Agano jipya, (yaani Damu ya Yesu), ina nguvu kuu ya kuvunja maagano yote, mtu aliyoingia na miungu, au shetani.. na kumwacha mtu kuwa huru kabisa kabisa.

Je umeingia ndani ya Agano la Damu ya Yesu?..

Kama bado, Mlango wa Neema bado upo wazi, lakini hautakuwa wazi hivyo siku zote, siku moja utafungwa na hakuna atakayeweza kuinga.. Kama unataka uzima, na kheri, basi mpokee Yesu, lakini kama hupendi uzima wala kheri basi baki kama ulivyo…

Waebrania 12:24  “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.

25  Angalieni msimkatae yeye anenaye. Maana ikiwa hawakuokoka wale waliomkataa yeye aliyewaonya juu ya nchi, zaidi sana hatutaokoka sisi tukijiepusha na yeye atuonyaye kutoka mbinguni”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Watu wenye kuvunja maagano ndio watu wa namna gani? (Warumi 1:31)

Tofauti kati ya mtu na mwanadamu ni ipi?

EZEKIELI, ITABIRIE MIFUPA MIKAVU.

MJUMBE WA AGANO.

KUVUNJA MAAGANO YA UKOO.

SHUSHANI NGOMENI NI WAPI KWA SASA?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
7 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Elias Joseph Mbowe
Elias Joseph Mbowe
1 year ago

Nimebarikiwa sanaa

Fidelis Kassian Augustine
Fidelis Kassian Augustine
1 year ago

Be Blessed For The Fruitful Lesson

Fidelis Kassian Augustino
Fidelis Kassian Augustino
1 year ago

Am too Interested With The Lesson…God Keep you..

Anonymous
Anonymous
1 year ago

Leave your message