MJUMBE WA AGANO.

MJUMBE WA AGANO.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe..karibu tujifunze Biblia…

Malaki 3: 1 “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi”

Mpango wa Mungu katika kumwokoa mwanadamu umegawanyika katika sehemu mbili..Agano la kale(au kwa lugha nyingine agano la kwanza)..pamoja na Agano jipya (au agano la pili).

Ndio ni kawaida lazima viwepo vipande viwili ili kukikamilisha kiumbe hai..Na upande mmoja lazima uwe na nguvu kuliko mwingine…Kwamfano umbile la Mtu limegawanyika katika sehemu mbili zinazofanana…Upande wa kushoto na upande wa kulia…Ndio maana utaona mtu ana miguu miwili, macho mawili, mikono miwili, n.k Na kama ukizidi kuchunguza utaona pia..katika sehemu hizo mbili kuna upande mmoja upo na uwezo mkubwa kuliko upande mwingine..ndio utaona mtu anauwezo wa kuandika vizuri kwa kutumia mkono mmoja tu, na akijaribu kutumia upande mwingine inakuwa ni shida kidogo.. kadhalika anauwezo hata wa kupiga teke kitu kwa utashi Zaidi kupitia huo huo upande anaoutumia mkono wake kuandikia n.k Lakini pande zote hizo mbili zikishirikiana kwa pamoja uwezo unakuwa mkubwa Zaidi..mtu akinyanyua kitu kwa mikono miwili anafanikiwa Zaidi kuliko anayetumia mkono mmoja. N.k

Na biblia ni hivyo hivyo imegawanyika katika sehemu kuu mbili..Agano jipya na Agano la Kale. Agano jipya lina nguvu na uwezo na utashi Zaidi kuliko agano la kale…Ingawa maagano yote mawili ni lazima yaungane ili kulitimiza kusudi la Mungu. Kama vile tusivyoweza kusema hatuhitaji mkono wa kushoto kwasababu ni dhaifu kuliko wa kulia, au hatuhitaji mguu wa kushoto kwasababu ni dhaifu kuliko wa kulia..hapana..vyote viwili vina umuhimu wake..

Sasa Agano la kale mjumbe wake alikuwa Nabii Musa..ambaye ndiye aliyepewa zile amri na sheria awahubirie wana wa Israeli. Na sheria zile zilikuwa zinaandikwa kwenye mawe, na mbao..

Musa alihubiri….Mtu hatakiwi kuzini kwasababu sheria inasema usizini!…mtu hatakiwi kuiba kwasababu sheria inasema usiibe!…Ikiwa na maana kuwa kuna maandishi fulani ya kurejea ili kuzijua amri za Mungu..Kuna mahali fulani pameandikwa kwamba USIZINI! Ndio maana watu hawapaswi kuzini.

Hilo ndio Agano la kwanza…Sheria zilikuwa zimandikwa mahali fulani.

Lakini Agano la pili ambalo mjumbe wake ni Yesu Kristo..kama maandiko yanavyosema katika..

“Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili”.

Yeye(Yesu) sheria za Mungu haziandiki kwenye mawe na mbao na kutupa sisi kama alivyofanya Musa…bali katika vilindi vya mioyo ya watu ndiko anapoziandikia…Maana yake ni kwamba mtu akitaka kupata uhakika kwamba ulawiti ni dhambi bila hata ya kwenda kurejea kwenye maandishi yoyote…inakuwa ile sheria tayari imeshaandikwa ndani yake..Kunakuwa kuna kitu fulani kinamshuhudia ndani yake na kumfundisha kwamba ulawiti ni machukizo kwa Mungu bila hata kwenda kusoma mahali popote…yaani zile sheria za Mungu zinakuwa zinaandikwa moyoni mwake. Kunakuwa kuna masomo fulani yanatiririka ndani yake kupitia hata vitu vya asili kiasi kwamba yule mtu anauwezo wa kutenda mapenzi ya Mungu bila hata kusukumwa sukumwa wala kuwekewa sheria na taratibu, na amri fulani za kufuata kama mtoto mdogo. Anakuwa kila kitu anachokifanya anajua sababu yake.

Ni kama mtu ambaye kakomaa kiakili ambapo anajua akilowa jasho tu anahitaji kwenda kuoga na kubadilisha nguo…anakuwa hana kitabu cha baolojia mbele yake ambacho anatembea nacho na kukirejea kila siku na kutafuta mahali panaposema mtu ni lazima aoge ndipo awe msafri Yeye mwenyewe tu ndani ya akili yake kuna masomo tayari ya umuhimu wa kujiweka msafi bila hata kufundishwa na mtu. Hahitaji kitabu cha baolojia kumfundisha umuhimu wa kuoga, hahitaji kuhubiriwa hubiriwa kila kona umuhimu wa kuoga..haihitaji kukalishwa semina na kukumbushwa kumbushwa…Kwani anajua wajibu wake..kwanza yeye mwenyewe tu atajikuta anapenda kuwa msafi…Na kila siku utakuwa anazidi kutafuta kujiweka kuwa msafi.

Na ndivyo hivyo hivyo Agano jipya linavyofanya kazi… linamfanya mtu atafute kuwa msafi (yaani Mtakatifu) bila kuwekewa sheria wala kusukumwa sukumwa..linamfanya mtu aone ndani yake kwamba kuna kila sababu ya yeye kujiweka mbali na uchafu wa ulimwengu huu, kujiweka mbali na anasa, uasherati, utukanaji, usagaji, wizi…Linazidi kumfanya aone sababu ya yeye kuiogesha roho yake kila siku kwa kujifunza Neno na maombi…Agano hili halihitaji kila siku kumkumbusha mtu wajibu wake.. Wote walioingia katika agano hili wanatimiza sheria ya Kristo ndani ya mioyo yao bila shuruti. Na hiyo yote inachochewa na Roho Mtakatifu atakayeingia ndani ya mtu.

Utauliza ni wapi katika maandiko, Agano hili la sheria kuandikwa ndani ya mioyo yetu lilitabiriwa..?

Waebrania 8:8 “Maana, awalaumupo, asema Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya;

9 Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana.

10 Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; NITAWAPA SHERIA ZANGU KATIKA NIA ZAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAZIANDIKA; NAMI NITAKUWA MUNGU KWAO, NAO WATAKUWA WATU WANGU.

11 Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.

12 Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena.

13 Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka”

Unaona hilo ndio agano jipya!… Ukitaka kutafuta ni wapi kwenye biblia Mungu kakataza sigara ni Dhahiri kuwa agano hili bado halijakuingia ndani yako..ukitaka kutafuta ni wapi kwenye biblia nguo za kubana na suruali, na vimini, na vipodozi vimekatazwa…fahamu kuwa bado agano hili halijaingia ndani yako, ukitafuta kwenye biblia ni wamendikwa usitoe mimba ni dhambi, au usitumie madawa ya kulevya.. Ni sawa na kutafuta ndani ya kitabu cha baolojia ni wapi pamekataza watu kupiga mswaki?

Je! Unataka kuingia ndani ya hili agano leo?..Yupo Mjumbe wake…ni lazima umkubali huyo kwanza…ukimkubali huyo na akiingia ndani yako atayaondoa yote ya kale na kuyafanya yote kuwa mapya..Atazibua ufahamu wako kwa Yule ROHO MTAKATIFU atakayekupa kiasi kwamba utaona kuzishika sheria za Mungu sio ngumu..utaona kuwa mtakatifu sio kugumu…

Unaona Watoto wadogo wanavyosumbua kuoga wenyewe mpaka uwalazimishe sana..lakini mtu mzima anakuwa anaoga hata mara 3 kwa siku kwa miaka 20..na wala hachoki?..Ndivyo na wewe Yesu Kristo atakachokifanya ndani yako…Ataigeuza akili yako kwa Roho wake Mtakatifu na kuwa kama ya mtu mzima…hutatamani hata kusikia harufu ya uasherati, wala matusi, wala uchungu, wala vinyongo, wala kujichua, wala kutazama picha chafu mitandaoni, wala pombe. Na juu ya hayo atakupa uzima wa milele.

Waebrania 9:15 “Na kwa sababu hii ni MJUMBE WA AGANO JIPYA, ILI, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele”.

Kama unataka leo Mjumbe huyo aingia ndani yako na kukutengeneza…

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, .

NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu katika Roho na Kweli, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

TOFAUTI KATI YA SHERIA YA ROHO WA UZIMA NA SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI!

KWANINI WENGINE WANYAKULIWE,NA WENGINE WAACHWE?

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

Kwanini Bwana Yesu, aliruhusu yale mapepo yawaingie nguruwe?

Sanduku la Agano lilikuwa linawakilisha nini katika Agano jipya?

ANGALIA USIJE UKANG’OA NGANO KATIKATI YA MAGUGU.

MAJINI WAZURI WAPO?

JE KUPONYWA NI UTHIBITISHO WA MUNGU KUWA NA WEWE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments