MAFUNDISHO MAALUMU KWA WANANDOA: Epusha Wivu katika ndoa:
Huu ni mfululizo wa mafundisho maalumu yawahusuyo wanandoa: Ikiwa hukupata sehemu za nyuma, basi waweza kututumia ujumbe kwa namba zetu zilizo chini ya somo hili, tukutumie;
Leo tutaona jinsi wivu unavyoweza kuathiri kwa sehemu kubwa mahusiano ya wanandoa.
Kibiblia wivu upo wa aina mbili:
1) Wivu wa kipepo: Ni ule wa kumuonea mtu kijicho, yaani kutotaka, mwenzako kufanikiwa kwasababu wewe hukufanikiwa kama yeye alivyofanikiwa, kutaka kile ambacho mwenzako anacho uwe nacho wewe huku hutaki yeye awe nacho. Biblia imetuonya sana dhidi ya wivu huu, kwasababu ni zao la shetani. Ndio walikuwa nao masadukayo na makuhani kwa Bwana wetu Yesu na mitume wake, pale walipoona neema ya Mungu ipo juu yao kubwa lakini kwao haipo, (Matendo 5:17, Warumi 13:13)
2) Wivu wa kimahusiano: Wanandoa, Huu ni wivu ambao ni wa asili, Mungu kauweka ndani ya mtu, huu upo katika mahusiano ya kindoa,au maagano Na ndio Wivu ambao Mungu amekiri pia mwenyewe anao.(Kutoka 20:5)..Huu ni wa kuulinda sana, hususani pale unapoingia kwenye ndoa, kwasababu madhara yake ni makubwa zaidi hata ya hasira, au ghadhabu. Biblia inasema hivyo katika..
Mithali 27:4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu”.
Huu ndio umesababisha watu, kugombana, kuchukiana, kusalitiana na hata wakati mwingine kuuana, na kuwasababishia matatizo na wengine ambao hata hawahusiki.
Leo tutatazama, ni kwa namna gani, kinywa cha mwanamke, kinaweza kuwasha wivu mbaya sana, kwa upande wa pili. Na somo linalofuata tutaona tabia ambazo mwanaume anapaswa ajiepushe nazo, kuepukana na madhara ya wivu kwenye ndoa yake.
hii itakusaida, kuishi kwa amani na utulivu na kuinusuru ndoa yako, .
Sasa embu tusome kisa hichi tunachokiona katika 1Samweli 18:7. Si kisa cha kindoa lakini ni kisa kimuhusucho Daudi na Sauli, Wengi wetu tunajua sababu iliyomfanya Sauli amchukie Daudi, ambaye hapo mwanzo alimpenda ilikuwa ni Wivu. Lakini wachache sana, wanafahamu CHANZO cha wivu huo, kilikuwa ni nini?
Biblia inatupa majibu, kilikuwa ni wanawake, waliotoka na kutoa sifa zao, mahali pasipostahili kwa wakati ule. Embu Tusome.
1Samweli 18:5 “Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; SAULI AKAMWEKA JUU YA WATU WA VITA; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.
6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.
7 NAO WALE WANAWAKE WAKAITIKIANA WAKICHEZA, WAKASEMA, SAULI AMEWAUA ELFU ZAKE, NA DAUDI MAKUMI ELFU YAKE.
8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?
9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile”.
Hicho ndicho kilichokuwa chanzo, cha vita vya Daudi na anguko la Sauli,. Wanawake wale walikuwa wanasema kweli, kwa waliyoyaona, lakini hawakutumia busara kuimba mbele ya mfalme, kwa wakati ule.. Huwenda hata Daudi, alitamani wakae kimya, wasimsifie yeye zaidi ya mfalme wake, mbele ya umati.. Lakini wale wanawake hilo halikuwa akilini mwao. Hawakujua kuwa kumbe nyimbo zao, sifa zao, maneno yao, ni panga ndani ya mioyo ya wakuu wao.
Ndio ikawa sababu ya Sauli kughahiri, hata vyeo vyote alivyompa Daudi, akampokonya na kumfukuza na kutaka kumuua kabisa, kwa kosa tu la wale wanawake. Lakini kama wale wanawake wangetumia busara, kumwimbia mfalme zaidi, basi Daudi angeendelea kustarehe na kudumishwa katika ufalme ule.
Maana yake ni nini?
Maneno yoyote ya sifa yanayotoka kinywani mwako wewe kama mwanamke, yana matokeo makubwa sana kwa upande wa pili. Sasa tukirudi katika upande wa ndoa, Wivu unatokea pale ambapo unathamini, au unasifia wanaume wengine zaidi ya mume wako. Ukiwa umeolewa tambua kuwa mume wako ndio,bora kuliko wanaume wote ulimwenguni, ndio mwenye sifa zote kuliko wanaume wote ulimwenguni.Hata kama wale wengine wamemzidi yeye kwa kiwango kikubwa kiasi gani, acha kuwazungumza zungumza mbele ya mume wako.
Hii ni kwa faida yako, na kwa wengine. Wanaume wengi wanagombana na marafiki zao vipenzi, kisa tu wake zao,wanapowasifia, wanakuwa mpaka maadui kwa sababu ndogo ndogo tu kama hizi,..Labda utasikia mmoja anasema, “mume wangu,rafiki yako huwa anapendezaga uvaaji wake, yaani navitiwa nao”..Kauli kama hizi ziepuke kinywani mwako, ili kunusuru, urafiki au ujirani wenu.
Kwa ufupi kauli zozote za sifa, zichungumze mara mbili mbili; Unaweza usione shida yoyote, au ukadhani ni jambo dogo tu, lakini upokee huu ushauri utakufaa kwa siku za mbeleni, , hilo jambo linamuathiri sana mwanaume. Usimzungumze zungumze mwanaume mwingine mbele ya mumeo, isipokuwa kwa kiasi, hata wale unaowaona kwenye tv, au unaowasiliana nao kwenye simu. Kumbuka wivu unawashwa na mambo madogo sana.
Bwana akubariki.
Je! Umeokoka? Je! Unauhakika wa maisha yako ya milele baada ya kifo? Kumbuka Kristo yupo mlangoni kurudi, dalili zote zimeshatimia, Huu si wakati wa kumbelezewa tena wokovu, ni wakati wa kujitahidi kuingia ndani ya Safina(Yesu Kristo) kwa nguvu zote, maana muda umekwisha.. Tubu dhambi zako, ukabatizwe mgeukie Bwana akupe uzima wa milele.
Maran Atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)
WANA-NDOA: Baba Mkwe, Na mama Mkwe.
About the author