Kama watu wamefunga ndoa ya serikali na wakaachana, wanaweza kuoa au kuolewa tena na watu wengine?
JIBU: Shalom, Ndoa iliyofungwa kiserikali, au kwa namna yoyote ile…ambayo imehusisha makubaliano ya pande zote mbili na taratibu zote ikiwemo mahari na kutangazwa mbele ya jamii kuwa watu hao wawili wamekuwa mume na mke…kwa namna yoyote ndoa hiyo haipaswi kuvunjwa kwasababu imetangazwa tayari mbele ya mashahidi, hivyo hiyo tayari ni ndoa (ingawa sio ya kikristo)..
Na endapo ikitokea wawili hao wamefunga ndoa hiyo ya kiserikali na wakaachana, basi mbele za Mungu watakuwa na hatia…(Na kumbuka ndoa ya kiserikali hawafungi na wakristo, yaani maana yake mtu ambaye tayari ameshamjua Yesu Kristo na kumwamini, hawezi kwenda kufungishwa ndoa ya kiserikali, mkristo anayefunga ndoa ya kiserikali ni mwasherati), wanaofungishwa ndoa hizo za kiserikali ni wale ambao bado hawajamjua au kumwamini Yesu Kristo, au kwa namna nyingine wapagani, mfano wa ndoa hizo ni kama ile ya Herodia ambayo alimwacha mumewe aliyeitwa Filipo na kwenda kuolewa na ndugu ya mume wake, sasa ndoa hiyo ya Herodia na Filipo haikuwa ya kikristo, pengine ilikuwa ya kiserikali au ya kitamaduni za taifa lao au ya kidini yao lakini maadamu ilikuwa imeshahalalishwa na jamii yao au serikali yao basi ilikuwa ni dhambi kwa Herodia kumwacha mume wake huyo na kwenda kuolewa na ndugu ya mume wake (kasome kisa hicho katika Marko 6:17-18).
Lakini ikitokea mmoja wa waliofungishwa ndoa ya namna hiyo /kiserikali kaamini na kuwa mkristo na mwenzake hataki kuishi naye kwasababu tu kawa mkristo na akaamua kumuacha..hapo huyu aliyeachwa kwasababu ya Imani yake ya kikristo atakuwa huru kuolewa/kuoa na mtu mwingine ambaye ni mkristo mwenzake tu, lakini kama hata baada ya kuokoka kwake mwenziye ambaye anaishi naye hataki kuokoka lakini bado anataka kuendelea kuishi naye..huyu hana budi kuendelea kuishi naye hata kama hajaokoka..na endapo akimwacha kwasababu tu hataki kuokoka atakuwaa na hatia mbele za Mungu..Na akimwacha na kwenda kuoa/kuolewa na mwingine atakuwa anazini.
Sasa wapo watu huko nyuma kabla ya kuokoka walifunga ndoa ya kiserikali, na baada ya kuokoka wanapojaribu kuwashawishi wake zao/waume zao nao pia waokoke kama wao, wanapowaona wanakataa basi wanakusudia kuwaacha..ingawa bado wanapedwa na hao wenza wao na hawajaachwa..lakini wao kwasababu wameokoka hawataki tena kuishi na wale waume zao/wake zao ambao hawajaokoka..Ndugu usifanye hivyo ni dhambi kubwa sana!..Mume wako/mke wako uliyefunga naye ndoa hata kama ni mlevi lakini hataki kukuacha, basi hupaswi kumuacha…na hiyo ni kulingana na Biblia kasome..1Wakorintho 7:10-15.
Na pia ikitokea wote wawili hapo kwanza walikuwa wamefunga ndoa ya kiserikali na sasa wameokoka na kuifahamu neema ya Kristo, Hawa wote wawili wanapaswa kwenda kanisani kuifanya ndoa yao iwe ya kikristo. Kwasababu ilipofungwa kiserikali haikumhusisha Kristo wala maagizo yake, Wanapaswa kwenda kuahidiana upya mbele za Mungu na wanadamu kwamba wataishi kwa uaminifu pasipo kuachana, na kifo ndicho kitakachowatenganisha, na kwamba watakuwa kielelezo kwa watakatifu wengine wowote kwa kuishi katika ndoa ya kikristo ya mume mmoja na mke mmoja, na mambo mengine ambayo watayaahidi mbele ya kanisa la Mungu na mbele ya Kristo mwenyewe. Baada ya hapo ndoa yao itabarikiwa na Mungu, na kuwa ya kikristo na zile baraka zote za wanandoa zitafuatana nao.
Sasa kuna kundi lingine ambalo linajiita ni wanandoa…Hili ni lile ambalo walikutana tu na kuamua kuishi Pamoja, pasipo utaratibu wowote…ni ile watu wawili wamekutana tu kijana na binti na kuwekana ndani, hakuna cha mahari, hakuna imani. Hawa kibiblia wanafanya uasherati (NI WAASHERATI).
Na endapo ikitokea mmoja kaamini katika hali hiyo waliyopo ya kukaa Pamoja (maana yake katubu na kuwa Mkristo). Moja kwa moja yule aliyeamini anapaswa avunje hayo mahusiano, kwasababu ni uasherati ndio aliokuwa anaufanya..Anapaswa avunje hayo mahusiano hata kama wameshazaa Watoto, arudi kwa wazazi wake, au akaishi peke yake kwa kujitegemea na wanawe… mpaka huyo mwenzake naye atakapotubu kama yeye na kuwa mkristo na kwenda kufunga ndoa kanisani. Lakini endapo huyo mwingine kakataa kutubu katakata na kujisalimisha kwa Yesu Kristo, basi huyu aliyetubu yupo huru kuolewa/kuoa mtu mwingine lakini aliye mkristo kama yeye tu!…(hapaswi kwenda kuoa/kuolewa na mtu ambaye sio mkristo)
Kumbuka tena mtu ambaye ameshamjua Yesu Kristo, na kufahamu kuwa ndoa halali ni ile ya kikristo (mfano wa mimi na wewe ambao tumeshajua sasa) na ameshafahamu kuwa inapaswa ifungwe mbele ya kusanyiko la Kristo, akienda kufunga ndoa yoyote ile kinyume na hiyo, akaenda kufunga ndoa aidha ya kimila au ya kiserikali au akijichukulia tu mke/mume na kuishi naye ndani…pasipo kwenda kuifungisha ndoa yake kanisani BASI ANAFANYA UASHERATI!!…Na waasherati wote biblia inasema hawataurithi ufalme wa mbinguni (1Wakoritho 6:9).
Na pia maana halisi ya neno ndoa ni Muunganiko wa MUME na MKE na sio muunganiko wa mume na mume au mke na mke…Hivyo hicho kinachoitwa ndoa ya jinsia moja hakipaswi kiitwe hivyo…kinapaswa kiitwe “uasherati wa jinsia moja”…na sio “ndoa ya jinsia moja”..Hivyo serikali inayohalalisha “uasherati wa jinsia moja” Huo Mungu kaukataa na ni machukizo makubwa mbele za Mungu..kasome Walawi 20:13.
Je umemwamini Yesu Kristo?, kama bado unasubiri nini?, hizi ni siku za mwisho na Kristo yupo karibuni kulichukua kanisa lake, je utakuwa miongoni mwa watakaonyakuliwa, Unafahamu kuwa kanisa hili tunaloishi ndio kanisa la mwisho, hakutakuwa na kanisa lingine baada ya hapa?
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?
Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?
NDOA NA HARUSI TAKATIFU.
Je! ni halali kutoa cheti kwa wakristo wanaooa?
NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.
Rudi Nyumbani:
Print this post
Kwanini unaipinga ndoa Ya Kiserkali Mwalimu? Nazani Ni Jambo Nzuri kulingana
Na Desturi Ama Katiba Ya inch inapashwa Ndoa yangu ijulikane Kiserkali. Ya Kaisari yaliyo Ya Kaisari na Ya Mungu yaliyo Ya Mungi
Shalom..Nadhani hapo hatuzungumzii ndoa kutambuliwa na serikali..kinachozungumziwa ni ndoa ya kiserikali VS ndoa ya kikristo.. Ikiwa ndoa yako umeifungisha kanisani, ikiwa upo utaratibu wa kutambuliwa na serikali ni vema, lakini ndoa tu inayofungwa serikalini halafu haitambuliwi na Mungu hiyo sio ndoa ya kikristo
Shalom.
Bwana Yesu asifiwe sana.
Hii mada ya ndoa za serikalini ina maandiko mengi yanayopingana (a lot of contradicting statements) ambayo yanaleta mkanganyo badala ya kuujenga mwili wa Kristo.
Je, biblia inapinga ndoa ya serikalini kwenye andiko lolote? Kama la, basi kwa nini muiite ni ‘uasherati’?
Imeandikwa Warumi 13:1-2 [1]Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.
Utaratibu wa kiserikali usiovunja moja kwa moja amri za Mungu umewekwa na Mungu mwenyewe. Hebu tafakarini mlichoandika.
Je, Mungu hayupo serikalini hadi mseme hiyo ndoa sio ya Mungu?
Na kama munaita ndoa ya serikalini ‘uasherati’, kwa nini mnasema wasiachane hata kama mmoja wa wanadoa anataka ndoa iendelee? Hamuoni mnachanganya mambo hapo?
Je, kila ndoa ya kanisani ndio ndoa ambayo Mungu yupo? Hamjasoma ya kuwa yapo makanisa ambayo ni ‘kiti cha enzi cha shetani?’. Ni mungu gani anayeshuhudia ndoa zilizofungwa kwenye makanisa hayo? Si shetani mwenyewe???
Je, uwepo wa Mungu kwenye ndoa ni kwa sababu wamefunga ndoa kanisani, kimila au serikalini? (hata makanisa feki yaliyo kibiashara nayo yanajiita ‘kanisa’)… Au uwepo wa Mungu kwenye ndoa ni ‘state of heart’ ya hao wanandoa? Kama wanaye Mungu ndani ya mioyo yao, si huyo Mungu anatembea nao popote pale watakapokuwepo? Kwani Mungu amefungwa kwenye specific location?
Ni maoni yangu hili somo liandikwe upya baada ya tathmini.