Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku nyingine tena yenye neema za Bwana.
Napenda leo tujifunze, ni nini kwanza Bwana anahitaji kuona kwetu kabla ya yeye kuachilia neema zake katika mambo tumwombayo au tuyatafutayo. Embu tusome habari hii kwa mara nyingine tena..
Luka 5:4 “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. 5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, TUMEFANYA KAZI YA KUCHOSHA USIKU KUCHA, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. 6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; 7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. 8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. 9 Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata;”
Kumbe Bwana Aliona taabu ya Petro usiku ule ilivyokuwa, aliona kule kutafuta kwake usiku kuchwa pasipo mafanikio kulivyokuwa. Alipokuwa anatupa nyavu hapati, anajaribu tena hapati, anasogea sehemu nyingine avue ndio anakosa kabisa mpaka kunapambazuka, haambulii chochote..
Na ndio maana hatushangai jambo la kwanza Yesu alilomwambia Petro mara baada ya kuhubiri kwake, sio Petro twende shambani kwako nikakubariki, au twende tukahubiri injili, ..Hapana bali tweka vilindini ukavue samaki, nikabariki kwanza kwa kile ulichokuwa unakisumbukia kwa muda mrefu..
Hata sasa Kristo ni Yule Yule, kabla ya kutupigisha hatua yoyote kiroho..Hatuna budi kwanza tufanye kazi ya kuchosha usiku kucha, wakati mwingine bila mafanikio yoyote. Watu wengi wanataka Mungu atembee nao kwa viwango vya juu zaidi, lakini hawapo tayari kutaabika kwanza, hawapo tayari kutumika kwanza, katika utumishi wa Mungu kwa muda mrefu, tena ule ambao hauonyeshi matunda yoyote ya awali, lakini tunataka tulale, tuamke kesho tuwe kama Musa.
Huduma nyingi zimekufa kwa namna hii, pale wanapoona hakuna maendeleo au hatua zozote, mwishowe wanakata tamaa ya kumtumikia Mungu, wanavunjika moyo, wanaghahiri, wanakwenda kutafuta shughuli nyingine.
Ndugu, Hatuna budi kufahamu wakati mwingine ni desturi ya Mungu kutuacha kwanza, kwa kipindi Fulani, atupime uaminifu wetu, lakini pia atutengeneze, si kila wakati mambo yote yatakuja papo kwa papo kama wengi wanavyosema, yaweza kuchukua mwaka kama sio miaka, lakini tukivumilia, siku isiyokuwa na jina tutashangaa vile tulivyovitamani, tunavipata kwa urahisi sana, tena bila kusumbukia, wala kuchukua muda kama ilivyokuwa hapo mwanzo, Hatua kama hiyo ukishaifikia, ujue tayari Kristo ameshaona utumishi wako. Lakini lazima tufanye kazi ya kuchosha usiku kucha.
Waweza kusema, jambo kama hili alilifanya siku hiyo tu ya kwanza alipokutana na Petro, lakini utaona mwishoni kabisa mwa huduma yake kuwa nao, baada ya kufufuka kwake, mitume kwa mara nyingine tena walienda kuvua samaki, lakini usiku ule wote hawakupata kitu, ilipofika asubuhi wakamwona Yesu amesimama pwani, ndipo akawauliza wanangu mna kitoweo? Wakasema hapana, akawaambia watupe jarife upande wa kulia watapata (Yohana 21:1-13)
Na kweli samaki ambapo waliwasumbukia usiku kuchwa, wakawapata kwa dakika tano, tena sio kule vilindini bali pale pale pwani. Unataka Mungu aikuze huduma yako, tumika kwanza kwa Bwana, fanya uinjilisti sana, hata kama huoni mtu yeyote ameokoka leo au kesho, wakati wa Bwana ukifika, utaona maajabu. Lakini ukikata tamaa, ukasema sioni chochote, Kristo atasema hustahili kupokea neema.
Wewe ni mwimbaji wa Injili, imba sana, dumu kwa uaminifu kufanya mazoezi, tunga, jifunze kwa moyo wako wote, nyimbo za utakatifu, na kuponya,bila ulegevu, hata kama utaambiwa hujui kuimba,wewe imba sana, hata kama miaka 10 itapita bila kuona kazi yako inamponya mtu..endelea tu, wakati utafika wa Bwana kuachilia neema yake, ataibariki sauti yako, na kuwa msaada ya maelfu ya watu duniani. Sauti itakuwa ni ileile lakini itajazwa neema na nguvu.
Kuna wakati ambao Yesu alipowalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, waende ng’ambo, usiku ule bahari iliwachafukia, lakini maandiko yanatuambia Yesu aliwaona wakitaabika katika kuvuta makasia, lakini hakufanya chochote, mpaka usiku sana wa manane ndio akawafuata akiwa anatembea juu ya maji. Ndipo akawatulizia dhoruba yao. (Marko 6:45-52).. Katika habari ile utajiuliza ni kwanini Yesu awaache wataabike, muda wote ule bila kuchukua hatua..jibu ni kuwa alikuwa anawajengea ushuhuda. Nasi pia Kabla ya Yesu kuzimisha dhoruba katika maisha yetu, na kutupa amani daima, yatupasa tuwe wastahimilivu sasa katika majaribu mengi na shida kwa ajili ya jina lake.
Luka 6:21 “Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka”.
Jambo lolote la ki-Mungu unalopenda kulifanya, litende kwasababu Mungu anataka kuona kwanza kiu yako kwenye hilo jambo. Vilevile kama unataka Mungu akubariki, penda kutoa bila kutazamia malipo yoyote sasa, toa tu, hata kama ni kwa miaka, unaona unapata hasara tu, usikate tamaa, malipo yake utayaona wakati Fulani mbeleni, Bwana atakapoachilia neema zake.
Hii ni kanuni ya Ki-Mungu, aliitumia kwa, kwa Ibrahimu, Kwa Yusufu, kwa Musa, hata na kwetu pia anaitumia ikiwa tutakubali kwanza kufanya kazi ya kuchosha isiyokuwa na faida kwa muda mrefu.
Usikate tamaa, Bwana awe nawe.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.
Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?
REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.
USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU UKAE NANYI NYOTE.
Biblia inamaanisha nini iliposema “wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa;?
About the author