Swali: Katika Wagalatia 3:13 maandiko yanasema Bwana Yesu alisulubiwa juu ya mti, lakini tukirejea tena Yohana 19:19, tunaona biblia inasema Bwana alisulubishwa juu ya msalaba.. je maumbile ya huo msalaba au huo mti yalikuwaje?.. je ulikuwa ni mti uliosimama kama nguzo au miti miwili iliyokutana kama alama ya kujumlisha?
Jibu: Tuirejee mistari hiyo..
Wagalatia 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu AANGIKWAYE JUU YA MTI”.
Na tena..
Yohana 19:19 “Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI”.
Bwana Yesu alisulubiwa juu ya msalaba ambao ulikuwa ni wa malighafi ya mti, na si wa malighafi ya chuma, au ya shaba, hiyo ndio maana ya “kuangikwa juu ya mti”,
Lakini tukirudi katika umbile la msalaba wa Bwana kama ulikuwa ni wa wima mfano wa nguzo au wa kukutana mfano wa alama ya kujumlisha, ili tujue maumbile yake yalikuwaje ni lazima turejee historia kidogo, kwasababu biblia haijatoa maelezo juu ya umbile la msalaba, maelezo iliyotoa ni malighafi ya msalaba tu!.. kuwa ni malighafi ya mti kama tulivyosoma hapo katika Wagalatia 3:13.
Tukirudi katika Historia sote tunajua kuwa wakati Bwana yupo duniani, utawala uliokuwa unatawala dunia nzima ulikuwa ni utawala wa Rumi, na ndio uliomsulubisha Bwana Yesu.
Sasa kulingana na historia, warumi walikuwa na adhabu nyingi walizowahukumu nazo wahalifu. Na mojawapo wa adhabu walizozitoa kwa wahalifu wakuu ilikuwa ni kumtundika mtu juu ya msalaba, na msalaba huo haukuwa nguzo moja ndefu, hapana bali ulikuwa ni nguzo mbili zilizokutana! (kafuatilie historia).
Hivyo mtu alining’inizwa mikono ikielekezwa katika nguzo mlalo na miguu na kichwa vikielekezwa katika nguzo wima, na mwili huo ukishikiliwa na misumari, na watu walisulubiwa uchi wa mnyama pasipo hata kuwa na kipande chochote cha kuzuia hata sehemu za siri.
Lengo la adhabu hiyo ilikuwa ni kumtesa mtu huyo kwa mateso na maumivu makali, na pia kumwua kwa kifo cha aibu, kutokana na kosa lake alilolifanya. Lakini si wahalifu wote waliokuwa wanahukumiwa adhabu hiyo, bali wale waliokutwa na kosa la kustahili kusulubiwa hivyo.
Kwahiyo Bwana Yesu aliangukia katika hukumu ya namna hii ya kusulubiwa juu ya msalaba, ingawa hakufanya kosa la kustahili kuuawa!, Lakini kwasababu ilikuwa ni kwa makusudi ya ukombozi wetu ilimbidi afe kifo cha aibu kama hicho ili sisi tupone!.
Lakini swali ni je! Wale wanaoamini kuwa Bwana Yesu alisulubiwa katika Nguzo ya wima, je hawataokolewa ikiwa wameshika na kuzitenda kanuni nyingine za imani?
Jibu ni la!.. Mtu akiamini kuwa Bwana Yesu alisulubiwa katika mti uliokuwa wima, au katika Miti miwili iliyokatana kwa mfano wa alama ya kujumlisha.. haimwongezei chochote wala haimpunguzii chochote katika vigezo vyake vya kuokolewa… Suala la msingi ni kuamini kuwa Yesu aliteswa na kusulubiwa kwaajili yetu, na akazikwa na kufufuka na akapaa mbinguni, na siku ya mwisho atarudi tena kutuchukua, hivyo tutubu na kuacha dhambi, lakini Mambo mengine hayana msingi sisi kuyajua…
Aina ya mti Bwana aliosulubiwa nao kama ni mshita, au mkoko hauna maana yoyote sisi kujua… vile vile na urefu wa mti au maumbile yake hivyo havitusaidii chochote wala havituongezei kitu katika vigezo vya kuokolewa, kama tu vile sura ya Bwana isivyoweza kutuongezea kitu kwa wakati huu (kwani hakuna anayeijua sura yake lakini bado wokovu tunapata) vivyo hivyo na maumbile ya msalaba hayatuongezei chochote, bali kuzaliwa mara ya pili.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?
UTHAMINI WITO WA PILI WA YESU ZAIDI YA ULE WA KWANZA.
BASI MUNGU ALIMWADHIMISHA MNO.JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?
NI NANI ATAKAYEUCHUKUA MSALABA WA YESU?
Wapelelezi wa uhuru wa wakristo ni watu gani (Wagalatia 2:4)?
Rudi nyumbani
Print this post