Boazi na Ruthu.
Atukuzwe Yesu Kristo Bwana wetu na mwokozi wetu, Nakukaribisha tuzidi kuzitafakari siri za ufalme wa mbinguni.
Awali ya yote tukumbuke kuwa mahusiano ambayo Yesu anayatengeneza kwa kila mwaminio sio mahusiano kama ya rafiki na rafiki, au ndugu na ndugu, hapana, bali kama ya Bwana-arusi na Bibi-arusi.
Ni vema hilo ukalifahamu mapema, kwasababu kitakachotufanya tuende mbinguni, ni Ndoa, na sio urafiki. Hivyo yeye kama Mfalme ndio Bwana-arusi, na sisi ni Bibi-arusi wake. Tunapojiunganisha naye, ni lazima tuonyeshe tabia za bibi-arusi wa kweli, vinginevyo hatutapata kibali cha kuwepo katika karamu ya Arusi yake, atakayoifanya mbinguni kwa wateule wake kwa tukio linalojulikana kama Unyakuo.
Mimi na wewe hatua budi kuhakikisha tunakuwa bibi-arusi safi wa Kristo, na sio masuria, ili tupate kibali cha kukubaliwa na yeye siku ile ya mwisho.
Leo wa neema za Bwana, tutajifunza kwa kupitia maisha ya Boazi na Ruthu. Kumbuka hadithi zote unazozisoma katika biblia zina ufunuo wa Kristo na kanisa lake. Hivyo usomapo hakikisha unamwomba Roho Mtakatifu akufunulie, ili biblia kwako isiwe kama vitabu vingine vya hadithi.
Sasa kama wewe ni mwanafunzi wa Biblia utakuwa umeshawahi isoma habari ya Ruthu. (Kama hujasoma nashauri ukakisome kwanza hicho kitabu, ndipo utaelewa vema, kiini cha somo hili, kwasababu hatutakichambua chote).
Utakumbuka, Boazi alikuwa ni shemeji wa yule mwanamke mjane aliyeitwa Naomi. Biblia inasema Boazi alikuwa ni tajiri sana, na mkuu katika mji ule. Lakini huyu Naomi alikuwa pia na mkwe wake aliyeitwa Ruthu.
Ruthu naye alikuwa mjane, kwani alifiwa na mume wake kabla hajapata mtoto. Hivyo wote wawili walikuwa ni wajane yaani Naomi na Ruthu, isipokuwa Ruthu alikuwa bado ni kijana aliyekidhi vigezo vya kuoelewa tena, lakini Naomi alikuwa ameshakuwa mkongwe hawezi kuolewa tena.
Lakini siku moja Naomi, akaona si vema mkwe wake Ruthu abakie kama yeye. Akaanda mazingira ya kumpatia mkwe wake mume mwingine, ndipo akachunguza na kuona kuwa Boazi ndiye amfaaye. Hivyo akaunda mpango aliokuwa na uzoefu nao, akamfundisha Ruthu namna ya kumwingia, na kwa kupitia njia ile basi Ruthu atapata kibali, kwa mtu huyu tajiri na mkuu wa mahali pale.
Embu tuutazame mpango wenyewe, tunaousoma katika ile sura ya 3, kisha tuone kanuni na sisi ya kukubaliwa na Kristo.
Ruthu 3:1 “Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema? 2 Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani.
3 Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa.
4 Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya.
5 Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya.
6 Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza”
Ukichunguza hapo utaona, Ruthu anapewa hatua tano za kupitia.
Naomi alijua uchafu, haupatani na bibi-arusi yoyote. Hakuna mume anayependa mwanamke mchafu, ni sharti awe msafi tena kwelikweli. Ndipo hapo sasa utaona akamwambia Ruthu akaoge kwanza awe safi. Ikifunua kuwa mkristo yoyote kabla ya kukubaliwa na Kristo, ni sharti kwanza awe safi kwa maji, yaani Ubatizo, ambao unaleta ondoleo la dhambi zake. Kama hujabatizwa, ni sharti ubatizwe katika maji ya kuzama, na kwa jina la Yesu Kristo, ili dhambi zako ziondolewe, Ndipo ukidhi hatua ya pili ya kumkaribia Kristo.
Kuoga tu peke yake haikutosha aliambiwa pia ajipake mafuta, Ikifunua kuwa Mkristo yoyote ni lazima awe na mafuta rohoni mwake. Na mafuta hayo ni Roho Mtakatifu. Ukikosa Roho Mtakatifu kamwe huwezi kukubaliwa na Kristo.
Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”
Ruthu alikuwa na mavazi yake ya kawaida, lakini hapa Naomi anampa shauri avae mavazi mengine yanayofanana na ya bibi-arusi, meupe safi, aonekane tofauti na wanawake wengine, apendeze, avutie machoni pa Boazi atakapoenda kujionyesha kwake.
Maana yake ni kuwa kila mkristo lazima awe na vazi la arusi, na vazi lenyewe ni Utakatifu. Kama tunavyosoma katika Ufunuo 19:8.Ukipoteza utakatifu, kamwe Kristo hawezi kukupokea, haijalishi utasema nimeokoka.
Ugani ni mahali wanapopepeta nafaka, Hivyo Boazi alikuwa ni mtu wa kazi, muda wote utamkuta yupo kazini kwake, si mtu aliyekuwa mlegevu, Ukitaka kumpata sharti na wewe pia uingie ugani kwake. Hivyo Ruthu ilimpasa aende vilevile, lakini alipewa maagizo kwamba iwe kwa siri, asijulikane na mtu yoyote yule.
Ikifunua kuwa, pamoja na kwamba, utakuwa umeokoka, huna budi kujishughulisha na kazi ya Bwana. Na wewe pia uwepo shambani mwake, lakini ukiwa na vazi lako la thamani(yaani Utakatifu). Na wakati uwapo huihitaji, kutenda kazi yake kama mtu wa mshahara bali kama mtumwa asiyekuwa na faida, uhakikishe upo kama mtu asiyetambulika na Kristo. Unatumika ndipo baadaye yeye mwenyewe aone vema kujifunua kwako.
Luka 17:5 Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani.
6 Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.
7 Lakini, ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng’ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula?
8 Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa?
9 Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? 10 Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya
Na hatua ya mwisho aliyopewa Ruthu na Naomi ni kujilaza miguuni pa Boazi. Maana yake ni kujivika unyenyekevu, Unakubali kulala kwenye miguu yenye mavumbi ya Bwana wako. unathamini cha Bwana ambacho kinadharauliwa, unathamini watu wa Mungu, .. Hapo ndipo pawe makazi yako daima, penye unyenyekevu.
Hivyo baada ya kutimiza, hatua zote hizo 5, yaani kuoga, kujipaka mafuta, kuvaa vazi la bibia-arusi, kudumu ugani na kulala chini ya miguu ya Yesu. Fahamu kuwa Kristo atajidhihirisha kwako, kama Boazi wa Ruthu.
Kumbuka maagizo hayo yote, Ruthu hakujiamulia tu, bali aliyapokea, kwa mkwe wake mzoefu aliyeitwa Naomi. Na sisi Naomi wetu ni Mitume na Manabii, yaani Biblia Takatifu. Tukiipenda, kuyashika yaliyoandikwa mule, basi tutakuwa bibi-arusi wa Kristo kwelikweli. Mtume Paulo aliandika hivi;
2Wakorintho 11:2 “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.
3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo”.
Zingatia: Kama wewe si bibi-arusi, huwezi kwenda kwenye Unyakuo. Hizi ni siku za mwisho, wakati wowote Yesu anarudi, Je! umejiandaaje? Utajibu nini siku ile, utakapoulizwa kwanini hukuitii injili? Wakati ni mchache sana tunaishi katika dakika za nyongeza tu, Tengeneza maisha yako sasa, huu sio wakati wa kuhubiriwa injili ya kubembelezwa, ni wewe mwenyewe uone uhalisia utubu. Yesu yupo mlangoni.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:
ALIPO NA ATAKAPOKUWEPO BIBI-ARUSI WA YESU KRISTO.
INAYOENDELEA SASA NI HUDUMA YA RUTHU.
EWE MKE! HESHIMA YAKO IPO KWA WAKWE ZAKO.
About the author