Mhubiri 10:20 Usimlaani mfalme, la, hata katika wazo lako; Wala usiwalaani wakwasi chumbani mwako; Kwa kuwa ndege wa anga ataichukua sauti, Na mwenye mabawa ataitoa habari
JIBU: Ni vema kutambua kuwa aliyeandika habari hii alikuwa ni mfalme, hivyo alitambua vema alichokiandika, na kwa hekima ya Ki-Mungu akazinakili ili ziwe onyo na angalizo kwetu . Ni wazi kuwa aliwahi kukutana na taarifa nyingi za uasi zilizowahi kupangwa kinyume chake kwa siri, au maneno ya unafiki, au ya dhihaka zilizosemwa kwa siri kinyume chake. Na yote hayo yakamfikia kwa haraka sana, kinyume na matarajio ya wale waliyoyapanga. Na huwenda wakawa wanabakiwa na maswali mengi, ni nani anayetoboa siri zao?.Wakakosa majibu
Sasa ni kwanini iwe hivyo?
Ni kwasababu Utawala wowote wa wakuu, unaundwa pia na ulinzi wake maalumu, (unaojulikana na ule wa siri usiojulikana). Kiasi kwamba chochote utakachokipanga kinyume chake kwa siri , tambua tu kitamfikia. Ndio maana hapo anasema usiwalaani katika wazo, au katika chumba chako cha siri.. Akiwa na maana hata wazo lako usiliruhusu kufanya hivyo, kwasababu mtu anayanena yaujazayo moyo wake. Kabla uasi haujatokea nje, unaanzia kwanza rohoni.
Halikadhalika wakwasi wanaozungumziwa hapo, ni watumishi wa wafalme, aidha mawaziri, au maakida, au maliwali ambao kikawaida huwa ni matajiri, vivyo hivyo na wao usijaribu kufanya hivyo ukidhani taarifa hazitawafikia. Zitawafikia, Mhubiri anatumia mfano wa ndege anasema.. ‘Kwa kuwa ndege wa anga ataichukua sauti, Na mwenye mabawa ataitoa habari’. Yaani kwa jinsi ndege wanavyoweza kusafiri kwa haraka, sehemu moja hadi nyingine, kwa wepesi wao na safari yao ya anga isivyo na vikwazo, ndivyo watu usiowajua watakavyoifikisha habari kwa wakuu wao, kinyume na matazamio yako.
Ndivyo ilivyokuwa kipindi cha mfalme Ahasuero, kulitoka watu wawili waliopanga mikakati kwa siri kumuua, lakini taarifa zilimfikia haraka mfalme kwa kinywa cha Mordakai mlinzi wa mlangoni, na wale watu wakagundulikana wakauliwa mara moja. (Esta 2:21-23)
Hakuna jambo lolote la siri ambalo halitajulikana kwa wakuu.
Tunaye Mfalme wa Wafalme, YESU KRISTO ambaye ndiye anayepaswa kuogopwa na watu wote ulimwenguni. Na kwamba hatupaswi kufanya jambo lolote kinafki, au kwa-siri mbele zake, linalokinzana na ufalme wake duniani. Kwasababu yote yatakuja kufichuliwa na kuwekwa wazi siku ile ya mwisho ya hukumu.
Yeye mwenyewe alisema;
Luka 12:2 “Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. 3 Basi, yo yote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari”
Hivyo uonapo kazi ya Mungu ya kweli inatendeka, kuwa makini sana na kinywa chako, uyapinge hata hayo mawazo yanayotaka kukwambia utukane, au ukufuru, au upinge. Vilevile wewe kama mhudumu wa kazi ya Bwana, tumika kwa uaminifu na kwa hofu ukijua kabisa mambo yako yote yanaonekana wazi mbele za Mungu, hakuna maficho.
Tuwe makini sana na ufalme wa Yesu Kristo duniani.
Je! Upo ndani ya Kristo? Je! Unatambua kuwa hizi ni nyakati za hatari, Yesu yupo mlangoni sana kurudi kulichukua kanisa lake? Unaishi maisha ya namna gani, ukifa leo huko uendako utakuwa mgeni wa nani? Embu tubu dhambi zako mgeukie Bwana akutakase, umtumikie yeye katika kipindi hichi kifupi tulichobakiwa nacho, itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima kisha ukapata hasara ya nafsi yako?. Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo, Basi fungua hapa kwa mwongozo wa sala hiyo ya toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
YESU NI MFALME WA AINA GANI KWAKO?
Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?
BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?
Uasherati wa Kiroho maana yake nini?
About the author