SWALI: Nimesikia hili neni Rhema, likitajwa sana Kwa watumishi na sehemu mbalimbali, naomba nifahamishwe maana yake Nini, mbona silioni kwenye biblia?
JIBU: Ni vema kutambua kuwa Biblia, katika eneo la agano jipya sehemu kubwa imeandikwa kwa lugha ya kiyunani. Hivyo Kuna baadhi ya maandishi ambayo tukiyasoma katika lugha nyingine mfano kwenye yetu hii ya kiswahili, tunaweza kuona yalimaanisha jambo lile lile moja lakini tukirudi kwenye lugha ya asili ya kiyunani yalimaanisha maana zaidi ya Moja.
Kwamfano, tunapokutana na hili Neno “NENO”. kwenye tafsiri yetu ya kiswahili, Mahali pote limeandikwa hivyo hivyo tu “Neno” likimaanisha Neno la Mungu.
Lakini tukirudi kwenye lugha ya asili ya kiyunani zipo sehemu limelitajwa kama “Logos”na sehemu nyingine kama “Rhema”
Logos ikiwa na maana Neno la Mungu la Daima/ wazo la Mungu/mpango wa Mungu ulioandikwa na pia kama Yesu Kristo mwenyewe, ambaye ndio Neno lililofanyika mwili.
Lakini ‘Rhema’: maana yake ni “Neno lililosemwa na Mungu” . Ni neno la wakati husika, sio la daima.
Mfano wa maandiko yanayolitaja Neno kama Logos ni haya: Yohana 1:1-18, Yakobo 1:22, Waebrania 4:12. N.k
Na mfano wa maandiko yanayolitaja Neno la Mungu kama Rhema ni haya;
Mathayo 4:3-4
[3]Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. [4]Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Hapo Bwana aliposema, “ila Kwa Kila Neno litokalo katika kinywa Cha Bwana”..alimaanisha Neno lisemwalo na Bwana.. mfano wa Eliya alipomwambia yule mwanamke mjane, Bwana asema hivi; “lile pipa la unga halitapinguka, Wala Ile chupa ya mafuta haitaisha”. (1Wafalme 17:14). Halikuwa Neno ambalo lilitumika Kwa wakati wote, ambalo hata sasa tunaweza litumia sisi, Bali la wakati ule ule tu, amefunuliwa, akalisema na ikiwa hivyo.
Lakini ‘Rhema’ ni yaliyonenwa Kwa wakati huo tu..tofauti ya Yale yaliyokuwa Daima.
Neno lingine ambalo linasomeka kama Rhema katika biblia,. Ni wakati ule mitume wamehangaika usiku kucha kutafuta samaki, lakini kulipokucha Yesu akawaambia watweke.mpaka vilindini wakavue. Petro akasema maneno haya;
Luka 5:5
[5]Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.
Aliliamini Neno lililosemwa na Bwana (na ikiwa vile).
Ili kuelewa vizuri tunaweza kusema “logos” ni BIBLIA TAKATIFU, na Rhema’ ni Neno mtu analofunuliwa Kwa kipindi Fulani.
JE! MUNGU ANASEMA NA SISI HATA SASA KAMA RHEMA?
Ni kweli Mungu ameshatupa njia yake kuu ya kusema na sisi, ambayo ni Kwa kupitia Biblia. Lakini pia bado Mungu anasema nasi, na kutushushia Neno lake Kwa wakati husikia litufae.
Tuwapo katika kanisa. Mungu hutumia karama mbalimbali, kusema nasi, au kutupa ujumbe wake. Anasema kutumia unabii au fundisho, au Neno la hekima, au maono, au ndoto, kutuwasilishia Neno lake.
Lakini pia ni lazima tujue kuwa Neno hilo lililofunuliwa ni sharti lisikinzane na Neno lake lililoandikwa. Vyote viwili vikichanganyikana huleta matokeo makamilifu na kutufanya tumwone Mungu katika uhalisia wake zaidi katika maisha yetu, kwasababu yeye Yu hai.
Lakini ipo hatari kubwa sana. Kwani katika siku hizi za mwisho wapo baadhi ya watu wanalichukua Neno liliokuwa kama Rhema, na kulifanya logos yao. Ndio hapo wanaposoma Bwana Yesu alitema mate chini akachanganya na udongo, akampaka mtu machoni akaona, hivyo na wenyewe wanafanya hivyo Kwa kisingizio kuwa andiko limeruhusu. Au wanapomsoma mtume Paulo anatoa leso yake, Kisha watu wanapona kupitia Ile, na wenyewe wanafanya hivyo hivyo, wakisema andiko limeruhusu. Hawajui kuwa ulikuwa ni ufunuo wa wakati ule ambao si agizo kuu, ni Rhema’.
Na madhara ya jambo hili ndio linageuka kuwa ibada ya sanamu. Tunayo mifano kadhaa katika biblia ya watu ambao waligeuza Rhema kuwa Logos, ikawapelekea kuingia katika laana. Kipindi Wana wa Israeli wakiwa jangwani, walipomkosea Mungu alimwagiza Musa aunde nyoka wa shaba, ili Kila amtazamaye apone. Na kweli ilikuwa vile. Lakini baada ya pale haikuwa sheria mama kama vile torati, kana kwamba waendelee kufanya vile. lakini tunaona baadhi ya watu walikuja kuifanya kama ndio sehemu Yao ya ibada ya uponyaji Kwa Mungu,.mpaka Mungu akachukizwa ikawapelekea kupelekwa tena utumwani Babeli, ikiwa kama mojawapo ya sababu.(2Wafalme 18:4)
Agizo letu la wakati wote ni JINA LA YESU TU! ndio logos yetu Bwana aliyotuagiza tutumie, wakati wote. Ikiwa hujafunuliwa kutumia kisaidizi/kiambatanishi kingine basi usifanye kwani huyo sio Mungu nyuma yake. Tegemea Biblia zaidi.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?
UUNGU NI NINI? (1Petro 1:3-4)
Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?
NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.
Miimo ni nini na kizingiti ni nini?
Maziara ni nini? Je! Na Tunaruhusiwa kuyajenga kwenye makaburi yetu?
Maswali na Majibu
Rudi nyumbani
Print this post