Swali: Je sisi watu wa agano jipya ni lazima kuwa na vipindi vya kuombea mlimani?. Na je huko mlimani Mungu ndioko anakosikia Zaidi maombi kuliko chini?.. msaada!
Jibu: Hakuna agizo lolote katika biblia la mahali rasmi pa kuombea!, kama ni mlimani au kama ni chini.. Lakini tunaweza kujifunza kupitia watu kadhaa katika biblia jinsi walivyoomba na kisha tunaweza kujifunga kitu.
BWANA YESU MWENYEWE.
Mathayo 14:22 “ Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.
23 Naye alipokwisha kuwaaga makutano, ALIPANDA MLIMANI FARAGHANI, KWENDA KUOMBA. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake”.
Na pia…
Luka 6:12 “Ikawa siku zile aliondoka AKAENDA MLIMANI ILI KUOMBA, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu”.
Soma pia Marko 6:46 na Yohana 6:15, utaona jambo hilo hilo la Bwana kupanda mlimani kuomba, na pia utaona sehemu nyingine alipanda na wanafunzi wake, soma Luka 9:28.
Umeona?.. Kama Bwana Yesu kuna nyakati alikuwa akienda mlimani kuomba, yeye pamoja na wanafunzi wake maana yake si bure!.. Kuna kitu cha ziada katika milima.
Na kitu hiko si kingine Zaidi ya UWEPO WA MUNGU. Milimani kunakuwa na Uwepo wa Mungu zaidi ya mabondeni?. Na kwanini milimani kunakuwa na Uwepo wa Mungu Zaidi ya sehemu nyingine nyingi?.
Ni kwasababu kule juu kunakuwa na utulivu,.. na siku zote utulivu unavuta uwepo wa Mungu, na milimani ni sehemu ambazo hazina usumbufu hivyo ni rahisi mtu kuzama katika roho kuliko akiwa chini penye masumbufu mengi na mwingiliano wa Sauti nyingi.
Umewahi kujiuliza ni kwanini minara ya simu huwa inapelekwa juu katika milima na haiwekwi mabondeni?.. Ni kwasababu kule juu network inapatikana vizuri Zaidi ya chini, kwasababu hakuna vizuizi vingi vya kuzuia mawimbi kusafiri. Sasa kama wanadamu wameiona hiyo siri iliyopo juu ya milima, vipi kwetu sisi wakristo?
Si kwamba Mungu hatakusikia ukiomba mabondeni, atakausikia lakini ule uwepo wa Mungu kwako unaweza usiupate vizuri kuliko kama ungeenda kuomba sehemu iliyoinuka (Milimani). Ndio maana utaona mtu anakuwa mzito kuomba, pasipo kujua chanzo ni nini?.. Wakati mwingine si mapepo!, bali ni mazingira tu!… Badili mazingira na utaona jinsi utakavyozama katika roho na maombi!.
Kwahiyo kama wakristo ambao pia ni mwanafunzi wa biblia, ni lazima tuwe na vipindi vya kupanda mlimani kuomba!. Kama mahali ulipo hapana milima, basi linaweza lisiwe jambo la lazima sana, lakini kama ipo basi tenga muda wa kufanya hivyo mara chache chache na utaona matokeo makubwa sana na vile vile utaona utofauti na utafungua mlango mpana sana wa kupokea mafunuo kutoka kwa Baba.
Bwana akubariki.
Marana tha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?
UTAONA MAMBO MAKUBWA KULIKO HAYA.
About the author