Kwanini Bwana Yesu aikabidhi roho yake mikononi mwa Baba (Luka 23:46)?

Kwanini Bwana Yesu aikabidhi roho yake mikononi mwa Baba (Luka 23:46)?

Jibu: Tusome kuanzia mstari wa 43..

Luka 23:44  “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,

45  jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.

46  Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU.

47  Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki”.

“Mikononi mwako naiweka roho yangu”… haya yalikuwa ni maneno ya Mwisho ya Mwokozi wetu Yesu Kristo alipokuwa pale msalabani?.. lakini swali? Ni kwanini aseme hivyo? Je kulikuwa na ulazima wowote  wa yeye kusema vile, na sisi je tunafundishwa kusema maneno kama hayo tunapokaribia hatua za kumalizia safari zetu za maisha?

Kabla ya kujibu, ni muhimu kufahamu kuwa kabla ya Bwana Yesu kufa na kushuka kuzimu na kupewa zile funguo za Mauti, sehemu ya wafu haikuwa salama (maana yake roho za watatakatifu bado hazikuwa salama hata baada ya kufa).

Ndio maana utaona hata Nabii Samweli ambaye alikuwa ni mtu wa haki sana mbele za Mungu, lakini baada ya kufa kwake, yule mwanamke wa Endori aliyekuwa mganga aliweza kumtoa kuzimu na kumpandisha juu kichawi.

1Samweli 28:7 “Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. 

8 Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako. 

9 Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?

10 Naye Sauli akamwapia kwa Bwana, akasema, Aishivyo Bwana, haitakupata adhabu yo yote kwa jambo hili. 

11 Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? NAYE AKASEMA, NIPANDISHIE SAMWELI”.

Umeona hapa? roho ya nabii Samweli inataabishwa na wachawi hata baada ya kufa kwake.. Ndio maana utaona Samweli baada ya kupandishwa juu alimlalamikia Sauli kwanini anamtaabisha.

1Samweli 28:15 “Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu?….”

Kwasababu hiyo ndio maana Bwana Yesu akaikabidhi roho yake kwa Baba, kama tu alivyokuwa anazikabidhi kazi zake na safari zake kwa Baba kipindi akiwa hai, vivyo hivyo alifahamu kuwa kuna umuhimu wa kufanya hivyo pia kwaajili ya roho yake baada ya kufa.

Lakini tunaona alipokufa, Baba alimpa funguo za KUZIMU na MAUTI sawasawa na Ufunuo 1:17

Ufunuo 1:17 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,

18  na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU”

Maana yake kuwa kuanzia wakati wake mpaka mwisho wa dunia, shetani hatakuwa na uwezo tena wa kuzitaabisha roho za watakatifu waliokufa, hivyo Bwana Yesu sasa ndiye mwenye mamlaka hayo juu ya roho zote za waliokufa na walio hai.

Warumi 14:8 “Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana.

9 Maana Kristo alikufa akawa hai tena KWA SABABU HII, AWAMILIKI WALIOKUFA NA WALIO HAI PIA”.

Kwahiyo kwasasa hatuna hofu tena ya kwamba baada ya kifo roho zetu zitataabishwa, bali tukifa basi uhai wetu (roho zetu) zinafichwa mbali na adui. Na sehemu hiyo ya maficho ambayo shetani hawezi kuifikia ni Paradiso, mahali pa mangojeo na raha, huku tukiingoja ile siku ya ahadi, ya unyakuo wa kwenda mbinguni. Haleluya!.

Kwahiyo kwasasa hatuna maombi ya kuzikabidhi roho zetu kwa baba wakati wa kufa, kwasababu tayari Kristo anazo funguo za mauti na kuzimu, bali tunapaswa wakati huu sasa tulio hai tuyakabidhi maisha yetu kwake, na kuishi maisha ya kumpendeza,  ili tutakapomaliza safari ya maisha yetu basi tujikute tupo sehemu salama, kwasababu hatujui ni saa ipi tutaimaliza safari yetu ya maisha hapa duniani.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

JIWE LILILO HAI.

ORODHA YA IMANI POTOFU- Sehemu ya 1.

Je Lutu alikwenda kuwahukumu watu wa Sodoma na Gomora? Kulingana na Mwanzo 19:9?

Kwanini Bwana Yesu alisema pale msalabani naona kiu?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments