Huu ni mwendelezo wa Mafundisho maalumu yawahusuyo wanawake.
Mwanamke aliyepoteza shilingi moja.
Luka 15:8 Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? 9 Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.
Bwana Yesu alipenda kutumia mifano halisi ya kimaisha kutufundisha habari za rohoni. Kwamfano katika habari hiyo tunafahamu mfano huo ulikuwa analenga mambo ya ufalme wa mbinguni, jinsi Mungu anavyomthamini mtu wake mmoja aliyepotea katika dhambi, pindi atubupo na kurejea. Kwamba tendo hilo linamfanya yeye pamoja na malaika zake mbinguni kufurahi sana.
Lakini leo nataka tujifunze kuhusu mfano huo katika uhalisia wake wa kimaisha kama ulivyoandikwa. Kuna maswali lazima ujiulize kwanini amtaje mwanamke na sio mwanaume. Kisha aipoteze shilingi yake pale NYUMBANI kwake, na sio sehemu nyingine, labda barabarani au sokoni? Tofauti na mfano uliotangulia ambao unamzungumzia Yule mtu aliyepotelewa na kondoo mmoja akawaacha wale 99 akaenda kumtafuta Yule mmoja huko maporini.
Na hatua ambazo alitumia kuitafuta shilingi ile hadi kuipata, kuna funzo gani pia?.
Kumbuka kimaandiko aliyekabidhiwa nyumba aisimamie ni mwanamke, ndio maana biblia inasema,
Mithali 14:1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
Na hazina yake inapatikana humo, lakini pia ikipotea, basi hupotelea humo humo.
Tukisema nyumba hatumaanishi, gorofa, na sebule na jiko. Hapana, bali tunamaanisha wale waliomo mule. Hao ndio hazina yake hasaa.
Sasa katika mfano huo mwanamke huyu alikuwa na shilingi 10, labda tuseme hao ni watoto 10, au ndugu 10, lakini mmoja akapotea, huwenda akawa mtundu, au mwizi, au kibaka, au shoga, au jambazi n.k. Lakini Mwanamke huyu hakukata tamaa na kukaa chini na kusema, Ahh! Ninao hawa 9, wenye kujitambua na wenye nidhani. Embu ngoja niachane na Yule pasua kichwa mtukutu, mwenye kiburi, asinipe presha, nifarijiwe na hawa wanangu 9 wazuri. Hapana, bali alilazimika kufanya jambo ili kuhakikisha amempata na Yule.
Hivyo kama tunavyosoma, hakukaa tu hivi hivi, na kuzungumza. Bali alichukua hatua fulani, na hatua zenyewe ndio hizi tatu.
Hii ikiwa na maana gani? mpaka anafikia hatua ya kuwasha tamaa, maana yake ni kuwa chumba hicho kilikuwa na giza, hivyo asingeweza kuipata shilingi yake katika mazingira yale. Tafsiri yake ni nini? Alimkaribisha Kristo. Ambaye ndio Nuru ya ulimwengu katika nyumba yake.
Hivyo hatua ya kwanza katika kutatua tatizo lake, alimtambua Kristo kwenye nyumba yake. Na sasa Nuru ilipomulika ndipo akatambua kuwa nyumba ilikuwa chafu. Kama asingewasha taa, kamwe asingeweza kugundua kuwa Vitu havipo katika mpangalio wake. Hivyo ikampasa aanze kwanza kuifagia nyumba ile, aipangilie vizuri. Makombo yaliyodondoka sakafuni ayafagie, vikombe na vijiko vilivyokaa hoe hae, aviweke mahali pake, nguo ambazo hazijakunjwa aziweke kabatini, uwazi uwepo. Hakukimbilia kuitafuta shilingi yake katika hatua hiyo. alijua hawezi kuipata katika mazingira yale, machafu, imejificha sana.
Hivyo ikamchukua muda Fulani mrefu kuisafisha nyumba yake, mpaka hatimaye, pengine baada ya saa 6, ikawa safi. Kila kitu kikawa katika mpangilio wake.
Ndipo sasa akaenda katika hatua ya mwisho ya “kuitafuta kwa bidii ile shilingi”. Akaanza kupita eneo moja baada ya lingine, hakutoka nje ya nyumba kwenda kuitafuta barabarani, hapana bali pale pale ndani kwasababu alijua fedha zake hazijawahi kutoka nje ya nyumba.
Na hatimaye akaipata. Na mwisho wa siku akawaalika na marafiki zake, wakafurahi pamoja. Kwasababu ilimgharimu kuipata tena.
Hii ni kufunua nini?
Wanawake wengi wanapoona aidha ndugu zao nyumbani, au watoto wao, au ndoa zao zimeharibika,. Wengine wanakimbilia kwa waganga ili wasaidike, hapo umepotea, wengine wanakimbilia kwa washauri wa kijamii, bado hujapata suluhisho. Suluhisho pekee ni Nuru ya ulimwengu. Yesu Kristo, aimulikie kwanza nyumba yako.
Na Yesu anachokifanya ni kukuonyesha madhaifu uliyokuwa nayo, uchafu uliomo nyumbani mwako, ili urekebishe (ndio ufagie). Sasa wengine wanapofikia hatua hii, wanapoona wanahubiriwa waishi maisha ya utakatifu, wawe watu wa ibada majumbani mwao, wawe waombaji, wafungaji, wafukuze tabia zisiojenga majumbani mwao, waweke mipaka Fulani kwenye familia zao. Wanaona kama wanatwikwa mzigo juu ya mzigo. Wanamkimbia Kristo, wanabakia kulia tu, na kuhuzunika..
Wanachofikiria tu, ni utatuzi wa tatizo, mume aache pombe (aokoke), watoto wawe wasikivu, nyuma iwe na amani, n.k. lakini hawataki wao wenyewe kurekebisha baadhi ya mambo makwao. Hapo ndugu ukikwepa hatua hii, sahau kukipata unachokitafuta. Hata upewe bahari nzima ya mafuta ya upako, na pipa la chumvi. Unapoteza muda, hutatui jambo lolote.
Kristo anataka usafi kwanza, ndipo akupe jicho la kuiona shilingi yako iliyopotea. Sasa ikiwa utatimiza mambo hayo mawili yaani KRISTO ndani yako, na usafi wako. Kinachofuata ni kutafuta ulichokipoteza.
Hii ndio hatua sasa ya kumuhubiria, kumshauri, kumwonya, kumvuta kwa Bwana. Sasa ukiendelea hivyo hivyo, muda si mwingi utampata kiwepesi sana haijalishi alikuwa amepotea kiasi gani, au alikuwa sugu namna gani. Hakuna linaloweza kujificha mbele ya Nuru. Tatizo lolote sugu unalolijua wewe la kifamilia, kwa kufuata kanuni hizo litatatulika tu.
Hivyo wewe kama mwanamke, itambue huduma hii iliyopewa na Bwana, laiti kama wanawake wote, wangekuwa ni wa kujiwajibisha kwa namna hii, jamii zetu na familia zetu zisingekuwa na migogoro mingi,wala injili isingekuwa ngumu sana kuihubiri kwasababu tayari walishatangulia walioweka misingi bora nyuma. Hii ni huduma kubwa sana kwa mwanamke na Bwana anaithamini sana.
Simama katika nafasi yako wewe kama mama, wewe kama Dada, nyumba au familia itasimama, endapo wewe utasimama.
Bwana akubariki
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mafundisho mengine:
MAFUNDISHO KWA WANAWAKE
MWANAMKE ABIGAILI ANAFUNZO GANI KWA WANAWAKE?
Je mwanamke Fibi, alikuwa ni askofu wa makanisa, kama mitume?
BADO TUTAHITAJI TU KUSAIDIANA.
Je Mungu anaketi katika giza? (1Wafalme 8:12)
MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)
Rudi nyumbani
Print this post