JINSI YA KUVURUGA MIPANGO YA MUNGU.

JINSI YA KUVURUGA MIPANGO YA MUNGU.

Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno ya uzima.

Kuna vitu ambavyo Mungu amepanga, vitokee kwa njia ya asili, na vingine amepanga vitokee ndani ya wakati wake alioukusudia.  Kwamfano ikiwa amekusudia baada ya miaka kumi ndio uone majibu ya lile hitaji ulilomwomba, yeye mwenyewe ataanza kukuandalia njia sasa, na hatimaye ule wakati ukifika basi atafungua njia ya kukipata.

Lakini vipi kama utakihitaji kwa majira haya ya sasa. Na wakati huo huo iwe ni mapenzi ya Mungu na sio yako. Je hilo linawezekana? Maana yake ni kuwa  uivuruge mipango yake ili afanye sasa hivi kile unachokihitaji. Je! Mungu anaruhusu tuwe watu wa namna hiyo?

Jibu ni ndio.

Na aliyetufundisha siri hiyo si mwingine zaidi ya Kiongozi wetu mkuu wa imani YESU KRISTO.

Embu tafakari haya maneno aliyoyasema.

Luka 18:1  Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. 2  Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3  Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 4  Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5  lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. 6  Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. 7  Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8  Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

Katika vifungu hivyo ni wazi kuwa Bwana anajifananisha na huyo kadhi, ambaye hakuwa tayari kumsaidia Yule mwanamke mjane haja yake kwa wakati ule.  Lakini kutokana na hatua alizozichukua Yule mwanamke ilimbidi tu ampe kama alivyotaka.

Na ndivyo ilivyo kwa Mungu wako. Upo wakati unaweza kupata kile unachokitaka kwa wakati wako, na si kwa wakati wa Mungu? Zipo kanuni ambazo ukizitumia, zitakusaidia kuuvuta msaada wa Mungu kwa haraka zaidi.

Kanuni ya kwanza: Ni kuomba bila kukata tamaa.

Maombi ya kung’ang’ana yanaugusa sana moyo wa Mungu, zaidi ya sisi tunavyoweza kufikiri. Kwa bahati mbaya ni pale tunapoona Mungu amekaa kimya tunadhani, hasikii. Yeye mwenyewe anasema aliyeumba sikio utasemaje hasikii?? Tangu lini?. Mungu huwa anasikia, lakini anasubiri umakini wako wa kile unachokililia kwake, Kama alivyofanya huyo mwanamke. Kiwango chako cha kutokata tamaa, hupelekea majibu ya haraka ya maombi yako. Ukiomba leo hujaona kitu, unaendelea hivyo hivyo kesho, ikiwa kesho haipo, unaendelea kesho kutwa..hivyo hivyo hata kama ni kwa miaka 5, hakuna kusema, Mungu hatendi, au amenisusa. Omba bila ukomo, tena huku ukiamini asilimia mia kuwa  Bwana analishughulikia ,Usibahatishe kuomba. Utapokea kinyume na wakati.

Kanuni ya pili: Kustahimili vipingamizi.

Vipingamizi vinaweza kutokea kwa wanadamu, na wakati mwingine hata katika Neno la Mungu. Kwa wanadamu ni kama vile kuvunjishwa tamaa. Na kuambiwa Mungu hayupo na wewe, au umemkosea Mungu. Hilo unaweza kukumbana nalo sana. Lakini vilevile, Mungu anaweza kukuuliza, unataka upokee hili kwa sifa ipi uliyonayo? Wewe utamjibuje? Hilo nalo utakumbana nalo moyoni mwako.

Embu fuatilia kisa hiki.

Mathayo 15:22  Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.

23  Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. 24  Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

25  Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. 26  Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. 27  Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.

28  Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

Huyu mwanamke, alihitaji wokovu ambao wakati wake ulikuwa bado kwa watu wa mataifa, kwasababu Yesu alikuwa bado hajasulibiwa. Hivyo alipojaribu tendo ambalo lilikuwa ni gumu masikioni mwa watu. Moja kwa moja alikutana na vipingamizi. Cha kwanza ni kutoka kwa mitume walipoona Bwana hamjibu lolote, wakaanza kutaka afukuzwe, kwasababu anasumbua watu. Anapiga-piga kelele ovyo, anawavunjia wayahudi heshima, mpagani huyu. Lakini yeye hakujali yale maneno.

Baada ya hapo  akakumbana na Bwana mwenyewe, ambaye hapo mwanzo alimtazama wala hakumjibu neno lolote. Kumbuka, tabia hiyo ya kutojibu watu hakuionyesha kwa huyu mwanamke tu, bali kwa watu wengine pia, lakini huyu tu habari yake ndio imerekodiwa kwasababu ya kitu alichokifanya. Na alipoambiwa habari za mbwa, hakusijikia vibaya, akawa na hoja hapo hapo za kutetea, kwamba hata mbwa wanapata yale masalio yaangukayo kutoka mezani mwa bwana zake. Na mwisho wa siku akapokea alichokihitaji kinyume na taratibu.

Vilevile na wewe unachomwomba Bwana, atakuuliza una vigezo gani vya kupokea hiki. Hezekia alikuwa na hoja za kumpa Bwana na hatimaye akaongezewa maisha kwa kuponywa ugonjwa wake. Na wewe pia jiandae kwa hoja nzito, na majibu yako kwa Bwana daima yawe ni haya “Bwana sistahili kupokea, lakini Kristo tayari alikufa kwa ajili yangu msalabani, kunistahilisha mbele zako  ndilo linalonipa ujasiri huu wa kupokea chochote mbele zako kwa imani sawasawa (Waebrania 4:16)”. Ukifanya hivyo jiandae kupokea unachokihitaji.

Kanuni ya tatu: Tenda jambo la ziada:

Tendo la ziada, huvuruga mipango mingi ya Mungu. Kwamfano usipende kumwendea Mungu vilevile kwa desturi na mazoea ya sikuzote. Onyesha uhodari Fulani kwa Mungu, onyesha imani Fulani kubwa kwa Mungu. Mara nyingi Yesu alikuwa anafuatwa na Jeshi kubwa la makutano na kila mmoja alikuwa anahitaji ahudumiwe. Lakini utagundua wapo waliowahi kuhudumiwa kwasababu ya imani yao, na matendo yao ya kipekee kwake.

Zakayo hakufuata mkumbo, alibuni njia yake akapanda juu ya mkuyu Bwana akamwona. Yule mwanamke aliyetokwa na damu, hakufuata mkumbo, aliamini nikigusa tu pindo la vazi la Yesu nitapona. Yesu akaghahiri mwendo wake ili amtafute. Wale vipofu wawili Yeriko, waliposikia Yesu anapita, walipaza sauti zao kwa nguvu, wakisema Yesu turehemu. Yesu akawaponya

Vivyo hivyo na wewe, fanya jambo la ziada kwa Mungu wako. Kama ni kumsifu basi msifu zaidi ya kawaida ya sikuzote, uone kama hatafanya jambo kwako la ajabu. Kama ni kumtolea Mungu Mtolee zaidi ya kile kipimo cha kawaida. Fanya jambo kuu. Jimalize kwa ajili ya Bwana kwa kitu Fulani,  Utaamsha moyo wa Mungu akuhudumie kwa haraka sana.

Kanuni ya nne: Pia kuwa mfungaji.

Esta, aliweza kuuvuruga utaratibu wa mfalme. Siku ambapo alipanga kumwendea bila kualikwa. Utaona kuwa alifuata kanuni ya kufunga pamoja na watu wake kwa siku tatu. Ndipo akamkabili mfalme. Na mfalme akatii jambo lile. Kwasababu ilikuwa ni kifo kumfuata mfalme kama hajakualika.

Vivyo hivyo na wewe umwombapo Mungu jambo fulani, hakikisha unaambatanisha mifungo. Kwasababu hiyo hukuongozea umakini wako mbele za Mungu.

Ikiwa utafuata utaratu huo, basi uwezekano wa kupokea mahitaji yako kinyume na njia za kawaida ni mkubwa sana. Uombapo katika eneo lolote liwe gumu au jepesi Bwana atakumulikia nuru zake.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.

KAZI ZA ROHO MTAKATIFU

KANUNI RAHISI YA KUPOKEA BARAKA MARA DUFU.

IJUE KANUNI YA KUREJESHA NGUVU ZA KIROHO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments