Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu,
Ni swali ambalo linaulizwa na wengi, je ni kweli mtu anaweza kuzishinda tamaa za mwili? Au vishawishi vyake? Anaweza kweli kuacha dhambi ya uzinzi, au kujichua,au kutazama picha za ngono, au ulevi, au miziki, n.k.?
Jibu la kibinadamu ni hapana! Na ndivyo ilivyo.. Lakini jibu la Mungu ni ndio, kwasababu alisema kwake yote yanawezakana.(Mathayo 19:26).
Akili yako itakuambia haiwezekani, kwasababu hujajua kanuni ya kuwezekana. Mimi niliwahi pia kufikiri hivyo hapo nyuma. Lakini nikathibitisha kile maandiko yanasema, kuwa hilo jambo linawezakana, Mungu hasemi uongo. Sasa utauliza ni kwa namna gani?
Awali ya yote ni vema ukafahamu kuwa hakuna mwanadamu yoyote aliyeumbwa na uwezo wa kuzishinda tamaa za mwili. Hayupo. Vilevile anayejaribu kufanya hivyo kwa akili zake, na kwa nguvu zake peke yake, pia anajidanganya mwenyewe kwasababu, utafika wakati atayarudia yaleyale tu. Ikiwa wewe ni mmojawapo unayejaribu kupambana kwa nguvu zako, utavunjika moyo ni heri leo ujue kanuni sahihi ya kuitumia.
Kanuni imetolewa kwenye mistari huu.
Wagalatia 5:16 BASI NASEMA, ENENDENI KWA ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
Anasema “Enendeni kwa Roho”, biblia ya kiingereza inatumia neno “Walk in spirit” akiwa na maana “Tembeeni katika Roho”
Wakristo wengi, wanampokea kweli Roho Mtakatifu, wanajazwa Roho kabisa, lakini ni wachache sana “wanaotembea katika Roho Mtakatifu”.
Ni sawa, na mgeni unayemkaribisha nyumbani mwako. Halafu unapokwenda kazini, au matembezini unamwacha nyumbani, hajui kingine chochote kuhusu wewe zaidi ya maisha ya palepale unayokutana naye nyumbani. Ndivyo anavyofanywa Roho Mtakatifu na waamini wengi.
Tunamtambua Roho tu, pale tunapokuwa ibadani, lakini maisha nje ya ibada, sisi ni watu wengine kabisa. Na hapo ndipo linapokuja tatizo kwanini vishawishi na tamaa zinatushinda. Kwasababu hatutembei na Roho Mtakatifu.
Ukweli ni kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayekusaidia wewe kuua nguvu ya tamaa ndani yako. Na hivyo anahitaji uwepo wake uwe nawe wakati wote, ili hilo liwezekane. Ni sawa na GANZI, anayopigwa mgonjwa, wakati ganzi, ipo mwilini hawezi kusikia maumivu, lakini inapoisha maumivu yanamrudia kwa kasi, hivyo anahitaji kuongezewa ganzi nyingine, ili aendelee tena kukaa bila maumivu.
Ndivyo alivyo Roho Mtakatifu, huna budi kufahamu ni namna gani atakupiga ganzi, ili uweze kuishi maisha ya ushindi hapa duniani. Na kanuni si nyingine zaidi ya Kuenenda katika Roho. Kuanzia leo acha kupambana na hizo tamaa kivyako, hutazishinda, pambania kujawa na Roho lakini pia kutembea naye maishani mwako.
Kwa kuzingatia mambo makuu matatu.
1). KWA KUWA WAOMBAJI WA DAIMA:
Watu wengi wanapofikiria maombi akili zao zinakwenda moja kwa moja kudhani ni wasaa kwa kuwasilisha mahitaji yao. Lakini maombi si mahali tu pa mahitaji, bali ni mahali pa kujazwa Roho. Hivyo kama mtoto wa Mungu uingiapo kwenye maombi yako kila siku tumia nafasi ya kuomba ujazwe Roho Mtakatifu, akuongoze, akupe nguvu, akujenge nafsi yako, uimarike. Hivyo yakupasa uingie katika maombi ya ndani kabisa sio juu juu ya kutimiza ratiba, bali ya kuweka mawazo yako yote kwa Roho Mtakatifu, akujawe ndani yako, hili ni muhimu sana, kwasababu yeye ndio atakayekusaidia.
Sasa kwa jinsi unavyoomba kwa muda mrefu, na kwa mara kwa mara, ndivyo unavyozidi kumpa nafasi Roho wa Mungu kukujaza nguvu, na mwisho unaona vitu kama tamaa ni vidogo sana, kwasababu ganzi imeshaingia vya kutosha ndani yako.
Jambo hili linatakiwa liwe ni la kila siku(Waefeso 6:18). Kama wewe sio mwombaji, kiwango cha Roho kitakuwa kidogo ndani yako, mwili utakulemea tu, haijalishi upo kwenye wokovu kwa miaka 50, utasumbuliwa tu na tabia za mwilini, Ndio maana tunasisitizwa tuombe kila wakati. Maombi ni kila wakati, kila saa, omba kwa akili, pia omba wa kunena kwa lugha kwa jinsi Bwana atakavyokujalia. Lakini elekeza mawazo yako katika kujazwa na yeye, ukiwa ni mwombaji wa wiki mara moja uendapo kanisani jumapili, au mwezi mara moja, hapo unapoteza muda, hutembei katika Roho. Uthibitisho wa anayetembea kwa Roho ni Yule ambaye ni mwombaji wa kila siku.
2) LIWEKE NENO LA MUNGU AKILINI MWAKO WAKATI WOTE.
Neno la Mungu, husisimua roho zetu wakati wote. Na adui anachohakikisha ni kutufanya sisi tulisahau, hivyo mambo mengine yatawale akili zetu. Anajua akili yako ikiwa inatafakari habari na maonyo katika biblia, itakaa mbali na njia mbovu.
Pale adui anapotaka kukujaribu ukifiria wema Mungu aliomtendea Yusufu, kwa kuukimbia uzinzi, anajua utapata nguvu, pale Mungu alipomtukuza Ayubu kwa kukaa mbali na maovu, utapata nguvu, jinsi Danieli alivyokuwa mwaminifu, Mungu akamwinua anajua utaendelea katika uaminifu wako . Hivyo hapendi, wewe utawaliwe na Neno kichwani, anataka utawaliwe, na movie, utawaliwe na mipira, utawaliwe na siasa, na mambo ya mitaani, basi. Akili yako izunguke hapo, lakini isizunguke kwenye BIBLIA.
Ukijizoesha kilizungusha Neno la Mungu, na ahadi za Mungu kichwani mwako. Tafsiri yake ni kuwa unamzungusha Roho Mtakatifu, katika ulimwengu wako wa maisha. Na ni nini atakachokifanya kwako kama sio kukusimua roho yako, kwa Neno lile. Hivyo unayashinda yote kirahisi. Watu hawajui Neno la Mungu ndio Roho Mtakatifu mwenyewe wanasema nao.
Yohana 6:63 Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; MANENO HAYO NILIYOWAAMBIA NI ROHO, TENA NI UZIMA.
Soma sana Neno, lakini zaidi, lidumu kichwani pako, kutwa nzima. Huu ni ulinzi kamili, na silaha madhubuti ya mambo yote ya mwilini.
3) FANYA MAAMUZI YA GEUKO LA KWELI.
Maamuzi ni kutii. Ukiwa mtu wa nia nia mbili, unataka kumfuata Yesu, na wakati huo huo hutaki ulimwengu ukuache nyuma. Hapo napo unamzuia Roho wa Mungu kufanya kazi yake vema ndani yako. Unaweza ukawa ni mwombaji kweli lakini kama moyoni mwako hujaamua kufanya maamuzi, bado ni kazi bure.
1Yohana 2:15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele
Ukiamua kumfuata Yesu, fahamu kuwa hii dunia sio fungu lako tena, anasa sio rafiki tena kwako. sio tu na ulimwengu lakini pia na nafsi yako.Ndipo hapo unachukua hatua za dhahiri kabisa katika imani yako, kama ulikuwa na vichocheo vyote vinavyokusababishia utende dhambi, ndio hapo Yesu anakuambia ukate, usione huruma kutupa hizo nguo za kizinzi ulizozoea kuzivaa, kuachana na huyo girlfriend, kuacha hizo muvi za kizinzi, unazoangalia, usione shida kuacha kampani zako za walevu, usijihurumie hata kidogo, huku ukiwa na mawazo kuwa unafanya hivyo kwasababu ya Kristo ndiye atakayekupa neema ya kushinda.
Ijapokuwa mwanzoni utaona shida kwasababu unafanya kimwili, kwa utiifu wako huo baadaye Roho wa Mungu atakunasa, kwasababu umempa umiliki wote wa maisha yako. Ganzi kubwa sana itaingia ndani yako,.
Ukizingatia mambo hayo matatu, kila siku katika maisha yako. Basi wewe unaenenda kwa Roho. Hakuna litakalokuwa gumu kwako. Kwasababu si kwa nguvu zako bali kwa nguvu za aliye ndani yako, unayashinda hayo.
Wagalatia 5:25 Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
NI JAMBO GANI LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?
About the author