Swali: Katika Luka 19:26, kwanini Bwana YESU aseme kila mwenye kitu atapewa na yule asiye na kitu atanyang’anywa?, na kwanini isiwe kinyume chake?..kwasababu hilo ni kama jambo la kikatili, kumnyang’anya mtu kile kidogo alicho nacho.
Jibu: Turejee mstari huo..
Luka 19:24 “Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.
25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.
26 Nawaambia, KILA ALIYE NA KITU ATAPEWA, BALI YULE ASIYE NA KITU ATANYANG’ANYWA HATA ALICHO NACHO”.
Ni kweli tukisoma kwa tafakari za kawaida (za kimwili) ni kama jambo la kikatili, kumpokonya mtu kile kidogo alichonacho, lakini mstari huo hauhusu mambo ya mwilini bali ya rohoni (kwamba maskini anyang’anywe kidogo alicho nacho na apewe tajiri..La! hiyo sio maana ya huo mstari).
Ili tuelewe vizuri, turejee ule mfano wa Mzabibu katika Yohana 15:1-2, Neno la Mungu linasema..
Yohana 15:1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
2 KILA TAWI NDANI YANGU LISILOZAA HULIONDOA; NA KILA TAWI LIZAALO HULISAFISHA, ILI LIZIDI KUZAA”.
Kwa wale wakulima wanaelewa lengo la kuondoa yale matawi yasiyozaa matunda ni nini?.
Kusudi au lengo la kuondoa yale matawi yasiyozaa na kubakisha yale yanayozaa peke yake katika shina la mti ni kudhibiti matumizi mabaya ya chakula yatokayo katika mizizi kulekeka katika matawi.
Chakula kitokacho ardhini, na kupanda katika matawi ya mti, kama matawi yale yapo kumi (10) na kati ya hayo manne (4) ndiyo yenye kuzaa na (6) yaliyosalia hayazai, ni kwamba kile chakula kitokacho kwenye mizizi na kuelekea kwenye matawi hayo, kitajigawanya kulingana na idadi ya matawi yaliyopo.. na hivyo yale matawi manne (4) yazaayo yatapokea chakula kidogo, na yale (6), yatapokea kingi.
Sasa matokeo yake ni kwamba yale matawi manne (4) yazaayo yatazaa kwa kiwango kidogo kwasababu ya kiasi kidogo cha chakula yapokeayo, na yale mengine sita yasiyozaa yatakuwa yanapokea chakula cha bure ambacho hakiyasaidii matawi hayo, hivyo uzalishaji wa ule mti UTAKUWA HAFIFU, endapo ukiendelea kubaki na yale matawi yasiyozaa.. (mti utaonekana una matawi mengi na mkubwa lakini matunda machache).
Sasa kutatua hilo tatizo wakulima, huwa wanayaondoa yale matawi yasiyozaa ili yasiendelee kutumia chakula cha bure, na matokeo ya kuyaondoa kwa kuyakata yale matawi yasiyozaa, na kubakisha yale yazaayo peke yake, ni kwamba kile chakula chote kitokacho ardhini hakitapotea bali kitaenda moja kwa moja kwa yale matawi yazaayo..
Na matokeo yake yale matawi yazaayo yatapokea virutubisho vingi na kusababisha kuzaa Zaidi..Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba uwepo wa matawi yasiyozaa katika shina ni uharibifu kwa yale matawi mengine yazaayo..
Na hiyo ndiyo sababu ya Bwana YESU kusema, “KILA ALIYE NA KITU ATAPEWA, BALI YULE ASIYE NA KITU ATANYANG’ANYWA HATA ALICHO NACHO”.. maana yake KILA TAWI LINALOZAA LITAONGEZEWA NGUVU NA LILE LISILOZAA HATA KILE KIDOGO LIPOKEACHO LITANYANG’ANYWA (LITAKATWA).
Mathayo 3:10 “Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni”.
Ikiwa umepata Neema ya kusikia injili lakini unaichezea, hutaki kuzaa matunda ya haki kuwa makini sana, kuna hatari mbele yako!!
Ikiwa umepata Neema ya kusikia Injili na hutaki kubadilika miaka nenda rudi, uko vile vile, kuwa makini!!
Luka 13:6 “Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.
7 Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?
8 Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;
9 nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate”.
Ikiwa umepewa Karama/huduma na hutaki kuitumia, ipo vile vile kuwa makini sana!!.. hiyo Neema itaondolewa kwako na kupewa mtu mwingine ambaye atazaa matunda.
Mathayo 25:24 “Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;
25 basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.
26 Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
28 Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
29 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa”.
Bwana akubariki, na Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
TAWI LIZAALO HULISAFISHA ILI LIZIDI KUZAA.
SHIKA SANA ULICHO NACHO, ASIJE MTU AKAITWAA TAJI YAKO.
UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?
Tofauti kati ya zaka na sadaka ni ipi?
About the author