Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno ya uzima.
Katika nyakati hizi za hatari na udanganyifu mwingi, ni vizuri kujichunguza sana, ni Roho ipi umeipokea ndani yako. Kwasababu tabia unazozionyesha ni matokeo ya roho iliyopo nyuma yake, ikiwa wewe ni mpenda dunia basi roho ya dunia ipo ndani yako.
1Wakorintho 2:12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.
Vivyo hivyo ukijiona wewe ni mwizi, ujue roho ya wizi ipo nyuma yako.
Lakini maandiko yanasemaje kuhusu Danieli?
Yanasema ROHO BORA ilikuwa ndani yake.
Danieli 6:3 Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote
Maana yake ni kuwa Roho iliyozidi viwango, ndio iliyokuwa ndani yake.. Unajua mpaka inasema bora, maana yake zipo ambazo hazina ubora, kwa tafsiri nyingine “feki”, zenye mfano wa ile orijino. Ndicho shetani anachokibuni sana, ili awapoteze watu, wadhani wanaye Roho Mtakatifu, kumbe ni bandia.
Sehemu nyingine, inasema “Roho njema kupita kiasi”. Ilikuwa ndani yake..
Danieli 5:12 kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danieli huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danieli, naye ataionyesha tafsiri.
Umeona sifa ya roho hiyo ni lazima iwe ya ‘kupita kiasi’, sio ya kawaida, vinginevyo ni feki. Sifa za Roho wa Mungu, anapita kiasi. Katika ubora na wema.
Ndio iliyomfanya Danieli awe mkamilifu kama tunavyomsoma kwenye maandiko. Kiasi cha watu kutafuta kosa ndani yake, bila mafanikio.
Danieli 6:4 Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.
Na mtu yeyote anayesema ameokoka, Roho hii naye ni lazima imkalie. Roho iliyo bora, na njema kupita kiasi. Uthibitisho wa kwanza wa Roho uliyempokea ni Roho Mtakatifu, atakusukuma, kuwa Mtakatifu kama jina lake lilivyo.
Lakini iweje tunasema, tumepokea Roho, tunanena kwa lugha usiku kucha, tunatabiri, lakini Ubora wa huyo Roho hauonekani ndani yetu? Cha kushangaza utaona huyo mtu anasema haiwezekani kuishi maisha matakatifu hapa duniani, ndio hapo tunamhubiri Kristo, wakati huo huo, tunaishi kidunia, tunafunga na kuomba wakati huo huo, tunavaa ovyo ovyo, tunaabudu pamoja lakini chini kwa chini tunavisasi na vinyongo. Tunatoa sadaka lakini nyuma kwenye biashara zetu ni za rushwa rushwa.
Je! Hiyo ni Roho bora? Au imechakachuliwa?. Tumepewa ruhusu ya kujipima (1Yohana 4:1). Jihakiki, tangu ulipookoka hadi leo je, kuna mabadiliko yoyote ndani yako? Kama huna ni aidha ulimzimisha alipokuwa anaugua ndani yako ugeuke, au huna kabisa Roho Mtakatifu.
Habari njema ni kuwa Roho bora, ukimwita, huja ndani yako, au huamka tena. Ni wewe kuamini, na kutii kwa moyo wako wote. Kuwa tayari kuacha vyote(vya kidunia), na kumgeukia yeye. Na hatimaye atakuongoza na kukuweka sawa. Lakini sharti kwanza uaminifu kuwa utakatifu unawezekana, lakini pia ulimwengu utaukana.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
VIASHIRIA VINGINE VYA ROHO MTAKATIFU KUWEPO NDANI YAKO.
About the author