IHUBIRI INJILI, KILA MAHALI KWASABABU AKUZAYE NI MUNGU.

IHUBIRI INJILI, KILA MAHALI KWASABABU AKUZAYE NI MUNGU.

Jina la Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe.

Upo umuhimu wa kuhubiri injili mahali popote na katika mazingira yoyote kwasababu ni agizo la Bwana mwenyewe (Mathayo 28:18-20).

Wapo wanaoamini kuwa injili ya mitaani na masokoni hazina faida yoyote kwasababu watu wanakuwa hawapo katika utulivu.

Na pia wapo wanaoamini kuwa injili  za kwenye mikutano au makanisani ndizo zilizo bora kwasababu watu wanakuwa katika utulivu.

Lakini nataka nikuambie Injili zote zina umuhimu, (Za watu walio katika utulivu na utayari wa kusikiliza na za ambao hawako katika utayari)... na Mitume wa Bwana YESU walihubiri zote (katika masinagogi na masokoni).

Matendo 17:17 “Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku”.

Na hata Bwana wetu YESU alifanya hivyo pia..

Luka 8:1 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye”

Lakini leo nataka nikupe umuhimu wa injili za mitaani (za watu wasio na utayari wa kusikia).

Kikawaida ni ngumu kumsimamisha mtu barabarani na kumwambia asimame asikilize… Wengi wanakuwa hawana utayari huo.

Lakini anapopita au anapokuwa ameketi na wewe kukaa mbali naye kidogo na kulazimisha asikie kile anachokisema pasipo hata ridhaa yake, kuna vitu vitaingia ndani yake hata kama hataki.

Kwani lile Neno atakalolisikia hata kama ni moja, litakuwa mbegu njema ndani yake ambayo itachupuka kwa wakati wake.

Kwahiyo ni heri kusikia hata hilo moja kuliko kutokusikia kabisa, kwasababu wengine hata kanisani hawaendi kabisa, wengine ni wa imani nyingine, hawajawahi na wala hawana mpango wa kwenda kanisani wala kusogea mahali penye mahubiri….na wengine wanaamini wapo sahihi katika njia zao, hivyo hawahitaji kusikia kingine chochote, wameridhika na kutosheka na wanavyovijua au walivyo navyo.

Hivyo ukisema uwasubiri, au uombe ridhaa ya kuzungumza nao, hawafungui huo mlango!…sasa kundi hili linasaidikaje?…je kwa kuliacha tu?…au kusubiri au kuliombea tu!…

Jibu: Linasaidika kwa kusikia kwa lazima!.

Ezekieli 2:7 “Nawe utawaambia maneno yangu, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana”

Umeona?..ni lazima wasikie kwa lazima…Kwani atakapolisikia lile neno, pengine alishakwisha kusikia mengine kama hayo 99 na hivyo hilo moja lilikuwa limesalia kufikia hatua yake ya kutafakari zaidi na kutubu…na kupitia hilo neno moja basi ataenda kukata shauri la kumpokea Bwana YESU au kuachana na mwenendo anaouendea.

Vile vile huenda hilo la kwako ndilo Neno lake la kwanza kati ya maneno 99 yanayomngojea mbele ili aokoke. Kwahiyo unaposema na kuhubiri, unakuwa umeianza safari nyingine ndani ya maisha yake, ambayo inaweza kukamilika pengine baada ya miezi au miaka baadae…

Tatizo kubwa linalotukumba wahubiri ni kuona mtu hakati shauri pale pale tunapohubiri, pasipo kujua kuwa kazi za Roho Mtakatifu ndani ya mtu hatuwezi kuzitafsiri kwa akili.

Wapo ambao wanaosikia Neno kwa mara ya kwanza, wengine ndio mara ya pili na wengine ni mara yao ya mia na ya kuokoka.

Ni wachache sana, ambao wamepewa Neema wanaweza kukata shauri la uhakika siku ile ile wanapolisikia Neno, huwa wengi wanakuwa ni mashamba yenye magugu mengi, ambao inawachukua muda kutengenezeka, wanahitaji kusikia mara nyingi, ndio maana Bwana Mungu alikuwa anawatuma manabii wake kupiga kelele katika miji na vijiji, mara nyingi sana, kwasababu ya ugumu wa mioyo.

Isaya 58:1 “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao”.

Kazi ya kuhubiri si nyepesi, ni mapambano mengi na uvumilivu mwingi, na endelevu mpaka mmoja atubu, ndio maana maandiko yanasema mmoja anapopatikana basi malaika wanashangilia.

Luka 15:10 “Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye”

Swali ni je! UMEOKOKA???.

Pengine ni wewe ndiye unayeisikia injili muda mrefu na hutaki kubadilika, hutaki kuacha udunia, hutaki kuacha kuvaa suruali mwanamke, hutaki kuacha kuvaa vimini, hutaki kuacha ukahaba na ulevi, na kiburi na usengenyaji na wivu… nataka nikutahadharishe jambo moja kuwa Injili ya kurudia rudia kwako si mfano wa yale matangazo yanayojirudia kwenye redio au Tv, bali ni ushuhuda!.

Mathayo 24:14 “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja”.

Kama umeisikia mara kwa mara na unaendelea kuidharau, utakutana nayo mbele ya kile kiti cha hukumu, na hiyo itakuhukumu, hiyo ni kulingana na biblia.

Warumi 2:16 “katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu”.

Sasa endelea kusitasita na kuwa hivyo ulivyo mpaka ile siku…haya yote unayoyasoma na kuyasikia, utayathibitisha siku ile.

Bwana atusaidie..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

IMANI NI NINI?

Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?

TUSIWE WAVIVU WA KUSIKIA.

INJILI YA MILELE NI IPI KATIKA BIBLIA?

KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments