Swali: Kuna uhusiano gani kati ya aina ya maisha anayoishi mtu na ile siku aliyozaliwa?.. Kwanini Ayubu anailaani ile siku aliyozaliwa na ule usiku ilipotungwa mimba? (Ayubu 3:1-6).
Jibu: Turejee..
Ayubu 3:1 “Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake.
2 Ayubu akajibu, na kusema;
3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.
4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.
5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe.
6 Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi”.
Sababu kuu ya Ayubu kuilaani siku aliyozaliwa ni kutokana na majaribu aliyoyapitia!.. Ya kupoteza mali zake pamoja na watumwa wake, lakini pia ya kupoteza watoto wake na zaidi sana kupatwa na magonjwa.
Hali hiyo ya mapito magumu ndiyo iliyomfanya Ayubu ailaani siku yake ya kuzaliwa… Maana ya kulaani hapo “ni kutotamani kuzaliwa”, kwamba ni “kosa kubwa limefanyika yeye kuzaliwa/kuja duniani”.
Lakini pamoja na kwamba Ayubu aliilaani siku yake ya kuzaliwa bado hakumlaani MUNGU, wala kumwazia mabaya.. ndio maana hapo anasema… “Siku hiyo (ya kuzaliwa) Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie”.. kitendo hiko cha kumhusisha MUNGU katika kauli yake hiyo ni kuonyesha Ayubu alimheshimu MUNGU.
Lakini swali ni Je! jambo hilo Ayubu alilolifanya ni sahihi? Na Je na sisi pia tunaweza kuzilaani siku zetu tulizozaliwa ikiwa tutapitia majaribu yanayofanana au kukaribia kufanana na ya Ayubu?..
Jibu ni hapana! hatupaswi kuzilaani siku zetu tulizozaliwa, vile vile Ayubu hakufanya jambo lililo jema machoni pa BWANA kwa kauli ile!.. kwani tunaona ijapokuwa Ayubu hakumlaani MUNGU kwa kinywa chake lakini kitendo pia cha kuilaani siku yake ya kuzaliwa kilikuwa ni kosa, wala haikuwa ni busara kusema vile, bali alinena pasipo maarifa, ingawa nia yake ya ndani haikuwa ovu kama ile ya mke wake..
Ayubu 35:16 “Ndiposa Ayubu hufunua kinywa chake kwa ubatili; Huongeza maneno pasipo maarifa”.
Kwahiyo alinena hayo maneno pasipo maarifa, ndio maana mwishoni tunaona baada ya kutokewa na MUNGU katika upepo wa kisulisuli na kusahihishwa alitambua makosa yake ya kuwa maneno aliyoyatoa yalikuwa yana kasoro (yasiyo na maarifa) na alitubu..
Ayubu 42:1 “Ndipo Ayubu akamjibu Bwana, na kusema.
2 Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.
3 Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? KWA MAANA, NIMESEMA MANENO NISIYOYAFAHAMU, MAMBO YA AJABU YA KUNISHINDA MIMI, NISIYOYAJUA.
4 Sikiliza, nakusihi, nami nitanena; Nitakuuliza neno, nawe niambie.
5 Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona.
6 KWA SABABU HIYO NAJICHUKIA NAFSI YANGU, NA KUTUBU Katika mavumbi na majivu”.
Umeona hapo?, Ayubu anakiri makosa aliyoyafanya ya kusema maneno asiyoyajua, na anamaliza kwa kutubu. Ikimaanisha kuwa nasi hatupaswi kusema maneno kama hayo. Kukosoa siku uliyozaliwa bado kwa namna moja au nyingine ni kumkosoa MUNGU, Hata kama hatutalihusisha jina la MUNGU katika kukosoa kwetu huko, bado hatupaswi kulaani, kwasababu kila kitu kinakuja kwa makusudi..
Ikiwa unaona unapitia majaribu mazito usiojua mwanzo wake wala mwisho wake, suluhisho si kuikimbilia siku uliyozaliwa na kuilaani, au kujijutia kuzaliwa!.. hiyo haisaidii kitu, kwani hiyo siku imeshapita na haiji tena mbeleni,.. zaidi sana badala ya kulaani, ni vizuri kutafuta kujua chanzo cha majaribu hayo ni nini, kwa kujinyenyekeza mbele za MUNGU.
Na MUNGU kwakuwa ni mwaminifu kwetu na mwenye upendo, hawezi kamwe kutuacha muda mrefu katika mitihani mkubwa wa kutokuelewa sababu ya majaribu yanayotukabili, ni lazima tu ataonyesha njia na kutufunulia sababu ya mapito tupitayo….hivyo ni suala la kujinyenyekeza tu na kumngoja BWANA, Na si kulaani…
Laiti Ayubu angejua kuwa muda mchache tu umebaki wa MUNGU kwenda kumrudishia vile alivyovipoteza mara dufu, asingesema yale maneno ya laana,… lakini tunajua alisema vile pasipo maarifa ili baadaye na sisi pia tuje kujifunza.. ma ndio maana baadaye alitubu na MUNGU akamsamehe..
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
About the author