Zaburi 22:1 Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? 2 Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati.
Maneno haya ukiyatafakari, utagundua ni ya mtu aliyefikia hatua mbaya sana ya kukaribia kukata tamaa kwasababu ya aidha magumu, au huzuni, au mateso yasiyoelekeza anayoyapitia, akiangalia kulia, haoni tumaini lolote, akiangalia kushoto haoni mkono wowote wa Mungu ukimsaidia licha ya kuomba na kulia sana, kwa muda mrefu.
Sehemu nyingine anasema, amekataliwa kila kona, amekuwa kama msikwao kwa ndugu zake.
Zaburi 69:10 Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.
11 Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao. 12 Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki. 13 Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.
14 Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji. 15 Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze, Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.
16 Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. 17 Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi.
Mwandishi huyu alikuwa ni Daudi, alipitia kipindi kirefu sana cha kujiona kama vile Mungu kamtupa, hadi kuna wakati akaona heri aende kuomba hifadhi kwa maadui zake wafilisti ambao hapo mwanzo aliwafukuza na kuwaita makafiri (wasio tahiriwa), lakini safari hii kwa unyenyekevu wote, anaenda kuwa mmoja wa askari wao, ili tu apate hifadhi, asiangamie kabisa. Huyo ni mtu ambaye maji ya shingo yalimfikia kwelikweli.
Sio kwamba alikuwa haombi, au hamlili Mungu?. Au kwamba ana dhambi kuliko wengine, mpaka awe mtu wa bahati mbaya hivyo Hapana, nyakati zote alikuwa mwombaji, lakini akafika mahali katika uhalisia wa kibinadamu aliona kama Mungu amemwacha kabisa.
Lakini kwasababu huruma za Mungu zilikuwa nyingi juu yake alimpa moyo mkuu, wa kuendelea kumngoja Bwana. Ndio maana sehemu nyingi katika Zaburi anasisitiza sana Neno hili ‘mngojeeni Bwana’ (Zaburi 37:7, 25:3, 31:24,38:15, 40:1).
Sasa moja ya maneno machache ya Daudi yaliyonikuliwa na Bwana Yesu lilikuwa ni hili.
Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha?
Mathayo 27: 45 Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa.
46 Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Je! Unadhani kauli hiyo Yesu aliyoitoa alimaanisha kweli ameachwa?
Hapana, tangu mwanzo alikuwa anajua Mungu yupo pamoja naye, na kwamba saa yake imekaribia, muda si mrefu anakwenda kuinuliwa na kutukuzwa, tena sehemu nyingine anasema alishangalia pale msalabani (Wakolosai 2:15). Lakini kuinukuu kauli ile ni kuonyesha ubinadamu wetu, unavyoweza kutuhubiria tuwapo katikati ya shida, kwamba Mungu ametuacha hususani pale tunapopitia shida, na mateso.
Yesu alinukuu ubinadamu wetu kukumbuka mfano wa yale aliyoyapitia Daudi..
Lakini tunaona dakika chache baada ya pale, pindi tu alipokata roho, makaburi yakapasuka, wafu wakatoka makaburini, pazia la hekalu likapasuka, na baada ya siku tatu akafufuka, ukombozi wetu mkuu ukapatikana, ‘Lakini ni kwa maneno ya kudhaniwa kuwa Mungu amemwacha’.
Mathayo 27:50 Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.
51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka;
miamba ikapasuka; 52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; 53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.
Ndugu, upitiapo hatua hizo ambazo mawazo yako yanakufundisha kuwa Mungu hayupo na wewe tena, amekuacha, kwasababu ya shida unazozipitia muda mrefu, magonjwa yasiyokoma, umeomba mpaka umechoka, umelia hadi ukomo,wewe ona ni kawaida,…. Piga moyo konde Mngojee Bwana. Daudi alistahimili hatimaye akathibitishwa kwenye ufalme ambao ulidumu pamoja na vizazi vyake vingi tofauti na wafalme wengine wa Israeli. Mngojee Bwana, kimaombi, kwasababu baada ya joto huja mvua.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Nzi wa Misri, na Nyuki wa Ashuru vilimaanisha nini? (Isaya 7:18-20).
About the author